Tiba ya Loliondo yamtisha Kakobe |
WAKATI idadi kubwa ya wagonjwa wakionekana kumzidi nguvu mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwasapile, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe ameingia hofu ya kupoteza waamini kufuatia taarifa kwamba mchungaji huyo anatibu Ukimwi. Jana akihubiri katika kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Askofu Kakobe alisema uwepo wa mchungaji Mwasapile unatishia vituo vya maombezi vinavyofurika mijini kubaki vitupu kutokana na watu kukimbilia Loliondo. Habari kutoka Loliondo zinasema wakati watu wakiendelea kufurika nyumbani kwa mchungaji huyo ili kupata matibabu, mamia ya watu wengine wamekwama jijini Arusha na katika eneo la Mto wa Mbu kutokana na kukosa usafiri wa kuweza kuwafikisha nyumbani kwa mchungaji Mwasapile. Mwasapile(76) ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) na Inadaiwa kuwa anatibu magonjwa sugu ukiwemo Ukimwi. Mwananchi lilishuhudia mamia ya watu katika maeneo kadhaa ya jiji la Arusha na mji wa Mto wa Mbu kwenye barabara inayoelekea Samunge kupitia Engaruka na Ngaresero umbali wa takriban kilometa 400 toka Arusha mjini. Taarifa zinasema kuzidi kuongezeka kwa idadi hiyo kumechangiwa na baadhi ya ndugu za wagonjwa wa HIV, Saratani, Kisukari na pumu waliokuwa wamelazwa katika hospitali mbali mbali nchini, kuwaondoa wagonjwa hao na kuwapeleka kwa mchungaji huyo. Hali za baadhi ya wagonjwa zimeelezwa kuwa ni mbaya na wengine bado wamekwama njiani ambapo hadi jana vilikuwa vimeripotiwa vifo vya watu wawiliambao walifikishwa Loliondo kwa lengo la kupatiwa tiba. Mwandishi wa Mwananchi alishuhudia idadi kubwa ya magari yakifika kwa mchungaji huyo, huku wagonjwa wakiwa kwenye magodoro na wengine wakiwa hawajitambui kutokana na maradhi. Hali hiyo pia inachangiwa na masharti ya dawa hiyo, ambapo mchungaji Mwasapile anasema, hairuhusiwi kusafirishwa na ni yeye pekee kwa mkono wake akikupa ndipo utapona. Uhaba wa Magari Mbali na uhaba wa magari, pia gharama za magari ya kukodi na mabasi zimepanda. Magari ya kukodi kwenda na kurudi kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro, alipo mchungaji huyo imefikia kati ya Sh100,000 na Sh150,000 kwa mtu mmoja huku nauli za mabasi zikiwa ni kati ya Sh50,000 na Sh80,000. Bei ya magari ya kukodi siku tatu ziliyopita ilikuwa ni kati ya Sh50,000 hadi 80,000 ambapo mabasi ya kawaida nauli ilikuwa ni kati ya Sh14,000 hadi 20,000. Watu kuongezeka Mchungaji Mwasapile alisema juzi kuwa idadi ya watu watakaofika kupata tiba inatarjiwa kuongezeka na kwamba ameoteshwa kuwa watu watatoka mabara mbalimbali na kwamba itamchukuwa mwezi mmoja mtu mmoja kupata tiba. Dalili za hali hiyo, zimeanza kujidhihirisha kwani tofauti na awali ambapo kwenda kupata dawa na kurudi ilikuwa ni safari ya siku moja, hivi sasa maelfu ya watu kutoka mikoa mbali mbali nchini, wapo kwa mchungaji huyo kwa zaidi ya siku tano na hawajafanikiwa kupata tiba. Mchungaji Mwasapile anadai kuwa alioteshwa na Mungu kuhusu dawa hiyo inayotokana na mti aina ya Mugariga ambao ni chakula maarufu cha Twiga, tangu mwaka 1991 lakini alisubiri hadi mwaka jana alipoanza rasmi kutoa tiba. Alitahadharisha watu wenye virusi HIV ambao watakaokunywa dawa hiyo na kupona kujikinga na maambukizi mapya, kwa kuwa mgonjwa haruhusiwi kunywa dawa hiyo mara mbili. "Wanaopona HIV waache kujiingiza katika matendo ya kupata maambuki kwani hawatapona tena...; Hii dawa sio kinga ni tiba na hairuhusiwi kunywa zaidi ya kikombe kimoja,"alisema Mchungaji Mwasapile. Msaidizi wa mchungaji huyo, Marko Nedula alisema kuwa watu wengi wanaofika kupata huduma kwa mchungaji huyo wanatoka nje ya wilaya ya Ngorongoro hasa kutokana na wenyeji kudharau awali. "Hawa wanaoleta vurugu