Dowans, Tanesco wabanwa kortini
Dk. Sengondo Mvungi
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imesema kama kuna mazungumzo yanayoendelea nje ya mahakama baina ya Kampuni ya Dowans na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wawasilishe maombi ili mahakama itambue na isimamishe kesi hiyo.
Kadhalika,Tanesco kupitia Mwanasheria Mkuu, wameiomba mahakama siku 21,ili wawasilishe hoja zao kutokana na unyeti wa kesi hiyo ambayo ina maslahi kwa Taifa.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo jana kwa ajili ya kutajwa na kuangalia pingamizi zilizowasilishwa hapo.
Waliowasilisha pingamizi hizo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mwandishi wa habari wa gazeti la The Express, Timothy Kahoho.
Kesi hiyo namba nane ya mwaka huu, ilifunguliwa na Tanesco dhidi ya Dowans na inasikilizwa na Jaji Emilian Mushi.
Hata hivyo, Jaji Mushi alisema taarifa zilizopo ni kwamba kuna mazungumzo baina ya Dowans na Tanesco juu ya kuwashwa kwa mitambo hiyo, ambapo alizitaka pande hizo kuwasilisha maombi mahakamani hapo ili kesi hiyo
isimamishwe kupisha majadiliano hayo.
Tanesco iliyokuwa ikiwasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili ambao ni
Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju, Dk. Angela Mapunda wa kampuni ya uwakili ya FK Low Chamber, Profesa Florence Luoga na Jamhuri Johnson, ambapo Masaju alidai pia kesi hiyo imefika kwa ajili ya kuangalia kama pande zote zimepatiwa tuzo.
Alidai imebainika katika shauri hilo baadhi yao hawajapata tuzo ya kesi hiyo ambao ni LHCR na Kahoho, kutokana na hilo wakili wa Dowans, Kenedy Fungamtama, akifafanua sababu ya pande nyingine kutokuwa na tuzo hiyo alidai haikuwa jukumu lake kutoa tuzo hiyo kwa sababu zilitolewa na Mahakama ya Kimataifa (ICC) ambapo mahakama imetoa amri ya pande zote kupatiwa tuzo hiyo.
Fungamtama aliiomba mahakama hiyo siku 21 ili aweze kujibu pingamizi la Tanesco.
Pia mawakili wa upande wa LHCR, Hanord Sungusia, Francis Kiwanga na Dk. Sengondo Mvungi, waliiomba mahakama hiyo siku saba ili waweze kujibu hoja ambapo Kahoho naye aliomba siku 14 kama atakuwa na cha kujibu.
Jaji Mushi alisema kumekuwa na kelele za watu wakizungumzia suala la Dowans, wakati wanafahamu suala likishafika mahakamani halipaswi kuzungumzwa lakini alisema pamoja na kelele hizo, hazitasumbua mwenendo wa kesi hiyo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 30, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama pande zote zimekabidhiana nyaraka za kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment