Monday, 27 June 2011

Madawa ya kulevya ni tatizo

Na Salma Said
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Fatma Abdul-habib Fereji akibadilishana mawazo na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman nje ya ukumbi wa Baraza la wawakilishi leo muda mfupi baada ya kumaliza kuwasilisha hutuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha wa 2011-2012 ya wizara yake ndani ya baraza la wawakilishi.
UKIMWI NA MADAWA NI TATIZO ZANZIBAR
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej amesema tatizo la madawa ya kulevya pamoja na ukimwi ni janga la taifa ambapo jamii inatakiwa kupambana na kuliondosha tatizo hilo ambalo linaharibu nguvu kazi ya taifa.
Ferej alisema hayo katika kikao cha baraza la wawakilishi wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya ofisi ya makamo wa kwanza wa rais kwa mwaka wa fedha 2011-2012.
Alisema ukimwi umekuwa ukipunguza na kuathiri nguvu kazi ya taifa kutokana na ugonjwa huo ambao hauna tiba wala kinga kwa sasa tangu ulipoingia nchini katika mwaka 1985.
Ferej alisema katika kupambana na ukimwi Tume ya ukimwi inatarajiwa kutekeleza mpango wa awamu ya pili ya kupambana na ukimwi kwa mwaka 2011-2012 ikiwemo kuzishirikisha sekta mbali mbali ikiwemo za binafsi.
Alisema sekta binafsi mchango wake kwa jamii ni mkubwa sana na kama itatumiwa vizuri basi mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi pamoja na vita dhidi ya mapambano ya madawa ya kulevya yatafanikiwa.
Aidha alisema katika mpango wa awamu ya pili ya kupambana na ukimwi,Tume ya ukimwi itavitumia vyombo vya habari kwa ajili ya kuwasilisha mawasiliano kwa jamii katika mapambano ya ukimwi.
Katika kupambana na madawa ya kulevya Zanzibar,Ferej alisema serikali ipo katika hatua za kuandaa sera ya madawa ya kulevya pamoja na kuwasilisha mswada wa marekebisho ya sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar katika ngazi mbali mbali.
Aidha Ferej alipongeza jumuiya zisizokuwa na serikali NGO ambazo zinajishungulisha na mapambano ya madawa ya kulevya ikiwemo za makaazi na marekebisho ya vijana wanaoacha matumizi ya madawa ya kulevya.
Alisema huduma hizo za makaazi kwa kiasi kikubwa zimesaidia vijana kuacha matumizi ya madawa ya kulevya baada ya kupata mawaidha na mafunzo juu ya athari za madawa ya kulevya kwa jamii.
Mapema Ferej alisema kwamba hivi sasa Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira katika maeneo mbali mbali ikiwemo baharini pamoja na nchi kavu.
Alisema tatizo la uharibifu wa mazingira wa kuchota mchanga,ukataji miti pamoja na uharibifu wa mazingira kwa kukata mawe,hivi sasa umechukuwa kasi kubwa katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Fereji aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba kumekuwa na uharibifu wa mazingira kwa kuvua samaki aina ya kasa katika bahari ya zanzibar,hali ambayo inatisha kutoweka kwa samaki hao.
Alisema utafiti uliofanywa katika mwambao wa pwani kwa vijiji vipatavyo 8,ikiwemo Nungwi,Chwaka,Uroa pamoja na Fumba,Chukwani na Bumbwini inaonesha kwamba asilimia 53 ya watu waliohojiwa wamesema mazalia ya kasa yapo hatarini.
Mazalia ya kasa yapo hatarini kutokana na kuwepo kwa kasi ya ujenzi wa mahoteli katika mwambao wa pwani,hatua ambayo inawafanya kasa kushindwa kufika nchi kavu kwa ajili ya kutaga mayai.
Waziri huyo alisema serikali ya mapinduzi ya zanzibar imeadhamiria kuimarisha huduma za watu wenye ulamavu ili kuona kwamba wanaishi katika mazingira mazuri sawa na watu wasiokuwa na ulemavu kwa kuwa haki ya kuishi ni kwa watu wote.
Fereji alisema katika idara ya ulemavu tayari imetayarisha mfumo wa kumbukumbu kwa watu wenye ulemavu kwa sheria zipatazo 65 za mkoa wa kaskazini Unguja ili kujuwa takwimu halisi za walemavu waliopo visiwani hapa.
Aidha alisema idara ya walemavu inakusudia kutayarisha mifuko mbali mbali ya watu wenye ulemavu ambayo itasaidia kuondokana na tatizo la umasikini ambalo linawakabili watu wenye ulemavu Unguja na Pemba.
