Wednesday, 9 October 2013

Makada wa CCM wanaporuhusiwa kutukana jukwaani

                                                                                                                                                                                                        Salim Said Salim
KADIRI siku zinavyosonga mbele kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, hali ya kisiasa Zanzibar inazidi kuwa tete na ya wasiwasi.
Kinachoonekana ni ishara mbaya ya visiwa hivi kurudi kwenye siasa za chuki, uhasama, kutukanana, kupigana na hata kuuana.
Watu wanaopanda mbegu za chuki hawaguwsi na hawachukuliwi hatua za kisheria utafikiri wanatenda sawa.
Ni kama vile wamepewa leseni ya kuwa juu ya sheria na wanayo haki na mamlaka ya kutenda maovu kwa kutumia ndimi zao na kuandika matusi kwenye mabao ya matangazo.
Lakini wakitenda wengine ndipo hao wanaoitwa wasimamizi wa sheria wanapohangaika kufungua mashitaka ya kuwatuhumu kwamba wanahatarisha amani na utulivu.
Kunyamaziwa kimya na kutoshitakiwa kwa watu wanaofanya siasa za uhasama kunatoa tafsiri ya kuwa wanavyofanya ni sawa, wanaweza kuendelea, watalindwa na hakuna atayethubutu kuwagusa.
Hapo kwanza watu hawa walikuwa wakiporomosha matusi ya nguoni kwa viongozi wa vyama vya upinzani na serikali na wake zao.
Viongozi wastaafu wa serikali waliotofautiana nao kimawazo walikashifiwa, lakini hapakuonekana juhudi za wanaotukana kusakwa na kufunguliwa mashitaka.
Hapa ninakumbushia kwa uchungu kipeperushi kilichowakashifu marais wastaafu Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume. Mpaka leo hatujasikia kama ulifanyika upelelezi wa kuwatafuta waliofanya uhuni ule.
Siku hizi matusi ya nguoni yanamwagwa hadharani mchana kweupe na baadhi ya wakati kutangazwa moja kwa moja na vituo vya radio.
Vituo hivi havikatishi matangazo hayo, matusi, kama vile uchafu unaotoka midomoni mwa watu hawa, ni sawa na nyimbo za kuliwaza za taarabu.
Sasa watu wa kundi hili ambao ni viongozi wa CCM wamefungua ukurasa mpya wa kupalilia siasa za kibaguzi na kifashisti.
Wapo waliozungumza hadharani kuwataka watu wenye asili ya Pemba waondoke Unguja na kurudi kwao (Pemba).
Kwa kweli inasikitisha kuona hata viongozi wa serikali na CCM wenye asili ya Pemba wanabana kimya kama vile hawasikii ujumbe wa wahuni hawa na hawaoni fahari ya kuwa na asili ya Kisiwa cha Pemba.
Sijui tuseme watu hawa wameamua kukaa kimya kwa kuhofia wasipelekwe machinjioni Dodoma na kutangazwa kuwa ‘si wenzetu’au wameamua kimya kimya kuwakana wazazi wao na hawataki kuhusishwa na Pemba.
Nimesema mara nyingi na ninarudia kama yupo mtu anafanya utafiti wa matusi ya lugha ya Kiswahili au anaandika kamusi ya matusi ya Kiswahili hana haja ya kuhangaika.
Anachohitajika kufanya ni kwenda kwenye mikutano ya CCM inayofanyika Unguja na atapata kila kitu kutoka kwa viongozi wachache wa chama hiki kinachopenda amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.
Nimejenga hisia kwamba hata yakifanyika mashindano ya kimataifa ya matusi watu hawa wataipatia nchi yetu medali ya dhahabu!
Baada ya kuropokwa matusi ya nguoni watu hawa sasa wanawaandama Wapemba na Waarabu. Sijui Wapemba wanakosa gani, au kuwa wapinzani wakubwa wa CCM ndiyo nongwa?
Hapa ikumbukwe kuwa kama lugha chafu, vitisho, kupiga watu mikong’oto na kuua huibadilisha jamii iliyosema: “Hatutaki” basi Wapemba wangebadilika, lakini wanaonekana hawapo tayari kulegeza msimamo wao.
Chaguzi zinazofanyika Pemba ni kielelezo cha kuiambia CCM haitakiwi katika kisiwa hicho.
