Thursday, 3 March 2011

Polisi wamkamata Dk. Slaa, wabunge

  Wahojiwa kituo cha polisi Kahama
  Waendelea kuwasha moto Bukoba
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga jana lilimkamata na kumhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kwa tuhuma za kufanya mkutano wa hadhara bila kibali cha jeshi hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa Dk. Slaa alikamatwa jana majira ya saa 12.30 asubuhi akiwa wilayani Kahama pamoja na wabunge wengine wawili wa viti maalum wa Chama hicho.
Wengine waliokamatwa na kuhojiwa jana ni wabunge wa Viti Maalum, Rachel Mashishanga wa Mkoa wa Shinyanga na Chiku Abwao wa Mkoa wa Iringa.
Walikamatwa katika Hoteli ya Pine Ridge iliyopo mjini Kahama. Kikosi cha kumweka ndani Dk. Slaa, kiliongozwa na Ofisa Upelelezi wa mkoa (RCO), Kashindye Hussen, aliyewapeleka kituo kikuu cha polisi cha Kahama.
Kamanda Athumani alisema baada ya polisi kukamilisha mahojiano na watuhumiwa hao walidhaminiwa na kuondoka kuelekea mkoa wa Kagera ambako wanaendelea na ratiba ya maandamano na mikutano yao ya hadhara.
Alisema katika mahojiano yake na polisi, Dk. Slaa amewalalamikia Viongozi wa Chadema wilaya ya Maswa kushindwa kutoa taarifa Polisi na kumsababisha kufanya mkutano bila ya kibali katika mji mdogo wa Malampaka wilayani humo.
Alisema licha ya Dk. Slaa kukamatwa kwa kufanya mkutano bila ya kibali pia anatuhumiwa kuzusha na kutangaza kwenye mkutano wa hadhara alioufanya mjini Maswa jana majira ya saa 6.00 mchana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Brigedia Jenerali (mstaafu) Dk. Yohana Balele, amefariki dunia.
Kamanda Athumani alisema akihutubia katika mkutano huo, ghafla Dk. Slaa aliwaambia wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo kuwa amepata taarifa kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga amefariki dunia katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Alisema Dk. Slaa alikatisha hotuba na kuwaomba wananchi wasimame kwa dakika moja kwa kumuombea mkuu wa mkoa wa Shinyanga jambo ambalo lilitekelezwa na wananchi hao.
Kamanda huyo aliongeza kuwa Dk. Slaa alifanya mkutano wake ambao ulikuwa na kibali Machi Mosi mwaka huu, majira ya saa 6 mchana katika mji wa Maswa na baadaye siku hiyo hiyo alikwenda katika mji mdogo wa Malampaka na kuhutubia mkutano wa hadhara ambao haukuwa na kibali cha polisi.
“Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tuhuma zote mbili na itakapobainika kuwa watuhumiwa walihusika na tuhuma hizo watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili,” alisema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Bukombe jana kuwa Dk. Slaa alikamatwa jana saa 2:05 asubuhi kwa madai ya kufanya mkutano katika kijiji cha Malampaka kilichopo katika wilaya ya Maswa.
Chadema ilianza maandamano na mikutano ya amani Alhamisi iliyopita jijini Mwanza na kuwakusanya maelfu ya watu na kuendelea Musoma na baadaye Shinyanga.
Mbowe alisema kuwa kabla ya jana asubuhi kukamatwa kwa viongozi hao, RCO alikuwa akiwasiliana na viongozi wa Chadema akitaka kuonana na Dk. Slaa usiku, lakini viongozi wa Chadema waligoma na kumtaka kuonana na kiongozi huyo asubuhi, kitu ambacho kilifanya hoteli hiyo kuzingiza na polisi usiku kucha.
Mbowe alisema kuwa Dk. Slaa na wenzake waliieleza polisi kuwa wao wakiwa viongozi wa juu walifanya mkutano wao kwa nia njema na kwamba walisimama hapo wakijua kuwa viongozi wao wa wilaya walikuwa na mawasiliano na polisi.
Baada ya kuachiwa huru mjini Kahama, Dk. Slaa na wenzake waliendelea na safari na kukutana na viongozi wengine akiwemo Mbowe katika mji wa Kemondo saa nane mchana kabla ya kuendelea na safari na kufanya maandamano makubwa ya amani mjini Bukoba na baadae kufanya mkutano katika uwanja wa Mashujaa mjini humo.
Wakati huo huo, umati wa wakazi wa mji wa Bukoba ulijitokeza katika maandamano ya amani yaliyoongozwa na viongozi wakuu wa Chadema.
Maandamano hayo yalipambwa na mabango, pikipiki na magari na kuanzia katika eneo la mzunguko wa barabara ya kuelekea Kyaka hadi uwanja wa Mashujaa.
Akihutubia mkutano huo, Mbowe alisema tamko la Rais Jakaya Kikwete kwamba watu wasijitokeze katika maandamano ya Chadema limewahamasisha watu kujitokeza kwa wingi katika maandamano hayo.
“Tamko la Kikwete la kutahadharisha watu wasijitokeze katika maandamano yetu limewahamasisha watu kujitokeza kwa wingi zaidi,” alisema.
Naye Dk. Slaa alisema polisi walimfuata juzi usiku hotelini mjini Kahama na kumtaka kwenda kituoni kukutana na RCO, lakini alikataa na kuwaeleza kuwa hawajui sheria kwamba kama ni kwenda angekwenda jana asubuhi.
Dk. Slaa aliwataka wananchi kumuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, atakapokwenda ziarani mkoani Kagera kuhusu hasara iliyopatikana kutokana na kampuni ya Meremeta.
Alisema leo chama hicho kitatoa tamko rasmi kuhusiana na vitisho vya serikali na masuala mbalimbali.

No comments:

Post a Comment