Mbunge akichokonoa tena Muungano
HOJA kuhusu Muungano imeibuka upya bungeni baada ya Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa, kulieleza Bunge kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, bado una matatizo mengi. Akichangia hotuba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge ya mwaka katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, mbunge huyo alisema Muungano bado una utata unaopaswa kushughulikiwa haraka. "Mheshimiwa Spika, wakati rais akitoa ufafanuzi kuhusu suala la Muungano alieleza kuwa Zanzibar ni nchi ndani ya nchi ya Tanzania lakini, Nje ya Tanzania nchi ni Tanzania. Lakini mheshimiwa spika, mpaka leo vitabu hivi, bado vinaitambua Zanzibar kuwa ni mkoa kama ulivyo wa Kilimanjaro," alisema mbunge huyo. "Mbona vitabu havitaki kubadilisha hilo ili Zanzibar isomeke kuwa ni nchi kama rais alivyosema, huu ni mzozo Zanzibar kuonekana kama mkoa na sisi (Wazanzibari), hatutaki," alisisitiza. Mbunge huyo alisema mbali na tatizo hilo la msingi, kero za Muungano bado ni tatizo ambalo halijapatiwa ufumbuzi na kwamba hali hiyo ni hatari kwa vizazi vya sasa na vijavyo. "Mmetaja serikali vikao vya urafiki mwema vya wizara, vikao vya Muungano mmekaa vingapi,"alihoji Kwa mujibu wa Mbunge huyo, Tanzania Bara inainyonya Zanzibar katika mambo mengi ikiwamo mgawo fedha zitokanazo na gesi, jambo hilo linalopaswa kutatuliwa haraka kwa kuwa halikubaliki. "Tulipoulizwa kuhusu fedha za gesi ziko wapi, mkasema ziko Hazina. Zanzibar ina serikali yake na viongozi wake kwa nini fedha ziende hazina na sio kuigawia Zanzibar sehemu yake. Tumesema mambo 22 yaliyoko kwenye Muungano ni mengi na tunataka yapunguzwe," alisema mbunge huyo. Alisema tofauti ya idadi ya watu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, ni tatizo lingine linaloleta tofauti ya mgawo wa rasilimali zilizopo nchini na namna pekee ya kuondokana na tatizo hilo, ni Zanzibar kutambuliwa kama nchi ndani ya Tanzania kama alivyosem rais. "Wenzetu mmetuendea kinyume, sisi tuko 1.5 tu na wenzetu huku (bara) mko zaidi ya milioni 40. Kwa nini mnatuhadaa kuiua JKU ili wote tuwe na JKT, Mngetuacha wenyewe (Zanzibar) tungekuwa mbali. Msitudanganye, hatuwezi kukubali kuipoteza nchi yetu,"aliendelea. "Muungano ni muhimu, mimi nilishazaa hapa bara (Tanzania) sasa wakati waziri anahitimisha hoja yake, nataka nisikie anasema chochote kuhusu hilo, sitaki nije kurudia tena hoja hii humu bungeni. Nasema siungi mkono hoja hii kwa sababu ya matatizo haya." Katika hatua nyingine Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi, alitumia muda wake mwingi kwenye mjadala huo kuitaka serikali ianze utaratibu wa kuwalipa mishahara madiwani, ili kuwapunguzia ugumu wa maisha. "Madiwani ni muhimu sana katika maendeleo ya taifa, leo tumo humu (bungeni) wenzetu wanaendelea na kazi huko. Naomba serikali iwalipe Sh500,000 kwa mwezi na wenyekiti wa serikali za mitaa walipwe Sh60,000,"alisema. |
No comments:
Post a Comment