Wednesday, 9 March 2011

Katiba mpya itamaliza Ukandamizaji-Kombani



Na Agnes Mwaijega
WAZIRI wa Sheria na Katiba Bi. Celina Kombani, amesema atahakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kutengeneza katiba mpya ili kuondoa dosari
 zinazochangia kuwakandamiza.
Amesema ili kufikia hatu hiyo wanawake wanatakiwa kupitia katiba iliyopo sasa ili kuwawezesha kupata muongozo sahihi ya mambo muhimu wanayohitaji.

Waziri Kombani alisema hayo Dar es Salaam jana kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya mwanamke duniani yaliyoandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF).
Alisema nafasi za wanawake zimeongezeka kwa asilimia kubwa na kwamba serikali inathamini mchango wao katika ngazi mbalimbali za uongozi kitaifa na kimataifa.

"Ni dhairi kwamba serikali inawapa kipaumbele wanawake, ndiyo maana idadi yao inaendelea kuongezeka kila siku katika nafasi za uongozi.
"Sasa hivi wanawake majaji ni wengi ukilinganisha na miaka ya nyuma," alisema Bi.Kombani.
Aliwataka wanawake waliopewa nafasi za uongozi kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kuwapatia fursa wengine.
Alisema Tanzania imekuwa mstari wa mbele  kuadhimisha siku ya mwanamke kwa kuzijali shughuli mbalimbali zonazofanywa na kundi hilo.

Alitoa mwito kwa watanzani kuhakikisha wanatoa kipaumbele na fursa ya elimu kwa watoto wa kike nchini.
Naye Mkurugenzi wa WiLDAF Bi.Judith Odunga, aliitaka serikali kuboresha fursa sawa katika ngazi zote za uongozi, kufuta sheria mbovu za mirathi, kuwalinda wanawake dhidi ya ukatili na kutoa mitaji mikubwa kwa kundi hilo ili waweze kujikomboa kiuchumi.

No comments:

Post a Comment