Vilevile watu wanaotukana na watoaji vitisho wanasahau kwamba viongozi wao hawakai kwa muda mrefu bila ya kwenda nchi za Kiarabu kuomba misaada na kila siku kuwaalika kuja Zanzibar Waarabu kutoka Oman na nchi za Ghuba.
Kama Waarabu si watu wazuri ni vizuri watu hawa wakawaambia viongozi wao wa CCM wasiende nchi za Kiarabu kuomba misaada.
Kama hatutaki kujidanganya inafaa tuelewe kuwa hili wimbi la kuwabagua Wapemba ni la hatari na likiachwa kuendelea halitakuwa na mwisho mwema.
Kwa kawaida binadamu huvumilia mengi, lakini uzoefu umeonesha miongoni mwa mambo ambayo watu hawapo tayari kuyavumilia ni ubaguzi.
Tumeiona hali ilivyokuwa Afrika Kusini na kwingineko, kwa hiyo si vizuri kutaka kuwa warithi wa siasa za makaburu.
Kwa muda mrefu Wapemba wamelalamika kwamba uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hawawatendei haki, wanawabagua na kuwatukana na hata kuwaita “vijibwa vya santuri”.
Vijana wa Kisiwa cha Pemba walifukuzwa shule kwa kutaka kujiandikisha kuwa wapiga kura wakati hilo halikutokea kwa wanafunzi wenye asili ya Unguja.
Ukipitia orodha ya watu waliofukuzwa kazi au nyumba zao kuvunjwa kwa sababu za kisiasa Zanzibar utaona zaidi ya asilimia 80 ya waliokutwa na uonevu huu ni Wapemba.
Nchi nyingi zilizovumilia watu kuhubiri siasa za ubaguzi, kama Rwanda, leo zinajutia.
Zanzibar ilionekana imejifunza kwa kupata kwa taabu muafaka wa kisiasa. Sasa wametokea watu wanaojifanya chakramu na kujiona wao ndio wao na wanaweza kumtukana na kumkashifu yeyote.
Hivi karibuni viongozi wa CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF walipofanya mkutano wa pamoja Zanzibar, miongoni mwa masharti waliyopewa na polisi ni kutotumia majukwaa kutukana.
Kwa hili Jeshi la Polsi linastahli pongezi kwa kuhakikisha siasa za matusi hazina nafasi katika nchi yetu. Lakini tujiulize, hao polisi hawana habari ya matusi yanayotolewa katika mikutano ya CCM?
Au ndiyo tunaambiwa wakitukana viongozi wa CCM ni sawa na kufukuza udi na kutia uturi, lakini wakifanya wengine huwa kinyume?
Kuvumilia wachache kutukana na kukashifu watu na kupandikiza mbegu za siasa za chuki na uhasama hakuitakii mema nchi hii.
Nchi yoyote ile ya kistaarabu, hasa ikiwa inajigamba kuwa na utawala wa haki na sheria haiwezi kuvumilia uhuni huu.
Hatari kubwa ninayoiona mbele ni kutokea wahuni wenye asili ya Pemba kuanza kampeni chafu dhidi ya wenzao wa Kisiwa cha Unguja.
Viongozi wa serikali, hasa wa CCM, wanapaswa kutafakari kwa makini kuhusu hali hii na kuelewa athari na hatari ya siasa hizi chafu. Ni lazima wawadhibiti wahuni wanaoharibu jina la chama chao.
Kila mtu anapaswa kutosahau Zanzibar ilikotoka, ambapo watu waliuawa na wengi kuwa vilema kutokana na siasa za chuki na uhasama.
Haikuwa kazi rahisi kwa Zanzibar kufikia hapa ilipo, lakini chochote kile ambacho hakitunzwi huharibika.
Watu huchezea mpira, karata, bao au gololi na si amani ya nchi.
Tusiruhusu wachache kuichafua hali ya amani na maelewano iliyopo Zanzibar. Balaa jingine likizuka hakuna atakayefaidika na watakaopata hasara na kujutia kuvumilia wahuni wanaopandikiza mbegu za uhasama na chuki ni watu wote wa Zanzibar.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, anapaswa kuelewa historia itakuja kumlaumu yeye zaidi na baadaye wengine kwa kuvumilia uchafu huu kama Zanzibar itarudi ilikotoka.
Kwa hili, Rais Jakaya Kikwete naye anao wajibu kama kiongozi wa taifa na Mwenyekiti wa CCM kuhakikisha anakomesha siasa za matusi, chuki na uhasama Zanzibar.
Zanzibar inaweza kujengwa kwa maelewano na si matusi na ubaguzi.

No comments:

Post a Comment