Monday, 21 March 2011

CCM yatapatapa
•  Masha asema chama kimemeguka
 

na Sitta Tumma na Danson Kaijage
KATIKA hali ya kuonyesha Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatapatapa baada ya kuanguka katika majimbo kadhaa nchini, viongozi wa chama hicho wameanza kutoa matusi dhidi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Matusi yaliyotolewa juzi na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Maburuki Igogo jijini Mwanza yaliwalenga Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Akihutubia mkutano huo wa kuwashukuru wananchi wa wilaya ya Ilemela na Nyamagana, Lusinde alimwaga matusi ambayo hayawezi kuandikika na kuwashushia tuhuma mbalimbali viongozi hao wa CHADEMA.
Hata hivyo, kauli hizo zilionekana kuwakera baadhi ya wananchi huku baadhi ya wana CCM wakionekana kushangilia.
Naye waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi na aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha, aliwashukia wana CCM wenzake na kuwataka kuacha majungu na kwamba chama hicho kimemeguka makundi, kuna CCM A na B.
Aidha, aliwarushia madongo watu waliomsakama na kumpikia majungu wakati wa uchaguzi na kusema “Walidhani watanikomoa…sasa nani wamemkomoa?” alihoji Masha.
Wakati huohuo, umoja wa vijana wa CCM umesema utahakikisha unafanya kila njia ya kuwadhibiti baadhi ya wanasiasa wa CCM wanaotoa kauli za kupingana na viongozi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa umoja huo taifa, Beno Malisa, alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa baraza la vijana lililofanyika mjini Dodoma.
Alisema kuwa wapo baadhi ya wana CCM wamekuwa wakitoa matamko ya kupingana na viongozi wa chama kwa lengo la kujitafutia umaarufu na kuongeza kuwa kikao hicho kimeweka mikakati ya kuhakikisha viongozi ndani ya CCM ambao wanatoa matamko kwa kutofuata utaratibu hawapati nafasi yoyote ndani ya chama.
Mbali na hilo katika maazimio yao vijana hao wa CCM wamesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanapambana na CHADEMA kwa kila namna ili kisiendelee na maadamano nchini.
Katika maazimio ya baraza la vijana pia wameitaka serikali kutatua mara moja matatizo yanayojitokeza katika vyuo vikuu na kusababisha kuwepo kwa migomo ya mara kwa mara bila kuwapo sababu za msingi.
Walisema serikali inatakiwa kushughulikia mara moja masuala yanayohusiana na mikopo katika vyuo vya elimu ya juu ili kuondokana na tabia ya wanavyuo kukosa pesa za mikopo na kusababisha migomo na kuwafanya wanavyuo kusoma kwa shida.
Hata hivyo, katika kikao hicho cha baraza la vijana wa CCM wameunda tume ya watu nane ambayo itashughulikia masuala ya vijana pamoja na kuboresha kufanya uchunguzi wa sehemu ambazo zinasababisha chama kuyumba.
Tume hiyo ya vijana inaundwa na Riziki Pembe ambaye ni mjumbe toka UVCCM Zanzibar, Fadhili Njagilo mwenyekiti vijana Iringa, Hussein Bashe, mjumbe bara ambaye pia ni mwenyekiti wa tume hiyo, Rogas Shemwelekwa mjumbe UVCCM Tanga, Daud Smail toka UVCCM Zanzibar, Ashura Shengondo toka UVCCM bara na Anthon Mavunde mjumbe toka UVCCM bara.

No comments:

Post a Comment