Saturday, 21 September 2013

Wapinzani wakutana na mkuu wa polisi


  • Watangaza kusitisha maandamano ya leo
  • Ni baada ya kukutana na IGP Said Mwema
Wapinzani wameufifisha moto wa kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, kwa kusitisha maandamano yalipangwa kufanyika leo.
Viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF vinavyoongoza harakati za kudai ya ushiriki mpana wa umma kutambuliwa katika muswada huo, wamekubaliana na Polisi kuhusu hatua hiyo.
Hata hivyo, pande mbili hizo zimekubaliana kuwa maandamano hayo yafanyike Oktoba 5, mwaka huu.
Wakati ikikubalika hivyo, Mkuu wa Polisi (IGP), Said Mwema, ameagiza wanachama na wafuasi upinzani waliokamatwa kutokana na kutangaza kuwapo maandamano hayo, waachiwe huru kwa dhamana.
Wenyeviti wa vyama hivyo, James Mbatia (NCCR), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema), wamefikia makubaliano hayo baada ya kukutana na IGP Mwema.
Hatua ya kusitishwa maandamano hayo imefikiwa ikiwa ni siku moja baada ya polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuyapiga marufuku.
Viongozi wa vyama hivyo walimfuata IGP Mwema, Makao Makuu ya Polisi na kushiriki kikao kilichofanyika kati ya saa 6:45 mchana hadi 10:32 jioni.
Kabla ya kukutana na Mwema, juzi viongozi hao kwa nyakati tofauti walieleza kuwa hawakubaliani na uamuzi wa Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kupiga marufuku maandamano hayo kwa madai kuwa sababu zilizotolewa na jeshi hilo hazikuwa za msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya viongozi wenzake, nje ya Makao Makuu ya Polisi, Profesa Lipumba alisema wamekubaliana na IGP Mwema kusitisha maandamano hayo.
“Tunatambua kuwa maandamano ni haki yetu ya kikatiba na tunapotaka kuyafanya, tunatoa taarifa polisi na siyo kuomba kibali, kwa hiyo maandamano ya kesho (leo) tumeyasitisha hadi Oktoba 5 mwaka huu badala yake kutakuwa na mkutano wa hadhara tu,”alisema.
Profesa Lipumba, alisema maandamano yatafanyika kwa nyakati na mahali tofauti nchini, ili kufikia lengo moja la kupinga mchakati wa muswada huo.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, yatafanyika Septemba 25 mwaka huu, baada ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa kisheria na kwamba programu za kufanya mikutano mikoani zitaendelea baada ya kufanyika maandamano ya Oktoba 5.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema mkutano huo utaanza saa 7:00 mchana na kuwataka wanachama, wapenzi na mashabiki kufika katika viwanja vya Jangwani kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Kwa upande wake IGP Mwema, alisema katika mazungumzo na viongozi hao wamekubaliana suala la kutii haki na wajibu bila shuruti ili kuifanya nchi kuwa ya amani.
Alisema katika kujenga ushirikiano mzuri na vyama vya siasa, wanachama na viongozi wa vyama hivyo waliokamatwa wakati wakitangaza taarifa za maandamano hayo wataachiwa huru kwa dhamana.
Juzi, Kova alipiga marufuku maandamano hayo kwa madai kuwa maeneo ambako yalipangwa kupita kuna mkusanyiko mkubwa wa watu ambao watakuwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, usafirishaji na mahitaji mengine ya kila siku ya kibinadamu.
Aidha, Kova alisema Polisi lilipata taarifa za kiintelijensia kuwa vyama hivyo, vimeandaa uhamasishaji mkubwa kwa watakaotumia pikipiki, guta na watembea kwa miguu.
Maandamano ya vyama hivyo vilivyoungana kupinga mchakato wa katiba, pia yalikuwa na lengo la kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete asiusaini muswada huo kwa madai kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Maandamano hayo ambayo yangewashirikisha viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo, yalipangwa kuanzia eneo la Tazara Veterani kupitia Barabara ya Mandela hadi Buguruni Sheli, Uhuru kupitia Malapa, Karume, mzunguko wa Shule ya Msingi Uhuru, Msimbazi, Fire Barabara ya Morogoro hadi viwanja vya Jangwani.
Wakati huo huo, kutoka Arusha, taarifa ya vyama hivyo vinatarajia kufanya maandamano ya amani na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara
jijini Arusha, Jumanne ijayo.
Akizungumza jana kupitia taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari, Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema maandamano na mkutano huo, ni tukio la kipekee na la aina yake kwa demokrasia ya Tanzania kushinikiza Rais asisaini muswada huo.
Alisema katika mkutano huo watatoa mambo ya msingi na yanayomuhusu kila mmoja nchini, ambaye ni Mtanzania mwenye nia njema na nchi hii kwa wakati wa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Golugwa alisema viongozi wa vyama, Freeman Mbowe (Chadema), Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR), wataongoza maandamano hayo.
Maandamano yanatarajiwa kuanza saa 6.00 mchana, eneo la Phillips na kuelekea Sanawari, barabara ya East African Community, Halmashauri, Clock Tower na barabara ya Uhuru (Sokoine), Meru Posta na Shoprite na viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro.
Alisema tukio hilo litarushwa moja kwa moja kupitia televisheni na kituo cha ITV na Radio One na vituo vya radio vilivyopo jijini Arusha.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment