Na Salma Said Zanzibar
Akina mama nao wamo katika kusikiliza mjadala wa katiba ya Tanzania ambayo kwa sasa imekuwa ikijadiliwa wakati wanasheria wakitoa mafunzo kwa kufafanua vifungu vya sheria na ibara za katiba hiyo ili kabla ya kuja
Wakitoa majumuisho baada ya kujadiliana kwa kina suala la mchakato wa kuanzishwa kwa katiba mpya katika ukumbi wa Taqwa uliopo Michenzani Mjini Zanzibar walisema wanaunga mkono kuelimishwa kwa wazanzibari juu ya umuhimu wa kuundwa kwa katiba hiyo ili kila mmoja aweze kujua faida zake na hasara zilizomo ndani ya katiba hiyo.
Aidha umoja huo wa jumuiya hizo inakusudia kuandaa kongamano jengine kubwa zadi juu ya kuandika katiba mpya pamoja na kuwashirikisha waumini juu ya kuandikwa katiba hiyo ili waweze kutoa maoni yao.
Waumini hao wamesema lazima vyombo vya serikali na taasisi za dini viwe mstari wa mbele katika kutoa elimu juu ya kuandikwa kwa katiba mpya na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili wakati utakapofika wa kutoa maoni wawe tayari wameshapata ufahamu juu ya katiba yao.
Wamesema michango itakayotolewa wakati wa kukusanywa maoni juu ya katiba mpya basi wajumbe wa tume hiyo itakayoundwa lazima waheshimu michango yote ikiwemo ya wazanzibari ili iwe na uwiyano juu ya Tanganyika na Zanzibar.
Akichangia mada katika kongamano hilo la katiba Professa Abdul- Shariff ameitaka jamii kuangalia kwa makini ni vipi itaweza kubadilisha muundo wa katiba ya Serikali ya Muungano ili iendane na matakwa ya wazanzibari.
Amesema inahitajika katiba mpya ya Muungano kwa vile katiba iliyopo haina uhalali kwa kuwa wananchi hawakushirikishwa wakati wa kuundwa kwake.
Professa Shariff alisema kuna utata katika katiba huku hasara ziiwa nyingi kuliko faida na wananchi wamekuwa wakidai haki yao lakini hakuna mipaka inayoeleweka kuna ongezeko la madai kuliko faida yake na Zanzibar ina haki ya kudai jambo hilo la katiba.
Kwa upande wake Sheikh Farid Hadi Ahmed amesema ni jambo la faraja waislamu kushirikishwa maamuzi yanayohusu nchi yao kwa kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakidai suala hilo lakini sasa angalau serikali imeona umuhimu wa viongozi wa dini kushirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya uundwaji wa katiba.
Sheikh Farid aliwataka viongozi hao kuitumia vizuri fursa hiyo walioipata na kuwaelimisha waumini wao katika suala zima la utoaji wa maoni juu ya katiba.
Amewaomba wanasheria kuendelea kusaidia kuichambua katiba vyema ili wananchi wengi wapate ufahamu katika baadhi ya vipengele ambavyo vina matatizo na sheria yeyote ambayo itakwenda kinyume na maadili ya Zanzibar basi irekebishwe.
Akitoa nasaha zake kwa viongozi hao wa dini Sheikh Farid amewataka waumini wa kiislamu kuacha tofauti zao na kuwa kitu kimoja kwa kutoa elimu ya marekebisho ya katiba kwa maslahi ya nchi na kuwapa moyo kwamba matarajio yao yatafikiwa kwa kuwa hakuna kisichowezekana katika kudai haki.
Bi Sada Mohammed akitoa maoni yake alisema lazima jamii itambue juu ya katiba iliyopo na halafu itolewe kasoro hapo jamii inaweza ikaelewa kwa vile watu wengi hawajui katiba.
Naye Hamad Othman alisema migogoro ya Muungano kila siku inaongezeka hadi sasa imeshafikia kwenye vyuo vikuu ambapo awali kulikuwa na utaratibu maalumu wa wanafunzi wa Zanzibar kupewa nafasi 200 lakini sasa nafasi hizo zimeondoshwa na wanakumbana na hubaguliwa usiokuwa na maana.
Alisema kuna masuala ya Zanzibar ambayo si ya Muungano na yanasimamiwa na kubebwa na Muungano jambo ambalo linapaswa kutafutiwa ufumbuzi katika katiba mpya ijayo.
Kero za Muungano zimekuwa zikiengezeka siku hadi siku pamoja na kuweko vikao vya kutatua lakini imeshindikana na ndio maana uchumi umedidimia kutokana na masuala yenyewe kuwa hayaridhishi.
Alisema si vyema kukawa na kasoro katika masuala ya Muungano na kwa wale wanaolaumu ikawa hoja zao hazifanyiwi kazi ambapo alisema muungano utalindwa kwa misingi ya katiba inayokubalika na sio katiba ambayo inakandamiza sehemu moja ya nchi.
Alisema muungano huu una faida lakini ni chache kuliko hasara zake ukiangalia sheria zote zinazoundwa sheria ya haki za binadamu nchi ya Zanzibar ilikuwa haitambuwi sheria hiyo kutokana na kuwa na aina fulani ya ujanjaujanja.
Akichangia katika mjadala huo, Juma Said Sanani alisema hapo nyuma Afrika mashariki ilipovunjika Zanzibar haikuwemo kwenye mgawanyo wa fedha lakini kilichopatikana kilifunguliwa Benki ya Tanzania (BoT).
“tuondoshe woga ili tusema yale yanayotuzonga katika katiba yetu tukikaa kimya wenzetu wanatapa mwanya wa kupitisha wanayoyataka wao halafu tuje kualamika” alisema Sanani.
No comments:
Post a Comment