Wednesday, 23 March 2011

Serikali itowe muongozo wa katiba

Na Salma Said
Mwakilishi wa Jimbo la Mjimkongwe Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu hoja yake binafsi anayokusudia kuiwasilisha kwenye Baraza la Wawakilishi kuliomba baraza hilo kupitisha azimio la kuitaka serikali ya mapinduzi Zanzibar kuandaa mapendekezo ya msingi yatakayozingatiwa katika mfumo wa uandaaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo ulifanyika kwenye ofisi ya CUF, Vuga Mjini Zanzibar leo

MAELEZO YA MHE. ISMAIL JUSSA, MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI WA JIMBO LA MJI MKONGWE, KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSIANA NA HOJA BINAFSI ANAYOKUSUDIA KUIWASILISHA KWENYE MKUTANO WA BARAZA LA WAWAKILISHI UNAOENDELEA
Leo hii asubuhi nimewasilisha kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi taarifa ya kusudio la kuwasilisha Hoja Binafsi kwenye mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea, chini ya Kanuni ya 49 (1) na (2) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi (Toleo la 2011).
Hoja Binafsi niliyoitolea taarifa imelenga kutumia Kanuni ya 27(1)(m); 27(3); 47(2); 48(1) na 49 (1) ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi (Toleo la 2011), kuliomba Baraza la Wawakilishi kupitisha Azimio la kuitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuchukua hatua za kuandaa mapendekezo ya mambo ya msingi ambayo Zanzibar, ikiwa mojawapo ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itataka yazingatiwe katika mfumo mzima wa utaratibu wa uandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii inatokana na hatua tuliyofikia baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa Taifa aliyoitoa Desemba 31, 2010, kutangaza kusudio la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuchukua hatua zitakazopelekea kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alieleza dhamira yake ya kuunda Tume ya Katiba itakayokusanya maoni ya wananchi kutoka makundi mbali mbali ya kijamii na kisha kusimamia kazi ya kuandaa mapendekezo ya rasimu ya Katiba hiyo Mpya.
Katika kutekeleza tamko hilo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano katika mkutano wake wa mwezi Februari 2011 kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano itapeleka Mswada wa Sheria kuhusu utaratibu utakaofuatwa katika kuandaa Katiba hiyo Mpya ya Jamhuri ya Muungano katika mkutano unaofuata wa Bunge utakaofanyika mwezi Aprili 2011.
Kutokana na hatua hizo, nimeona kuna haja ya kuliomba Baraza la Wawakilishi kuchukua hatua ya kutoa azimio litakalotoa mwongozo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka mambo ya msingi ambayo Zanzibar, ikiwa mojawapo ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapaswa iyawasilishe kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ili nayo yazingatiwe wakati huu Serikali ya Muungano ikiwa inaandaa Mswada wa Sheria utakaopelekwa katika mkutano ujao wa Bunge ambao utaweka mfumo mzima wa utaratibu wa uandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naamini kabisa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ndiyo yenye kushikilia dhamana ya uongozi wa Zanzibar na inayowakilisha maslahi, matakwa, matarajio, haki na wajibu wa wananchi wa Zanzibar ina wajibu wa kutayarisha mambo hayo ya msingi ambayo Zanzibar kama mshiriki mmojawapo wa Muungano inataka yazingatiwe na yaingizwe katika mfumo mzima wa utaratibu wa uandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao unapaswa kusimamiwa kwa pamoja na pande zote mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nimeamua kutumia haki hii inayotolewa na Kanuni za Baraza la Wawakilishi kuwawakilisha wenzangu ambao nao kama nilivyo mimi wanaamini kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya wananchi wa nchi mbili zinazounda Muungano huu yaani Zanzibar na Tanganyika na hivyo inapaswa kuwakilisha maslahi, matakwa na matarajio ya wananchi wa nchi hizi mbili.
Nafanya hivi pia nikiamini kwamba Baraza la Wawakilishi, kwa mujibu wa Katiba ndiyo Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma ndani ya Zanzibar, na hivyo lina dhamana ya kusimamia maslahi, matakwa, matarajio, haki na wajibu wa wananchi wa Zanzibar ambao kutoka kwao ndiko yanakotoka mamlaka ya kuendesha nchi na kutoka kwao ndiko kunakotoka nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba.
Hatua ninayopendekeza ichukuliwe na Baraza la Wawakilishi ya kuiagiza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa mwongozo huo ina lengo la kuepuka kurejea makosa yaliyofanyika huko nyuma wakati wa kuweka utaratibu wa kuandikwa kwa Katiba za Jamhuri ya Muungano zilizopita zikiwemo Katiba ya Mpito ya 1964, Katiba ya Muda ya 1965 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Naamini Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano itakayotokana na utaratibu huu unaokusudiwa kuanzishwa kuanzia mwezi ujao inapaswa iepuke makosa ya nyuma na badala yake iweke misingi imara ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili zinazounda Muungano huu na ambayo itakidhi hisia, maslahi, matakwa, haki na wajibu wa wananchi wa nchi zote mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.
Hoja Binafsi niliyoitolea taarifa ya kusudio la kuiwasilisha naamini itaisaidia nchi yetu kufikia malengo hayo niliyoyataja. Kuwasilishwa kwa hoja hiyo hivi sasa kutategemea maamuzi ya Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi ambaye, hata hivyo, naamini hatakuwa na pingamizi nayo kutokana na kulenga kusaidia nchi yetu na watu wake.
Napenda niweke wazi kwamba Hoja Binafsi niliyoitolea taarifa inalenga utaratibu wa kukusanya maoni na kuipata Katiba Mpya (process) na hailengi kujadili nini kinapaswa kuwemo kwenye Katiba Mpya (contents or substance). Hayo yatatolewa maoni na wananchi wenyewe wakati wake ukifika na kwa utaratibu utakaokubaliwa.
Maelezo ya kina ya maazimio niliyoyapendekeza yapitishwe na Baraza la Wawakilishi yatatolewa baada ya kupata maamuzi ya Mheshimiwa Spika kuhusiana na Hoja hii. Kwa sasa naomba taarifa hii itosheleze.
Ahsanteni sana.
ISMAIL JUSSA LADHU
MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI
JIMBO LA MJI MKONGWE (CUF)
ZANZIBAR
23 MACHI, 2011

No comments:

Post a Comment