leo hapa, mchungaji aliwambia siku nyingi njooni mpate tiba lakini walidharau,"alisema Nedula. FFU waongezwa Kutokana na maelfu ya watu kufika katika kijiji hicho kupata tiba jeshi la polisi mkoani Arusha, limelazimika kuongeza askari wa kutuliza ghasia(FFU) katika eneo la mchungaji huyo. Askari hao, wamekuwa wakisimamia na kupanga watu ili kupata tiba na kuimarisha ulinzi katika kijiji hicho, ambacho hakina huduma za kulala, vyoo, hoteli wala umeme. Akizungumzia hali ya sasa Loliondo, Mkurugenzi wa kampuni ya kukodi magari ya Sanufa , Said Kakiva aliomba serikali kuingia kati suala hilo kwa kupeleka mahema eneo la tiba na kukarabati barabara. "Mimi magari yangu yote yamekodishwa kupeleka wagonjwa, kwa huyo babu, lakini, barabara ni mbaya sana na kule hakuna huduma zozote muhimu kama mahala pa kulala na chakula,"alisema Kakiva. Alisema suala la matibabu ya magonjwa sugu Lilondo serikali inaweza kulifanya ni sehemu ya kutangaza utalii kwani, watu wa mataifa mengi wanafika kupata tiba ambayo inatokana na miti ya asili ya Tanzania. "Serikali itengeneze sasa barabara, kwani barabara hii ndiyo iliahidiwa lami na rais na inakwenda hadi mkoani Mara,"alisema Kakiva. Hofu ya Askofu Kakobe Askofu Kakobe alisema Watanzania wengi wanapenda uwongo kuliko ukweli na kutahadharisha kuwa kutokana na kuwepo mtu huyo watu hawatasubiri tena maombezi bali watapukutika kwenda Loliondo.“Hofu yangu iko katika vituo vya maombezi vilivyofurika mjini, wakati huu vitabaki tupu, watu wataenda Loliondo na hawatasubiri tena maombezi,”alisema Kakobe na kuongeza : “Tukisema tusubiri serikali ama TFDA ituthibitishie itakuwa ngumu maana kila mmoja anatia bidii kama polisi na wengine”.Alisema kanisa lake litaendelea kuwepo na kamwe haliwezi kutikiswa na Loliondo na kujigamba kuwa wanaweza kumsambaratisha mchungaji huyo. Kakobe alieleza kuwa kwake yuko muhubiri wa Injili iliyo hai na ambayo iko ndani ya Biblia huku akikumbusha mtu aliyemwita 'Babu wa Tegeta' ambaye alijitokeza miaka ya nyuma na kudai kuwa anatibu Ukimwi ambaye alisema walimsambaratisha.Kakobe ambaye alitumia muda mwingi kunukuu vifungu mbalimbali vya Biblia, alisema mfumo wa uponyaji wa Mungu umeshafunuliwa na kwamba kwa sasa hawahitaji Mungu yeyote atoe ndoto. “Hizi ni nyakati za mwisho, unatakiwa kuchagua kanisa ambalo utaongozwa katika haki na si kupeperushwa kama karatasi,”alisema Kakobe huku akishangiliwa na waumini wake.Aliwatahadharisha waumini wake akiwataka kuwa makini na mchungaji huyo huku akimtuhumu kwa kudai kuwa anatumia nguvu za giza. “Kama umesikia mtu fulani anafanya maombezi la kwanza la kujiuliza je ameokoka kwa sababu Mungu hatendi kazi na watu ambao hawajaokoka, lazima awe anahubiri Injili,”alisema.Askofu huyo alitumia ibada hiyo kuwahamasisha waumini wake kumpinga mchungaji huyo kwa maombi huku akitamka: "Kanyaga Babu wa Loliondo, sambaratisha babu wa Loliondo, kazi za babu saga."Kakobe alikwenda mbali zaidi na kumfananisha mchungaji huyo na mganga wa kienyeji huku akijigamba kuwa hata kanisani kwake watu waliokuwa na Ukimwi walipona.“Tusibabaishwe na Ukimwi, hapa tumeombea watu wamepona Ukimwi na vithibitisho vya vyeti vipo,”alisema Kakobe na kushangiliwa na waumini wake ambao baadhi yao walisikika wakisema, "tupo." Kakobe alisema hata kama mtu huyo angekuwa anatibu kwa Sh1 kwenye Neno la Mungu haikubaliki na kueleza kuwa maandiko yanasema, 'mmepewa bure toeni bure.'Katika hatua nyingine, askofu Kakobe alisema matatizo ya umeme nchini hayataisha hadi waziri wa Nishati na Madini aende akatubu kanisani kwake.Alisema mambo yanayojitokeza sasa ni matokeo ya yale waliyoyafanya Tanesco kanisani kwake na kutaka Ngeleja akatubu ili matatizo yaishe. |
No comments:
Post a Comment