Sunday, 6 March 2011

Pinda atoa msimamo wa Serikali

 


Phinias Bashaya, Bukoba

WAZIRI Mkuu amevitaka vyama vya upinzani  kuacha vyama vya upinzani kuacha uchochezi badala yake vusubiri uchaguzi Mkuu wa 2015, vinginevyo Serikali itakosa uvumilivu.

Pinda alitoa onyo hilo wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Uhuru mjini Bukoba jana, ikiwa ni siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halimashauri Kuu ya CCM, John Chiligati kuitaka dola nguvu kukidhibiti Chadema kwa sababu kinataka kuindoa Serikali iliyoko madarakani kinyume cha Sheria.

 Pinda alisisitiza: “Tusifanye mchezo na kitu kinachoitwa amani na utulivu. Natoa rai miaka mitano sio mingi na hakuna raisi anayekaa madarakani zaidi ya miaka kumi. 2015 anaachia ngazi watu wajipange vizuri kati ya sasa na wakati huo,” aliasa Pinda.

Alisema kambi ya upinzani isidhani kuwa inaweza kuing’oa CCM kwa njia ya maandamano, hivyo  kuishauri kambi hiyo ianze mikakati yake katika ngazi ya shina.

Hata hivyo alitoa onyo kuwa uvumilivu una mwisho na Serikali haitasita kuchukua hatua endapo viongozi wa Chadema wataendelea kufanya mikutano inayoweza kuwaahamasisha wananchi kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani.

Alisema hata kama katiba itaandikwa upya, kama wanavyotaka haitawasaidia wasipotambua tatizo linaloikabili kambi hiyo.

Hata hivyo, Pinda alisema Serikali haiwezi kujiingiza katika malumbano na Chadema kwa kuwa sasa ipo katika mikakati ya kuwatumikia wananchi ili kuwaletea maendeleo.

Pinda alisema hivyo kufuatia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa, aliyefanya mkutano mapema wiki hii kuwaagiza wananchi kwamba Waziri Mkuu akifika awake wazi kuhusu upotevu wa mabilioni ya fedha za umma kupitia kampuni za Kagoda, Meremeta na Tangold.

Pinda alisema hawezi kujibu kila jambo linalotoka kwa viongozi wa kambi ya upinzani na kuwa ana majukumu mengi ya kiwatumikia wananchi kuliko kutumia muda kujibizana na kundi hilo na kwamba
mbinu zao za kufanya maandamano nchi nzima haziwezi kuiondoa Serikali madarakani.

“Wenzetu wameona suluhisho ni kufanya maandamano, tuwatakie kila lakheri
wanapozunguka nchi nzima wasidhani kuwa hiyo ndiyo njia ya kutung’oa madarakani. Hilo halitawezekana,” alisema Pinda.

Jumatano iliyopit Dk Slaa aliwaagiza
wananchi akisema: “Waziri Mkuu akifika atoe majibu ya upotevu wa mabilioni ya fedha kupitia kampuni ya Kagoda, Meremeta na Tangold.”

Alidai kuwa pamoja na Serikali kuwafahamu wahusika waliochota fedha hizo imeendelea kukaa kimya akiuhusisha ukimya huo kama mkakati wa makusudi wa Serikali kuwalinda watuhumiwa.


Waziri Mkuu jana aliendelea na ziara yake wilayani Muleba ambapo alikagua miradi mbalimbali na kuagiza kuwa fedha zinazotolewa na Serikali, lazima zilingane na hali halisi ya maisha ya wananchi.


No comments:

Post a Comment