Kada CCM: Serikali ndiyo inayochochea machafuko
Asema imeshindwa kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali
Asema Chadema kinapaswa kupongezwa kwa kusema ukweli
Amkosoa Tendwa kwa kauli zinazoonyesha anatumiwa na CCM
Operesheni Sangara kuingia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
Asema Chadema kinapaswa kupongezwa kwa kusema ukweli
Amkosoa Tendwa kwa kauli zinazoonyesha anatumiwa na CCM
Operesheni Sangara kuingia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameibuka na kusema kuwa serikali ndio inayochochea machafuko na kuhatarisha amani iliyopo nchini kutokana na kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa, matumizi mabaya ya rasilimali za umma, vitendo vya rushwa na ufisadi.
Kauli ya kada huyo wa CCM, Balozi Paul Ndobho, imekuja siku chache baada ya serikali na CCM kulaani maandamano Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kauli za viongozi wake kuwa zinalenga kuleta machafuko na kuhatarisha amani nchini.
Akizungumza na NIPASHE jana, Balozi Ndobho, alisema kinachofanywa na Chadema kinapaswa kupongezwa na ni jukumu la chama cha siasa kuzungumzia mambo ambayo yanashindwa kushughulikiwa na serikali iliyopo madarakani.
" Mimi ni mwana CCM kabisa ila maoni yangu ni kwamba serikali na chama ndivyo vinavyohatarisha amani ya nchi na kuleta machafuko kwa kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei, ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi pamoja na kushindwa kutatua kero ya umeme inayolikabili taifa," alisema Balozi Ndobho ambaye amewahi kuwa balozi wa Tanzania katika nchi kadhaa na Mbunge wa Musoma Vijijini 1995-2000 kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi kabla ya kurejea CCM.
Alisema kauli za viongozi wa serikali na CCM kukishutumu Chadema ni wasiwasi wanaoupata baada ya kuona chama hicho kinaungwa mkono na idadi kubwa ya Watanzania hasa kinapozungumzia matatizo yanayolikabili taifa kwa sasa.
" Kwanza sisi CCM tuna wasi wasi na ushindi tulioupata kutokana na madai kuwa kulikuwan na uchakachuaji. Hii ndiyo inayotutia hofu kwamba je, umati mkubwa wa wananchi katika mikutano ya Chadema unaweza kutuletea shida, sasa tunabuni hata vitu ambavyo havipo," alisema na kuongeza kuwa:
" Mimi nadhani serikali na viongozi wa chama tungesikiliza hoja za wenzetu na kuzipatia ufumbuzi, lakini kuzuia maandamano yao ndivyo unazidi kuzidisha hasira kwa wananchi.”
" Unasema sukari ishuke je, kilichopanda hapa nchini ni sukari tu… kila kitu kimepanda, hali ya maisha ndio inayofanya watu kuichukia serikali na cha kufanya hapa ni vyema ukadhibiti hali hiyo, ufisadi na mambo mengine kama vile malipo ya Dowans na si kukimbia kulalamika tu, " alisema.
Aliwashauri baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao walijitokeza hadharani kupinga Chadema kutafakari kuwa kinachofanywa na chama hicho kina maslahi ya taifa hivyo kuacha kulinda maslahi yao badala ya wananchi waliowafikisha hapo.
Akizungumzia kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kuwa anaweza kuifuta Chadema, alimuonya kuacha kuzitoakwa kuwa zinaonyesha kuwa anaegemea upande wa chama tawala.
" Huyo Msajili anaweza kukifuta Chadema kwa kipi? ” alihoji na kumuonya kuwa kwa kuchukua hatua hiyo anaweza kusababisha nchi isitawalike.
Balozi Ndobho alimtaka Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, kufanya maamuzi magumu ndani ya chama hicho kwa kuwaondoa viongozi wote ambao ni mzigo kwake kuanzia kwa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba.
" Hivi Makamba anafanya kazi gani ndani ya chama, hata baadhi ya wajumbe wa NEC hawastahili hata kidogo kuendelea kuwa ndani ya chama. Huku kulindana kubaya na kama hawataki kubadilika wasubiri matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Watanzania wa leo si wa jana," alisema.
Aliongeza kuwa CCM imekuwa ikijidanganya kuwa bado inapendwa bila kutambua kuwa vijana wa umri wa miaka 18 hadi 45 sasa hawako tayari kuendelea kuwa na kadi za chama hicho na kuwataka viongozi wakuu wa chama kujipanga kuhakikisha wanarejesha imani kwa wananchi.
Kuanzia Februari 24, mwaka huu hadi Alhamisi iliyopita, Chadema kilifanya ziara ya Operesheni Sangara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Mwanza, Mara, Shimyanga na Kagera ambapo wananchi wengi walijitokeza katika maandamano ya amani na mikutano ya hadhara katika miji ya makao makuu ya mikoa na wilaya.
Madhumuni ya maandamano na mikutano yalikuwa ni kuishinikiza serikali isiilipe Kampuni ya kufua umeme ya Dowans fidia ya Sh. Bilioni 94 kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) baada ya kulishitaki Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kukatisha mkataba wa kuzalisha na kuliuzia umeme.
Chadema pia kilikuwa kinaishinikiza serikali kushusha bei ya umeme pamoja na kulalamikia kupanda kwa gharama za maisha.
Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake kwa Taifa mwishoni mwa mwezi uliopita, aliyalaani maandamano ya Chadema kuwa yana mwelekeo wa kuvunja amani na yanawachochea wananchi kuichukia serikali yao.
Baada ya hotuba hiyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwemo Augustino Mrema wa TLP) na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, walidai kuwa maandamano ya Chadema yana lengo la kutaka nchi isitawalike.
NYANDA ZA JUU KUSINI MWEZI UJAO
Wakati huo huo, Chadema kimepanga kuanza kuanza ziara ya Operesheni Sangara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hivi mwezi ujao.
Wabunge wote na viongozi wa juu wa chama hicho wataweka kambi mkoani Mbeya hivi karibuni kwa ajili ya kuendelea kuhamasisha umma kujiunga na chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, alitoa taarifa hiyo juzi wakati wa mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika wilayani Mbozi.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye maandamano hayo yatakayofanyika baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Aprili.
Imeandikwa na George Marato (Musoma) na Emmanuel Lengwa (Mbeya).
No comments:
Post a Comment