Wednesday, 23 March 2011

Mikakati yawekwa kudhibiti njaa 

Na Mwandishi wetu Salma Said
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akipokea album ya Mfumo wa Noti mpya za pesa za Tanzania kutoka kwa Gavana Mkuu wa BoT Prof.Benno Ndulu,alipofika na ujumbe wake Ikulu Mjini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika mikakati madhubuti ya kuweza kuzalisha na kuhifadhi chakula ili kupambana na mfumko wa bei za chakula nchini na duniani kwa jumla.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ulioongozwa na Gavana wa Benki hiyo Profesa Beno Ndulu, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa katika kutilia mkazo suala hilo katika kio cha Baraza la Wawakilishi kinachoanza leo miongoni mwa Miswada itakayojadiliwa ni pamoja na Sheria ya Uhakika wa Chakula ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo hilo lililokusudiwa katika suala zima la uhifadhi wa chakula.
Alieleza kuwa baada ya Sheria hiyo kupita wataalamu watakaa kwa pamoja na kuangalia namna ya kuifanyia kazi.
Dk. Shein alieleza kuwa suala la uhifadhi wa chakula ni muhimu sana hasa kwa wakati huu uliopo na kueleza katika kufikia hatua hiyo juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha sekta ya kilimo inapewa kipaumbele hasa kilimo cha umwagiliaji maji.
Alieleza kuwa kilimo cha mpunga ni miongoni mwa kilimo ambacho kitapewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa hapa nchini kwani mitakati madhubuti imewekwa katika kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji maji kinapewa kipaumbele Unguja na Pemba.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya kuweka mikakati katika kuimarisha kilimo cha mpunga pia, serikali ina lengo la kuimarisha kilimo cha mazao mengineyo likiwemo zao la muhogo na viazi. Alieleza kuwa mipango kabambe itawekwa katika kuhakikisha zao la muhogo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa chakula.
Alieleza kuwa tayari hekta 8500 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji, ambapo hadi sasa tayari hekta 700 za eneo hilo zimeshajengwa miundombinu ya umwagiliaji maji na tayari serikali inaendelea na matayarisho ya mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji maji kwa msaada wa serikali ya Jamhuri ya Korea ambapo jumla ya hekta 2000 tayari zimeshafanyiwa tathmini yakinifu.
Aidha, Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na maelezo ya Gavana huyo wa BOT ya kuwa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), inafanya vizuri katika kujiimarisha kibiashara na kuwa imara baada ya kuachiwa na serikali kufanya kazi zake wenyewe.
Alisema kuwa hiyo ni habari njema kwa Serikali la Mapinduzi Zanzibar na maendeleo ya Benki hiyo na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuisaidia ili ipate mafanikio zaidi.
Mapema Gavana wa Benki hiyo Profesa Beno Ndullu alimueleza Dk. Shein kuwa mfumko wa bei umekuwa kwa kiasi kikubwa hivi karibuni hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa bei ya chakula na mafuta hapa nchini hali ambayo pia, imeikumba dunia
Akimuelezea kwa upande wa Zanzibar, Gavana huyo alisema kuwa kutokana na Zanzibar kutegemea kwa kiasi kikubwa kuagiza chakula nje ya nchi hali hiyo imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa mfumko wa bei na kusababisha kupanda kwa bei za chakula ikizingatiwa kuwa hata zile nchi zinazouza chakula hicho hasa mchele nazo zimekubwa na upungufu wa chakula hicho.
Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo ipo haja ya kuzalisha chakula kwa wingi hapa hapa nchini hasa mpunga sanjari na kuweka mikakati ya uhifadhi wa chakula. Aidha, Gavana huyo alieleza kuwa katika kuimarisha sekta za maendeleo na kukuza pato la taifa sekta ya utalii imeweza kukusanya kiwango kikubwa cha mapato yake hapa Zanzibar.
Kwa upande wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Gavana huyo alieleza kuwa Benki hiyo hivi sasa imekuwa ni ya kwanza katika kujiimarisha kibiashara.
Alisema kuwa Benki hiyo hivi sasa imejijengea sifa kubwa na ina vigezo vyote vya usalama, mikopo yake ni mizuri hatua ambayo imewezesha kuwa benki imara hali ambayo inatokana na serikali kuiachia ifanye kazi zake wenyewe.
Alisema kuwa hivi sasa PBZ imo katika mchakato wa kuweka tawi lake huko Dar-es-Salaam na kueleza kuwa PBZ itakuwa ni benki kubwa na maarufu hapo baadae kutokana na kufanya vyema shughuli zake. Pia, alieleza kuwa Zanzibar kuna ukuaji wa Mabenki ambapo tayari hivi sasa kuna Benki 10 na matawi 25 kwa Unguja na 3 Pemba ambako nako kuna Benki 3.
Pamoja na hayo, Gavana huyo wa BOT, alimueleza Dk. Shein kuwa elimu kubwa wamekuwa wakiitoa kwa wananchi juu ya noti mpya zilizotolewa hivi karibuni. Pia, uongozi huo ulitoa pongezi zake kwa Dk. Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment