Wednesday, 9 March 2011

Sumaye amshangaa Tambwe

*Asema viongozi maslahi wasio na historia wanaiua CCM
*Asisitiza kauli zake ni taratibu hazihitaji vikao
*Sitta ataka CCM isishangae kukosolewa na wapinzani


Na Mwandishi wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaathiriwa na viongozi maslahi wasio na
 upeo wa kujua yale wanayosema yanakisaidia au kukiangamiza chama hicho katika siasa za ushindani wa vyama.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu kauli zilizotolewa dhidi yake na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa CCM, Bw. Hiza Tambwe.

Bw. Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), alisema baadhi ya viongozi waliopewa madaraka hawana historia na chama hicho na hawaelewi namna kauli zao zinavyokiathiri chama jambo ambalo sasa ni kero kwa wanachama na watu wenye uchungu wa kweli na CCM.

"Baadhi ya watu wanaokisemea chama sasa hawana historia na CCM, hawana upeo wa kujua yale wanayoyasema yanasaidia au kukiumiza vipi chama. Hii ni kero ndani ya chama hususani kwa watu wenye uchungu wa kweli na CCM," alisema Bw. Sumaye.
Hivi karibuni Bw. Sumaye alikaririwa na gazeti moja akikishauri chama chake kusimama kukabili hoja mbalimbali zinazotolewa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) badala ya kuiachia serikali peke yake kufanya hivyo.

Bw. Sumaye alionya kwamba si sahihi kwa CCM kukaa kimya wakati wapinzani wanaishataki kwa wananchi kuwa imeshindwa kazi, hivyo makada wa chama hicho wanapaswa kuchukua jukumu hilo haraka.
Kufuatia kauli hizo, Bw. Tambwe alikaririwa na gazeti jingine akimshambulia Bw. Sumaye kuwa kauli zake hazikuwa za kiungwana na zililenga kukishambulia chama hicho.

Alidai kwamba kauli hizo zililenga kujenga chuki miongoni mwa wanaCCM na ni chokochoko zinazotolewa na watu wenye nia ya kuwania urais mwaka 2015. Aliongeza kuwa si sahihi kwa mawaziri wakuu wastaafu kutoa ushauri barabarani kwani huko si kukijenga chama bali ni kukibomoa.

Akijibu hoja hizo Bw. Sumaye alisema alichoshauri ni taratibu za kawaida za chama ambazo hazihitaji kikao kwani siku zote CCM inapokuwa na jambo viongozi hufanya mikutano ya ndani na nje kuuhamasisha na kuuelimisha umma.

"Ni taratibu za kawaida za chama, wala hazihitaji kikao kwa sababu siku zote kinapokuwa na jambo viongozi hufanya mikutano ya ndani na nje, kuhamasisha na kuelimisha umma," alisema Bw. Sumaye na kuongeza;
"Nilichosema mimi hii kazi wanayofanya CHADEMA ni kuhamasisha umma na kazi ya siasa na viongozi wetu (wa CCM) katika ngazi mbalimbali wafanye vikao na kuelimisha umma. Hili kweli linahitaji mpaka nilisemee kwenye vikao?" alihoji Bw. Sumaye.

Alizidi kueleza," Nilitegemea Idara ya Propaganda iwe mbele badala ya kupambana na sisi tunaotoa ushauri mzuri kwa chama chetu, iandae utaratibu mzuri kuanzia ngazi za chini namna ya kuhamasisha na kuelimisha umma. Nashangaa sana Mkurugenzi wa Propaganda kusema navuruga chama, eti namtwishwa gunia la misumari mwenyekiti!

"Nilichofanya ni kumpunguzia kazi mwenyekiti wetu. Nataka viongozi wengine wa chama chetu wafanye mikutano ya siasa. Kumwachia mwenyekiti pekee ajibu hoja kwenye hotuba zake si sahihi, chama kimsaidie hiyo ndiyo kazi ya viongozi ndani ya chama.

"Kimsingi sioni kosa nililofanya. Nashauri Idara ya Propaganda ijipange katika ngazi mbalimbali za chama kujibu hoja hizi za CHADEMA zinazochafua chama chetu," alisema.