Waziri Fereji kwa mwaka wa fedha 2011-2012 ameliomba baraza la wawakilishi kuidhinisha jumla ya sh.1,573,000,000 kwa mwaka wa fedha ambapo kati ya fedha hizo jumla ya sh.1,493,000,000 kwa kazi za kawaida na jumla ya sh.155,000,000 kwa kazi za maendeleo.
KIKOSI CHA UOKOVU NA ZIMAMOTO
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inakusudia kuimarisha kikosi cha uokovu na zimamoto Zanzibar kwa ajili ya kuweza kutekeleza majukumu yake ikiwemo kutoa huduma mbali mbali za majanga ikiwemo moto.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame wakati akijibu swali aliloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Chaani (CCM) Ussi Jecha Simai aliyetaka kujuwa mikakati ya serikali katika kuimarisha kikosi hicho.
Makame alisema kwamba kikosi hicho kinakabiliwa na majukumu makubwa katika kutoa huduma zake kwa majanga mbali mbali ikiwemo moto,hivyo kinatakiwa kupewa huduma mbali mbali ikiwemo vifaa.
Alisema kwa sasa kikosi cha zima moto na uokovu kinashirikiana na vikosi vya taasisi mbali mbali vinavyotowa huduma kama hizo ikiwemo kikosi cha KMKM, pamoja na shirika la bandari.
Aidha alisema kwa sasa serikali ipo katika hatua za kukipatia kikosi cha zima moto na uokovu boti za kisasa kwa ajili ya kukabiliana na kutoa huduma mbali mbali wakati yanapotokea majanga makubwa kama moto.
Kwa mujibu wa sheria kifungu cha 4 cha sheria nambari 7 ya mwaka 1999, idara ya zimamoto na uokovu ndiyo chenye majukumu ya kuzima moto na kuokoa maisha ya watu na mali zao hapa Zanzibar.
Alisema kikosi hicho kwa sasa ndiyo tegemeo katika kukabiliana na majanga hayo visiwani hapa ambapo kimekuwa kikipambana na majanga kama moto, kuokoa maisha ya watu wanaozama baharini au kuingia katika visima.
Waziri huyo alisema serikali inaona upo umuhimu wa kuwepo kwa boti za kisasa kwa kikosi hicho cha zimamoto ambapo suala hilo serikali italishughulikia kwa kuwa kinategemewa sana katika kukabiliana na majanga mbali mbali.
SMZ KUDHIBITI BIDHAA MBOVU
Serikali ya mapinduzi ya zanzibar imesema sheria ya kuanzishwa kwa taasisi ya viwango ya Zanzibar imekamilika na kwa sasa inasubiri kupata baraka za rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein.
Hayo yalisemwa na naibu waziri wa biashara,viwanda masoko Thuwayba Edington Kisasi wakati akijibu swali aliloulizwa na mwakilishi wa jimbo la Rahaleo (CCM) Nassor Salim Ali aliyetaka kujuwa mikakati ya wizara kudhibiti bidhaa mbovu zilizopitwa na wakati.
Kisasi alisema kwamba sheria hiyo ambayo imepitishwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi imekamilika ambayo miongoni mwa mikakati yake ni kudhibiti uingizaji wa bidhaa zilizopitwa na wakati ili kuepuka kuifanya Zanzibar kuwa jaa la taka ‘dampo’.
“Mheshimiwa spika serikali imeaandaa sheria ya kusimamia viwango na ubora wa bidhaa ambayo inakusudia kuanzishwa kwa taasisi ya viwango ya Zanzibar taasisi hiyo itadhibiti bidhaa zilizopitwa na wakati zenye kiwango kidogo cha ubora”alisema Kisasi.
Wajumbe wa baraza la wawakilishi waliridhia na kupitisha mswada katika baraza la wawakilishi katika kikao cha mwezi wa Januari mwaka huu hatua ambayo itadhibiti uingizaji wa bidhaa zilizopitwa na wakati pamoja na bidhaa ziliopo chini ya ubora.
Waziri wa ofisi ya makamu wa kwanza wa rais Zanzibar Fatma Abdulhabib Fereji alisema kwamba Zanzibar inakabaliwa na tatizo la kuwepo kwa bidhaa chakavu zikiwemo za elektroniki kama redio na televisheni ambazo nyingi hazina viwango vinavyokubalika hasa katika kipindi kile ambacho hakukuwa na sheria.
Alisema kanuni ya kudhibiti bidhaa hizo ipo katika hatua za mwisho za kupitishwa katika vyombo vinavyohusika kwa ajili ya utekelezaji wake na kuona kwamba Zanzibar haigeuzi tena kuwa jalala la kuingizwa bidhaa mbovu.
‘Tumegunduwa kwamba zipo bidhaa nyingi za elektroniki zinazoingizwa nchini kama redio na televisheni ambazo kwa kweli hazina viwango vinavyokubalika lakini kanuni ya sheria inatayarishwa ambayo itadhibiti uingizaji wa bidhaa hizo ikishamalzia suala hili litapungua kwa kuwa tutakuwa tayari tuna sheria maana tulikuwa hatuwezi kudhibiti kwa kuwa hatukuwa na sheria hiyo” alisema waziri huyo.

No comments:

Post a Comment