Kuchukuwe fani ya sayansi
Na Salma SaidMaalim Seif alisema ni vyema wanafunzi wenyewe kuhimizana na kusaidiana katika suala hilo ili kukidhi mahitaji ya Serikali ipate wataalamu wa kutosha kwani wanafunzi wengi wamekuwa wakikwepa kuchukua masomo ya sayansi kwa kisingizio kuwa ni magumu.
Maalim Seif ametoa changamoto hiyo katika ukumbi wa Hoteli ya Bene mjini Morogoro, katika hafla ilioandaliwa na Jumuiya ya ZAMUMSA (Zanzibar University of Muslim Sudents Association), inayowashirikisha wanafunzi kutoka Zanzibar walio katika ngazi na fani mbali mbali za masomo ya chuo hicho.
Wahitimu hao katika kiwango cha shahada ya kwanza katika fani za Elimu na Mass Communication wanatarajiwa kumaliza rasmi masomo yao ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Julai, 2011 ambapo walitakiwa kujitahidi na masomo na kuelewa lengo lililowapeleka huko chuoni na kuachana na vishawishi vyovyote ambavyo vitapunguza ari yao ya masomo.
Makamu wa kwanza amesema suala la kuacha masomo ya sayansi inatokana na tatizo la msingi linaloikabili Zanzibar ambapo wahitimu wake wengi ni wale waliojikita katika masomo ya sanaa (art), hali inayoongeza idadi ya wasomi wanaobaki bila ya kuajiriwa, hususan katika sekta ya elimu, baada ya Wizara hiyo kusheheni wahitimu wa kada hiyo.
Aidha aliwataka wahitimu hao kulipa uzito unaostahili suala hilo kwa kuzingatia ushindani uliopo mbele yao katika soko la ajira, hususan pale Jumuiya ya Afrika Mashariki itakapoanza kufanyakazi rasmi na kuwataka kujikita katika elimu ambayo itatoa ushindani.
Maalim Seif aliwataka wahitimu hao kuwa na kiu ya kujiendeleza kwa kutumia vyema fursa ziliopo chuoni hapo pamoja na Chuo kikuu huria Tanzania ili kujiongezea maaifa na elimu kwani elimu ndio msingi wa maisha na pia ni kitu pekee muhimu ambacho kitakachomsaidia binaadamu katika dunia kwa kuwa mtu anapokuwa na elimu yake haiwezekani kumuazima mwengine.
.
Akizungumzia changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya elimu Zanzibar na zinazopelekea kuzorotesha maendeleo yake, Maalim Seif alisema Serikali inalitambua suala hilo na imejipanga vyema kukabiliana na changamoto hizo, kwa kuongeza kiwango cha mishahara ya wafanyakazi kuambatana na kwiango cha elimu, uzoefu na utendaji pamoja na kuhakikisha inalipa maposho na haki nyingine za msingi.
Alisema hatua hiyo pia inalenga kuondokana na tatizo la kukimbiwa an wataalamu wake kwa kile kinachodaiwa maslahi duni.Kuhusiana na tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu Zanzibar, Maalim Seif alisema linatokana an sababu kadhaa, ikiwemo ya ukosefu wa walimu wenye uwezo wa kutoa elimu bora itakayomuwezesha kijana wa Kizanzibar akimaliza masomo yake kumudu kufanya kazi mahala popote pale Afrika Mashariki.
Alisema ni mipango ya Serikali ya Zanzibar kuzipatia skuli zake vifaa vyote ikiwemo vitabu na Maabara ili kuwawezesha wanafunzi kuendana an wakati uliopo wa Sayansi na Teknolojia.Alisema pia Serikali inalenga kujenga madarasa zaidi ili wanafunzi waondokane na hali iliopo hivi sasa ya kurundikana idadi kubwa katika darasa moja, hatua inayowafanya walimu kushindwa kutoa elimu bora.
Aidha alisema moja ya changamoto kubwa inayoikabili Wizara ya Elimu ni kuwa na mitaala na vyuo vya Ufundi katika kila Wilaya za Unguja na Pemba.Alisema ni jambo la kusikitisha kuona skuli za Zanzibar zinashika mkia katika mitihani ya Kitaifa kidato cha nne na sita kila mwaka, na kuiacha skuli ya SOS pekee ikifanya vizuri kwa kile kinachoonekana kuwepo katika mazingira mazuri.
Katika hatua nyingine Maalim Seif aliwataka wahitimu hao watarajiwa kuwa wazalendo na kurudi nyumbani kulitumikia Taifa badala ya kuendekeza fedha mbele na kwenda nje ya visiwa hivyo kufanyakazi.Aliwataka kufahamu wajibu wao mkubwa katika kuliendeleza mbele Taifa na kurejea nyumbani kuwasaidia ndugu zao wanaokabiliwa na matatizo mbali mbali ya kijamii.
Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Kusini Pemba Mohammed Habibu Mnyaa, aliwataka wahitimu hao kuondokana na dhana potofu kuwa ajira ni ile itokanayo na Serikali pekee na badala yake kuangalia umuhimu wa elimu na kuibua njia za kujiajiri.
Mbunge huyo aliitupia lawama Bodi ya Mikopo Tanzania kwa kujenga mazingira yanayowafanya wasichana kujiingiza katika vitendo vya uasharati kutokana na udhaifu wa bodi hiyo, huku Serikali ikipaza sauti kupambana na ugonjwa wa ukimwi.
Katika kuchangia mtaji wa Jumuiya hiyo, Mbunge huyo kwa niaba ya wabunge wenzake kutoka Zanzibar alichangia shilingi Milioni mbili, kuendeleza miradi mbali mbali iliyolengwa kuanzishwa.
Mapema katika risala yao wahitimu watarajiwa, walimweleza Makamu wa kwanza wa Rais, juu ya hali ya elimu Zanzibar na mustakbali wake na kuainisha matokeo mabaya kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita.
Wakitolea mfano walisema katika mwaka wa 2011, ni wanafunzi watatu tu ndio waliofanikiwa kupata kiwango cha daraja la kwanza kisiwani Pemba, huku kutoka Unguja kukiwa na wanafunzi sita pekee kutokana maelfu ay watahiniwa wa kidato cha sita.
Aidha walilamikia ucheleweshaji wa ajira mpya kwa wahitimu wa vyuo, maslahi duni kwa wafanyakazi, uhaba wa nyenzo katika sekta ya elimu, kushuka maadili kwa wafanyakazi pamoja na kuitaka serrikali kuuboresha mfuko wa elimu Zanzibar.
Jumla ya wahitimu 93 wanatarajiwa kumaliza masomo yao,ikiwa ni muhula wa nne wa chuo hicho, ambapo kati ya wanafunzi hao asilimia 40 ni kutoka Zanzibar, huku wahitimu 50 tayari wakiwa wameshajaza fomu za kuomba ajira katika sekta tofauti Tanzania Bara.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na watu mbali mbali, wakiwemo wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya MUM, Mzumbe, UDSM, UDOM pamoja Wabunge mbali mbali wakiwemo wale wanaotoka Zanzibar.
No comments:
Post a Comment