JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Operesheni Kimbunga haikuondoa Wakimbizi nchini kama ilivyoripotiwa na baaadhi ya Vombo vya Habari vya hapa nchini na vya nje.
Ifahamike kuwa zoezi hili limehusisha Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) ili kuhakikisha kuwa wakimbizi hawahusishwi katika zoezi la kuondoshwa nchini.
Kwa mujibu wa tafsiri iliyotolewa na Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1951 kuhusu hadhi ya Wakimbizi, Mkimbizi ni mtu anayekimbia nchi yake kwa hofu ya maisha yake kuwa hatarini kwa sababu za kikabila, dini, utaifa, uanachama wa chama cha kijamii au kisiasa na kufuata hifadhi katika nchi nyingine.
Mkimbizi anapokimbilia katika nchini nyingine kuomba hifadhi ana haki ya kupewa hifadhi na kuhakikishiwa usalama wake. Pia ana haki ya kupokelewa na kutorudishwa katika nchi ambayo ameikimbia.
Hivyo , kutokana na Mkataba huo, Tanzania wakati inatekeleza Operesheni Kimbunga haikumgusa mkimbizi.
Aidha, ieleweke kuwa yapo mazingira ambapo hadhi ya mkimbizi hukoma pale ambapo suluhisho la kudumu la matatizo ambayo yalimfanya mkimbizi kukimbia nchi yake limepatikana na hivyo mkimbizi mwenyewe kutaka kurudi nchini kwake kwa hiari ama pale mkimbizi anapohamishiwa kwenye nchi ya Tatu kwa makubaliano maalum na pale ambapo mkimbizi anapewa uraia au ukaazi wa nchi iliyompatia hifadhi.
Hivyo basi, mkimbizi anaweza kuwa mhamiaji haramu pale ambapo hakurudi katika nchi yake kwa hiari baada ya kupatikana suluhisho kwa matatizo yaliyosababisha kukimbia ama hakupata fursa ya kwenda nchi ya Tatu na hakuomba Uraia au ukaazi wan chi iliyokuwa inampa hifadhi.
Ieleweke kuwa Mkimbizi ambaye alirudi nchini kwake kwa hiari yake na baadaye kuamua kurudi katika nchi iliyokuwa inamhifadhi hawezi kuendelea kuwa na hadhi ile ile ya ukimbizi . Mtu huyu anatakiwa kufuata Sheria ya Uhamiaji namba 7 ya 1995. Iwapo ataishi nchini bila kufuata sheria hiyo atahesabika kuwa mhamiaji haramu.
Inawezekana kuna watu ambao hadhi yao ya ukimbizi imekoma na wanaishi nchini isivyo halali wakakumbwa na Operesheni Kimbunga na kudai kuwa wao ni wakimbizi.
Juhudi za Serikali za kuwataka wahamiaji haramu kuhalalisha ukaazi nchini kwa hiari
Kwa vipindi tofauti, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji iliendesha zoezi la kuhamasisha watu wanaoishi nchini isivyo halali kurudi nchini kwao kutokana na hali ya usalama katika nchi hizo kuimarika. Aidha, kwa waliotaka kubaki na kuendelea kuishi nchini walielekezwa kufuata sheria na taratibu za Uhamiaji.
Utafiti uliofanywa na Mradi wa Kimataifa wa kushughulikia masuala ya kiuhamiaji ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unaoongozwa na Prof. Boneventure Rutinwa 2006/2007 katika mkoa wa Kagera unaonyesha kuwa Wilaya ya Karagwe pekee Inakadiriwa kuwa na wahamiaji haramu 30,850 lakini pamoja na kuhamasishwa kuhalalisha ukaazi wao, watu 2,000 pekee walifuata taratibu walizoelekezwa na Maafisa wa Idara ya Uhamiaji ili kuhalalisha ukaaji wao nchini.
Pamoja na juhudi zote za Serikali za kuhamasiha wahamiaji haramu kuhalalisha ukaazi wao nchini bado hawakufuata taratibu na badala yake utafiti unaonyesha kuwa waliendelea kuingia na kuhamia katika wilaya nyingine mfano Biharamulo na maeneo mengine.
UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA DHIDI YA WATENDAJI WA OPERESHENI KIMBUNGA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Simu: +255-22-2112035/40
|
S.L.P. 9223
| |
Nukushi: +255-2122617/2120486
Barua Pepe: ps@moha.go.tz
|
Dar es Salaam
Septemba 19,2013
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Julai 29, 2013 aliagiza kufanyika kwa opereheni maalum ya kuondoa uhalifu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita mbao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew Sukambi imeanza rasmi Septemba 6, 2013 baada ya kutoa muda wawiki mbili kwa wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari yao au kuhalalisha ukaazi wao nchini.
Wakati Operesheni hii ikifikia katika Wiki yake ya Pili, Serikali kupitia kiongozi wa Operesheni Brigedia Jenerali Mathew Sukambi inawapongeza watendaji wote wa operesheni hii kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa unyenyekevu na kiuzalendo kuhakikisha kuwa zoezi la kuondoa uhalifu na kukamata wahamiaji haramu linafanyika kwa nidhamu ya hali ya juu na mafanikio.
Aidha, kumekuwepo na tuhuma mbali mbali zinazotolewa kupitia Vyombo vya Habari ambazo hazina ukweli.
Tuhuma za rushwa dhidi ya watendaji wa Operesheni Kimbunga
Operesheni Kimbunga inahusisha watendaji kutoka vyombo mbali mbali nchini vikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU), Idara ya Usalama wa Taifa, Idara ya wanyamapori na taasisi nyingine za serikali.
