Thursday, 3 March 2011

Uingereza yaipa Tanzania Sh.1.5trilioni

 
Ramadhan Semtawa

SERIKALI ya Uingereza itaipatia Tanzania Sh1.5trilioni kuisaidia kutekeleza Mpango Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na kupunguza umasikini.
Hatua hiyo ya Uingereza imekuja huku ikielezwa kwamba serikali imekuwa ikikabiliwa na ukata, hivyo baadhi ya mipango yake kutokwenda vizuri pamoja na kuwepo taarifa za baadhi ya nchi wahisani kuzuia misaada yake kwa serikali.

Lakini jana, Waziri wa Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza  (DFID), Andrew Mitchell alitangaza mpango huo wa kuisaidia Tanzania ambao utatekelezwa katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Mitchell alisema mpango huo ni kwa ajili ya nchi chache duniani ambazo nchi yake inaamini kuwa zimeonyesha matokeo makubwa na chanya kwa misaada yake. Tanzania itaanza kupata msaada huo kuanzia mwaka huu hadi 2015.

Kwa mujibu wa Mitchell, serikali ya pamoja nchini humo ilipoingia madarakani mwaka jana ilitambua kuwepo kwa hali ngumu ya kiuchumi, lakini bado ilikuwa ikijipanga katika utoaji wa misaada yake.

Alitaja maeneo ya msingi ya msaada huo kuwa ni kusaidia upatikanaji wa chakula, majisafi, huduma za afya, elimu, kujenga uwezo wa kuongeza ajira na kufanyakazi na sekta binafsi pamoja na kuweka mazingira ya kutoa fursa hizo zaidi.

Waziri huyo alisema anaamini kwamba katika kipindi hicho cha miaka minne ijayo, misaada ya Uingereza italeta tofauti katika maisha kwa mamilioni ya watu.

Alisema maeneo mengine ya msingi chini ya mpango huo kwa dunia ni pamoja na kutoa chanjo zaidi kwa watoto kwa magonjwa yanayozuilika,  kuokoa maisha ya wajawazito na kupunguza vifo visivyo vya lazima kwa watoto wanaozaliwa.

Waziri huyo alisema katika mapitio ya mpango huo wa dunia, wameangalia matumizi ya rasilimali mbalimbali kwa kuzithaminisha kwa mali kupitia asasi mbalimbali zinazofanyakazi na Benki ya Dunia (WB) na Umoja wa Mataifa (UN).

"Hakuna mtu anaweza kutilia shaka umuhimu wa asasi kama hizo katika kupambana na umasikini. Uingereza haitatoa fedha kwa asasi zisizotimiza malengo isipokuwa kuelekeza fedha kwa zile zinazotimiza malengo," alisema.   
Alisema ndiyo maana nchi hiyo imeanzisha programu ya uwazi katika misaada na asasi za kuangalia ili serikali iweze kuonyesha kwa walipa kodi wake namna fedha zao zilivyotumika katika misaada.

"Naamini Uingereza inaongoza kwa jinsi inavyosimamia uwazi katika misaada na tunashauri nchi nyingine kujiunga nasi katika jitihada hizi," alisema Mitchell.

Waziri huyo alisema matumizi sahihi ya misaada huboresha maisha ya mamilioni ya watu na kuongeza kwamba anajivunia namna Uingereza inavyotimiza malengo yake kwa mafanikio.

Tanzania imekuwa ikitajwa kama moja ya nchi duniani ambazo zimepiga hatua katika utekelezaji wa MDGs hasa kipengele cha elimu ya msingi, kupunguza vifo vya watoto na pia imekuwa ikijitahidi kuondoa umaskini chini ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kundoa Umasikini (Mkukuta).

No comments:

Post a Comment