CUF yabariki mikutano ya CHADEMA |
*Wadai wanachofanya ndiyo siasa Christina Gauluhanga na Stella Aron, jijini WAKATI Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ikianza kulichunguza kwa undani sakata la maandamano ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambalo limezua mzozo, Chama Cha Wananchi (CUF) kimeibuka nakusema wanachofahamu ni kuwa mgogoro huo ni wa kisiasa zaidi. Akizungumza na Dar Leo kwa njia ya simu leo, Naibu Katibu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, amesema wanachoamini wao ni kuwa maandamano na mikutano ya CHADEMA ni ya kisiasa. Amesema ikiwa Serikali inaona chama hicho kinavunja sheria ni bora kikawachukulia hatua za kisheria badala ya kulumbana. “Wanachofanya CHADEMA ni siasa. Kama Serikali imefanya uchunguzi na kubaini kuwa kuna uchochezi katika maandamano hayo sheria ichukue mkondo wake, na siyo malumbano tunayoyaona sasa,” amesema Mtatiro. Ameongeza kuwa CHADEMA huenda imeamua kufanya hivyo kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya mambo ambayo chama tawala kinaendelea kuyafanya, hususan kupanda kwa gharama za maisha. Wakati CUF wakiyasema hayo tayari Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa, amesema yupo sahihi na kauli yake kwa kuwa anaifahamu vizuri sheria na endapo atakuwa amekiuka taratibu basi sheria za nchi zitachukua mkondo wake kwa kufunguliwa mashtaka na ofisi ya DPP. ********************************** Machi 2, mwaka huu, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, barua ya onyo chama hicho. Barua hiyo yenye kumbukumbu namba CD.112/123/02/12 ilipelekwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA na nakala zake kupelekwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mahusiano na Uratibu na kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Msajili huyo alisema CHADEMA wakiwa katika mikutano ya hadhara katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mara, viongozi wa chama hicho wamesikika wakitoa lugha za vitisho, kashfa na matusi kinyume cha sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, kama ilivyorekebishwa mwaka 2009 pamoja na kanuni za maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007. “Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inakemea na kutoa onyo kwa viongozi wa CHADEMA kuacha tabia na vitendo vya uchochezi, vitisho, matusi na kashfa mara moja vinginevyo hatua za kisheria zitafuatwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Tendwa katika barua yake kwenda kwa CHADEMA. Tendwa alisema vitendo hivyo vinahatarisha amani na usalama wa nchi na kamwe hawezi kuacha viendelee bila kuchukua hatua. Barua hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekuja siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutoa tamko kwa kile kinachodaiwa CHADEMA kutoa kauli za upotoshaji na uchochezi zinazotolewa na na viongozi wake wa juu. Akisoma tamko hilo juzi, Katibu wa Halmashauri Kuu wa Itikadi na Uenezi, Kapteni John Chiligati, alisema CCM imeamua kuvunja ukimya baada ya kubaini kuwa viongozi wa CHADEMA na wabunge wao wamekuwa wakifanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa kutumia lugha za kichochezi. Chiligati alisema kitendo cha CHADEMA kumpa rais siku tisa ili atekeleze matakwa ya wananchi si kitendo cha kiungwana ila kinachotakiwa kwa CHADEMA kupitia kwa Dk. Slaa ni kuwatumia wabunge wake kuwasilisha hoja bungeni kwa masilahi ya taifa. Katika hotuba yake mwishoni mwa Februari mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete, aliionya CHADEMA kwa kuandaa maandamano ambayo alisema ni ya kichochezi ili kumng’oa madarakani. |
No comments:
Post a Comment