Mazingira ya kazi ya kuwakamata wahamiaji haramu na kuwahoji ili kuthibitisha uraia wao ni ya wazi hayawezi kuruhusu watendaji kuweza kupokea rushwa kama ilivyoripotiwa na Gazeti moja hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria.
Hata hivyo, wananchi wanapaswa kufahamu kuwa iwapo kuna mtendaji wa operesheni hii ameomba na kupokea rushwa wanakiuka sheria, hivyo ni vyema kama kuna mtu mwenye ushahidi wowote atoe taarifa kwenye ofisi za TAKUKURU zilizopo mikoani na Wilaya zote nchini.
Zoezi la Operesheni Kimbunga halilengi kunyanyasa wazee, watoto na wanawake wasio Raia walioolewa na Watanzania
Operesheni Kimbunga haikulenga kuwanyanyasa Wazee, Wanawake walioolewa na watoto wao wadogo wanaoishi nchini bila kufuata Sheria ya uhamiaji.
Kuna waliokuwa Wakimbizi 36,000 kutoka nchi ya Rwanda walioingia nchini miaka ya 1959 hadi 1961 waliokuwa wakiishi katika mkoa wa Kagera katika maeneo ya Kimuli, Nkwenda, Mwase na maeneo mengine ambao walipewa uraia wa Tanzania kwa tajinisi mwaka 1983 isipokuwa watoto wao kwa kuwa wazazi wao hawakuwaombea uraia huo. Raia hao 36,000 waliopewa uraia wa tajinisi hawakuguswa na operesheni hii kwani ni watanzania isipokuwa watoto wao ambao hawakuombewa uraia na wanaishi nchini bila hadhi yeyote ya kiuhamiaji.
Pia kuna raia wa kigeni waliokuwa wanaishi bila kufuata sheria za uhamiaji na Uraia ambao zamani walikuwa wakimbizi lakini hadhi ya ukimbizi iliondolewa baada ya nchi zao kuwa salama na kutakiwa kurudi.
Hata hivyo, kama mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete alivyoagiza kuwa zoezi lifanyike likiwa na sura ya kibinaadam pale inapobidi, raia hao wa kigeni waliokuwa wanaishi nchini bila kufuata sheria hususan wazee wameruhusiwa kubaki na kusaidiwa kufuata taratibu ili kuhalalisha ukaazi wao.
Aidha, ieleweke kuwa kuzaliwa Tanzania pekee hakumpi mtu haki ya kuwa Raia moja kwa moja mpaka taratibu nyingine zifuatwe. Kuna watoto walizaliwa Tanzania na Raia wa nchi za nje waliokuwa wanaishi nchini kabla ya kupatiwa uraia. Hao hawawezi kuwa raia moja kwa moja mpaka taratibu za kisheria zifuatwe.
Aidha, Operesheni Kimbunga haikulenga kuvunja ndoa na kusambaratisha familia. Lengo ni kuondoa wahamiaji haramu.
Wanawake walioolewa na Watanzania wametakiwa kujiorodhesha ili kupatiwa utaratibu wa ukaaji wao. Wanaume walifunga ndoa na Watanzania wanatakiwa kurudi katika nchi zao na wake na watoto wao na kwa wanaotaka kuishi nchini wanatakiwa kuomba vibali vya kuishi kwa kufuata sheria na taratibu za uhamiaji.
Operesheni Kimbunga haikulenga kuondoa wahamiaji haramu kutoka Taifa moja
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Operesheni Kimbunga inayoendelea katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita hailengi kuondoa wahamiaji haramu kutoka taifa moja na hadi Septemba 20, 2013, imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 9,283 toka nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Somalia, DRC Congo, Yemen na India.
Idadi kubwa ya wahamiaji hawa haramu waliokamatwa ni kutoka Burundi (5,355) wakiafuatiwa na Rwanda (2,379), Uganda (939), DRC Congo (564), Somalia (44), Yemen (1) na India (1).
Takwimu zinaonyesha kuwa mkoa wa Kigoma unaongoza kwa idadi kubwa ya wahamiaji haramu waliondoshwa nchini ikiwa na jumla ya wahamiaji haramu (4,365) ukifuatiwa na mkoa wa Kagera wenye ambapo walikamatwa wahamiaji haramu (4,335) na Geita (583).
Operesheni Kimbunga ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyokithiri vikiwemo ujambazi wa kutumia silaha,ujangili, utekaji wa magari na mauaji ya kikatili pamoja na migogoro ya ardhi inayotokana na wafuagaji kutoka nchi jirani kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho.
Aidha, jumla ya wahamiaji haramu 3,238 waliondoshwa nchini kwa amri ya Mahakama baada ya kupewa hati ya kufukuzwa nchini wakati wananchi wengine 1,108 waliokuwa wanachunguzwa kama kweli ni raia wa Tanzania waliachiwa huru baada ya watendaji kuthibitisha kuwa ni raia halali wakati huo huo wengine 1,303 wakiwa wanaendelea na uchunguzi ili kuthibitisha uraia wao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Julai 29, 2013 aliagiza kufanyika kwa opereheni maalum ya kuondoa uhalifu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita mbao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew Sukambi imeanza rasmi Septemba 6, 2013 baada ya kutoa muda wa wiki mbili kwa wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari yao au kuhalalisha ukaazi wao nchini.
No comments:
Post a Comment