Tishio la mabomu Gongo la Mboto |
*Hofu yatanda upya Christina Gauluhanga na Stella Aron, Gongo la Mboto SIKU chache baada ya nyoyo za wakazi wa Gongo la Mboto na maeneo jirani kukumbwa na hofu, upotevu wa mali, ulemavu na vifo vilivyotokana na milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Gongo la Mboto kikosi cha 511 KJ, hali hiyo ilirejea tena na kusababisha wakazi kuanza kuzikimbia nyumba zao. Hali hiyo imetokea jana kuanzia muda wa saa 9 jioni ambapo ilipofika usiku hofu zaidi ilizidi baada ya wakazi hao kushuhudia mionzi mikali ikitokea ndani ya kambi hiyo. Mionzi hiyo iliyofanana na radi ilisababisha hofu kwa wakazi hao ambapo walianza kubeba familia zao na kukimbia eneo hilo wakihofia kuwa huenda kuna mabomu mengine yanataka kulipuka. Kutokana na hali hiyo, wakazi walianza kuzagaa barabarani wakitembea kwa miguu huku wengine wakiwa wamepanda magari binafsi na daladala ambao walisisitiza kuwa hawawezi kuendelea kukaa eneo hilo kwa muda huo kwa kuwa limeashiria hatari. Wamedai kuwa Februari 16, mwaka huu ilipotokea milipuko dalili za awali waliziona kama hizo. Dar Leo ilishuhudia wakazi hao wakiongozana na watoto wao huku wakiwa wamebeba mizigo vichwani wakidai kuhamia kwa ndugu na jamaa zao. Hata hivyo, baadhi ya wakazi hao wlailiambia gazeti h ili kuwa mapema jana waliwaona Wazungu wakiingia katika kambi hiyo na baada ya muda walianza kuona mionzi mikali ikitokea kambini hapo. Wakazi hao wamedai kuwa awali walidhani ni dalili za mvua lakini walipoona inazidi kuendelea walijaribu kudodosa kwa wanajeshi wa kambi hiyo ambao waliwapoza kwa kuwaambia hakuna kitu kibaya kinachoendelea zaidi wageni waliofika kuchunguza milipuko ya mabomu iliyotokea siku za hivi karibuni. Kwa mujibu wa taarifa za awali zilizopatikana kupitia kwa msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe, kulikuwa na taarifa za kuwapo uteguaji wa makombora ambayo hayana nguvu na yatasafrishwa kwenda sehemu nyingine. Amesema kuna kikosi cha Wamarekani kilichofika kwa ajili ya uchunguzi na kama kutatokea taarifa nyingine wananchi watafahamishwa mapema iwezekanavyo. “Hata hivyo, kazi hiyo ya utenguaji wa mabomu haiwezi kufanyanyika bila kusambazwa kwa taarifa kwenye vyombo vya habari ili wananchi wafahamu nini kinaendelea tofauti na hivi sasa ambapo kunatokea uvumi ambao unatia hofu kwa wananchi,” amesema Mgawe. |
No comments:
Post a Comment