Monday, 7 March 2011

Uhaba wa Petroli waikumba Zanzibar

Petrol Pump
Uhaba wa mafuta ya petroli, umeikumba Zanzibar na kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya usafirishaji na uchukuzi baada ya kukosekana mwafaka wa kupandisha bei kati ya makapuni ya mafuta na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ).
Uchunguzi wa NIPASHE Zanzibar umebaini uhaba huo umesababisha mafuta ya petrol kuuzwa kwa bei ya ulanguzi lita moja shilingi 3,500 badala ya 1,735 kuanzia juzi.
Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa Kampuni ya mafuta ya United Petrol, Collins Chemngorem, alisema mafuta katika soko la dunia yamepanda bei kwa kiwango kikubwa, lakini kampuni zinazoingiza katika soko la ndani la Zanzibar zinaendelea kutumia viwango vya bei vya zamani na kupata hasara.
Alisema hali hiyo imesababisha wapate hasara ya shilingi mia moja katika kila lita moja kutokana na viwango vya bei vinavyotumika hivi sasa kupitwa na wakati.
Hata hivyo, alisema tayari wamependekeza serikalini viwango vya bei viangaliwe upya lakini hadi jana mchana serikali ilikuwa bado haijatoa uamuzi wake.
Alisema kampuni yake ina mafuta lakini viwango vya bei vinavyotumika hivi sasa havina faida kwa sababu wamekuwa wakipata hasara wastani wa shilingi milion 15 kwa siku.
“Tunaendelea kusubiri uamuzi wa serikali kuhusu viwango vya bei kupanda kwa sababu bei zinazotumika hivi sasa hazina faida kwa kampuni,” alisema.
Naibu Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Seif Shabani Seif, alisema ni kweli kampuni za mafuta Zanzibar zinataka kupandisha bei na mapendekezo yao tayari yamepokelewa serikalini.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria viwango vya bei ya mafuta hupangwa na Waziri kwa kushauriana na watendaji wakuu wa Wizara hiyo.
Juhudi za kuwapata wasemaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar hazikuweza kufanikiwa baada ya simu ya kiganjani ya Katibu Mkuu Wizara hiyo kuita mara kadhaa bila kupokelewa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini mafuta ya petrol yamekuwa yakiuzwa kwa bei ya ulanguzi ya shilingi 3,500 kwa lita nje ya vituo vya mafuta katika maeneo ya Kijangwani, Uwanja wa Ndege, Malindi na Mikunguni katika Manispaa ya mji wa Zanzibar.
Baadhi ya wananchi wameishauri serikali kuwaruhusu wafanyabiashra kupandisha bei ya mafuta ili kuondoa usumbufu kwa wananchi ambao wamekuwa wakisaka huduma hiyo na wengine kuanza kutembea kwa miguu licha ya kumiliki magari.
Mafuta ambayo yamekuwa yakipatikana katika vituo ni mafuta ya dizeli ambayo huuzwa kwa shilingi 1,740 kwa lita moja.
Makampuni yanayoingiza nishati ya mafuta Zanzibar ni Zanzibar Petroliam,(ZP) United Petroliam(UP) na Kampuni ya Gapco ambapo vituo vyote vya makampuni hayo vimekuwa vikikabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta hadi jana mchana.
Uchunguzi wa NIPASHE umegundua kuwa baadhi ya makampuni ya mafuta yana mafuta lakini wameamua kutoyauza hadi hapo serikali itakapokubali mabadiliko ya bei mpya ya mafuta.

No comments:

Post a Comment