Akizungumza kwa kujiamini Bw. Sumaye alisema hakudandia ndani ya CCM, historia yake ndani ya chama hicho ni ndefu kwani aliingia Umoja wa Vijana wa TANU mwaka 1969 akiwa sekondari Ilboru na mwaka 1972 alijiunga na TANU kabla ya mwaka 1977 alipokuwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa CCM.
"Chama hiki nimeingia kwa ridhaa yangu kutokana na kukipenda. Sikuingia kutafuta maslahi wala umaarufu kwa matusi. Tangu nimeingia CCM nimekuwa kiongozi. Nina historia ndani ya chama na nazielewa taratibu za chama chetu," alisema Bw. Sumaye.

Alisema jambo lingine linalokiathiri chama hicho ni mtazamo finyu wa baadhi ya viongozi ambapo mtu akitoa jambo lolote anasingiziwa kutaka kugombea urais mwaka 2015.

"Sasa hebu jiulize kama unataka kugombea urais, akili za kawaida zinakubali eti uanze kukivuruga chama chako hicho hicho unachokitegemea ugombee! Kwa nilichosema suala la urais halipo, nimezungumza kama kiongozi wa chama, kudhani hayo ni mawazo finyu. Kama ni hivyo si ningejipendekeza basi nisikivuruge ndio maana waingereza wanasema "common sense is not common" (Busara ya kawaida ni adimu)
"Nazidi kusisitiza kuwa, lazima chama kisimame tusijekuwa tumekaa tu huku upinzani unajenga hoja lazima tuchukue hatua kwa hali hiyo," alisisitiza.

Alielezea kuwa madai kwamba anamtwisha rais gunia la misumari hayana msingi kwani ingewezekana vipi asimame kidete wakati wa kampeni kumnadi na kuhakikisha anaendelea kushika usukani, leo amtwishe gunia la misumari!

Sitta na CCM kukosolewa

Katika hatua nyingine, mwandishi wetu Wilhelm Mulinda anaripoti kutoka Mwanza kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta amesema kuwa hakuna haja ya kuwashangaa wapinzani wanaokikosoa CCM kwa vile ni wajibu wao kufanya hivyo.

Bw. Sitta ambaye pia alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipindi kilichopita, aliyasema hayo jana jijini Mwanza wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mahojiano.
"Wala tusiwashangae wapinzani kuikosoa CCM kwani hawawezi kuifisia. Na wao wanataka siku moja wapate nafasi ya kuongoza nchi hivyo katika mazingira hayo hawana sababu
ya kuisifia CCM ambayo iko madarakani," alisema.

Bw. Sitta alisema kuwa wakati sasa umefika kwa CCM kujipanga kikamilifu na kuachana na ukiritimba wa mfumo wa chama kimoja cha siasa uliokuwepo zamani ili kukabili mikikimikiki ya ushindani wa kisiasa nchini katika wakati huu wa mfumo wa vyama vingi.

"Jamani ukiritimba wa mfumo wa chama kimoja cha siasa umekwisha hivyo ushindani wa kisiasa unaotakiwa kwa sasa ni lazima ni lazima kuukabili kwa kushindana kwa hoja
ili kueleweka kwa wananchi na si vinginevyo," alisema,

Aidha Bw. Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo mkoani Tabora alisema kuwa haina maana kujitapa wakati wa ukame kwa vile tatizo hilo ni janga linalotishia maisha ya watu linapoingia katika nchi yoyote ile duniani.
Alifafanua kuwa ukame ni tatizo kubwa ambalo linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi pale dalili zake zinapoanza kujitokeza kwa ajili ya kuwanusuru wananchi wasiathirike kutokana na hali hiyo badala ya kujitapa. Hata hivyo, Bw. Sitta hakuelezea alichomaanisha katika kauli yake hiyo.

Bw. Sitta alikuwa jijini Mwanza kwenye mkutano wa mawaziri na makatibu wa kudumu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo wanachama wake ni nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

No comments:

Post a Comment