Monday, 7 March 2011

Simba ajeruhi Dar es Salaam, auawa




Venance Nestory
WAKAZI wa Kimbangulile  Mbagala jijini Dar es Salaam, juzi walikumbwa na hofu ya aina yake baada ya simba dume kuingia mtaani hapo na kumjeruhi mkazi wa eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alithibitisha tukio hilo na kumtaja aliyejeruhiwa kuwa ni Hamisi Yasin (40).

Kamanda Misime alisema kuwa Yasin alijeruhiwa sehemu za shingoni na mikononi na kwamba kwa sasa majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya  Wilaya ya Temeke ambapo anatibiwa na kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo Yasin alijeruhiwa na  Simba huyo jana asubuhi baada ya kukumbana naye mtaani hapo.

Mmoja wa mashuhuda hao aliyejitambulisha kwa jina la Kassim John alisema Simba huyo alionekama majira ya saa 12:30 asubuhi na mtoto aliyekuwa akienda dukani ambapo alianza kutoa taarifa za kuonekana kwa alichokiita paka mkubwa kutokana na kutofahamu kuwa aliyemuona  hakuwa paka bali ni simba aliyekuwa akizunguka mtaani.
John alisema baada ya nusu saa kupita, ndipo wakazi wa eneo hilo walipomuona na kugundua hakuwa paka kama ilivyoripotiwa awali, bali alikuwa Simba dume, ndipo walipotoa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi Mbagala Rangi Tatu .
Muda mfupi baada ya taarifa hiyo, polisi walifika eneo la tukio na kuanza kumuwinda simba huyo ambaye aliingia katika nyumba ambayo haijakamilika iliyoko eneo hilo.
Alisema askari hao walichukua takribani nusu saa kumvizia  kabla ya kumshambulia kwa risasi na kufanikiwa kumuua simba huyo.

Baada ya kumuua Simba huyo askari waliubeba mzoga huo hadi katika kituo kidogo cha Polisi cha Maturubai kilichopo Mbagala Zakhiem  na baadaye kupelekwa  Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wakati hali hiyo ikiendelea kundi la watu kutoka katika vitongoji mbalimbali vya eneo hilo wakiwa  wameshika Mapanga na visu waliwafuata nyuma askari waliokuwa wamebeba mzoga wa Simba huyo wakitaka kupatiwa ili wagawane nyama yake.
“Tunataka Simba wetu, tugawane, tunataka Simba wetu tugawane,”waliimba watu hao huku wakiwa wameshikilia mapanga na visu.
Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kuonekana kwa simba katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam huku tahadhari ikitolewa kwa wakazi wanaoishi karibu na Hifadhi na Mbuga za wanyama kuwa makini na kutoa taarifa mapema polisi pindi wanapoona wanyama hao ili kuepusha madhara kwa wanadamu.

No comments:

Post a Comment