Wednesday, 2 March 2011

Familia za wafiwa G'Mboto kulipwa Sh8,5 milioni  
Smoke drifts over the Gongola Mboto military camp on the outskirts of Dar es Salaam Thursday Feb. 17, 2011

Patricia Kimelemeta na Elma Mhanje

SERIKALI imepanga kulipa kifuta machozi cha Sh8.5 milioni kwa kila familia, iliyopoteza ndugu kutokana na milipuko ya mabomu, iliyotokea katika Kikosi cha 511KJ cha Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Februari 16 mwaka huu na habari za awali zilisema zaidi ya watu 20 walikufa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa.
Milipuko katika kikosi hicho pia imesababisha maelfu ya watu kukosa makazi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya,

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema chini ya mpango huo kila familia iliyofiwa, inapaswa kuchagua mtu atakayesimamia mirathi ya marehemu.
Alisema kwa sasa serikali iko tayari kuanza kulipa kifuta machozi kwa kiwango cha Sh8.5 milioni na kwamba kwa msingi huo, kila familia iliyoathiriwa, ipaswa kuteua msimamizi.

Mkuu huyo wa mkoa, alisema pamoja na mambo mengine, msimamizi huyo atakuwa na jukumu la kufungua jalada la mirathi mahakamani kwa ajili ya malipo ya fedha hizo.


Kwa mujibu wa Sadiki, ndugu wa watu 29 waliokufa kutokana na milipuko ya mabomu Gongo la Mboto, watalipwa kifuta machozi.

Kabla ya kulipa machozi hayo, serikali iligharimia mazishi ya marehemu wa tukio hilo.

Katika mazungumzo hayo yake, mkuu huyo wa mkoa alisema serikali haitaruhusu ujanja ujanja kuchukua nafasi katika malipo hayo.

No comments:

Post a Comment