Thursday, 3 March 2011

CHADEMA yahofiwa kuzua vita

*Yawakumbusha vita ya Kagera
Na Waandishi Wetu, jijini

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukionya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuachana na maandamano yanayoashiria uchochezi, Waziri wake ameibuka kukionya chama hicho akikikumbushia Vita ya Kagera ya mwaka 1978-1979.

Akizungumza katika kipindi maalumu kilichorushwa na televisheni ya Taifa (TBC1), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, amesema kitendo cha CHADEMA kuendeleza mikutano aliyoiita ya uchochezi ni kwenda kinyume cha Katiba ya Nchi.

Amesema mazingira hayo yakiendelea yanaweza kuashiria kuwapo kwa vita, jambo ambalo linaweza kugharimu maisha ya wananchi wengi na kumwagika kwa damu.

Ameongeza kuwa iwapo CHADEMA watashindwa kusitisha mikutano hiyo itailazimu Serikali kutumia nguvu za dola na kukitaka chama hicho kisije kujutia uamuzi huo.

“Maandamano na mikutano ni haki kwa vyama vya siasa lakini ukitumia fursa ya mikutano kwa kutaka kuiondoa serikali iliyopo madarakani ni uchochezi na ukiukwaji wa Katiba ya muungano wa Tanzania,” amesema Wassira.

Wassira amesema nguvu za maandamano hayo zinaonyesha uchochezi dhidi ya serikali na hali ya hatari.

Jana viongozi kadhaa wa CHADEMA, akiwamo Katibu Mkuu, Wilbroad Slaa, na wabunge Chiku Abwao (Iringa) na Rachel Mashishanga (Dar es Salaam), walikamatwa na Polisi Mkoa wa Shinyanga kuhusiana na kufanya maandamano bila kibali, lakini hata hivyo waliachiwa baada ya mahojiano.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Diwani Athuman, amesema jeshi lake linaendelea na upelelezi kuhusiana na vigogo hao na taarifa kamili zitatolewa.

No comments:

Post a Comment