Waziri Sitta anguruma
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wiki iliyopita kilihitimisha ziara yake ya maandamano na mikutano ya hadhara katika mikoa na wilaya za Kanda ya Ziwa kikiishinikiza Serikali kutoilipa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans Sh. bilioni 94.
Mbali na hilo, pia Chadema kiliendesha maandamano hayo kwa ajili ya kuishinikiza Serikali kushusha bei ya umeme, kupinga kupanda kwa gharama za maisha na kupinga uchaguzi wa Meya wa Arusha, ambao unadaiwa kujaa mizengwe.
Baada ya ziara hiyo, Serikali ilikishutumu chama hicho kuwa maandamano yake ni ya kuwachochea wananchi waichukie na kukitishia kuwa itafika mahali serikali itakosa uvumilivu.
Kauli hizo zilitolewa kwa nyakati tofauti na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita kwa taifa, ambaye alisema kauli za viongozi wa Chadema ni hatari kwa amani ya nchi na kwamba zinalenga kuifanya nchi isitawalike.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, alidai kauli za uchochezi katika maandamano ya Chadema yatailazimisha serikali kukosa uvumilivu.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alirudia kauli ya Wasira akiwa ziarani mkoani Kagera kuwa itafika mahali serikali itakosa uvumilivu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, Sitta aliitaka Serikali kuwa nyepesi kwa kujirekebisha na kuwachukulia hatua viongozi wake ambao ni kero kwa wananchi.
Alisema viongozi hao ni wale wanaojinufaisha wenyewe pamoja na familia zao badala ya kuwatumikia wananchi.
Sitta ambaye alikuwa anahudhuria mkutano wa Afrika Mashariki, alisema Serikali inatakiwa kutambua kuwa vyama vya upinzani vipo na vimejiimarisha kwa kutaka kuiondoa madarakani.
Hata hivyo, alisema ndani ya Serikali iliyopo madarakani, kuna viongozi wazuri wanaokubalika kwa wananchi.
“Serikali hata siku moja isitegemee wapinzani wataongea lugha nyepesi, wapinzani sio rafiki zetu na kamwe hawawezi kutuonea huruma ila kinachotakiwa ni kujirekebisha haraka na kuwa wepesi wa kukubaliana na mambo,” alisema Sitta na kuongeza:
“Mfumo wa vyama vingi hauendelezi ukiritimba wa chama kimoja japo ilizoeleka kuwepo kwa chama kimoja, sasa wanatakiwa kushindana kwa hoja.”
Alisema Serikali iwe na kawaida ya kuchukua hatua za haraka pale jambo linapotokea badala ya kukaa muda mrefu bila ya kutoa maamuzi na kuwafanya wananchi kuwa na wasiwasi.
Aidha, Waziri Sitta alisema viongozi waliopo madarakani wanatakiwa kuachana na tabia ya kutumia vyeo vyao kuendeleza biashara zao, jambo ambalo alisema hata Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alilikemea kwa lengo la kuhakikisha watu wote kuwa sawa.
Alisema anashangaa kiongozi ambaye ni Mbunge na ni mfanyabiashara mwenye biashara kubwa anapata wapi muda wa kufanyabiashara hiyo kama sio kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuendeleza biashara zake.
Alisema kuwa anaamini kuwa wakati umefika kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete, kuchukua hatua.
Alisema Rais Kikwete hawezi kuyaacha mazuri ya CCM yakayeyuka bila sababu.
Alisema anaamini kuwa viongozi wa kitaifa watahakikisha imani kwa CCM inaendelea kuwepo kwa kuwa bado kina mashabiki wengi wanaokipenda ila wanakwazika wanapowaona viongozi wao wanachelewa kuchukua hatua.
Akizungumzia vuguvugu la kisiasa lililopo nchini, Sitta alisema sio busara kwa wapinzani kuhubiri habari za kumwaga damu na kuwataka wananchi kulinganisha wapinzani na serikali iliyopo madarakani kwa kuhoji kama itaweza kuwa serikali mbadala badala ya ile iliyopo madarakani ya CCM.
Alisema ana matumaini makubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015, CCM itaendelea kuwa madarakani kwani chama hicho bado kina hazina kubwa na watapatikana viongozi wazuri watakaoweza kuongoza.
No comments:
Post a Comment