Sunday, 6 March 2011

Tendwa ailima barua Chadema

Image

Elias Msuya na  Sadick Mtulya
MSAJILI wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa ameiandikia barua ya onyo Chadema akitaka iepuke kuhatarisha amani katika maandamano na mikutano yake inayoifanya nchi nzima.Katika mahojiano na Mwananchi Jumapili, Tendwa alisema kuwa kama Chadema itashindwa kutekeleza onyo hilo, itabidi achukue hatua nyingine kama sehemu ya adhabu.
“Nimeshawapa Chadema onyo, wewe ni nani hata useme nimechukua hatua gani? Au kwani kila ninalofanya hadi nitangaze?  ‘We have taken action’ (tumechukua hatua). Sasa je, watatekeleza tulilowaambia? Tutaangalia,” alisema Tendwa.

Tendwa alisema ingawa Chadema wako sahihi kufanya maandamano, hakuna haki isiyokuwa na wajibu, hivyo wanawajibika kufanya siasa za kistaraabu.“Hakuna haki bila wajibu. Ukishakuwa na haki ni lazima pia utimize wajibu, bila hivyo mizani yako haitakuwa ‘balanced’ (uwiano).

Chadema wanawajibika kufanya siasa za kistarabu,” alisema Tendwa. “Rais alitoa kauli tena kwa upole kabisa,’ alisema akifafanua kosa la Chadema katika maandamano na mikutano yao hiyo, ni kutoa lugha ya matusi na kauli za vitisho. "Wewe ni Mtanzania, Ukishatoa 'ultimatum' (Sharti la mwisho) au kumpa rais siku tisa unakuwa ume- threaten (tisha) jamii.
Ukishaleta lugha za matusi na vitisho eti utaleta ya Misri na Libya; Sisi na Libya tuna utamaduni tofauti kabisa. Sasa ukitaka kuleta mambo ya Libya hapa unadhani watu watajisikiaje?" alihoji Tendwa. Tendwa akitolea mfano wa nchi ya Marekani, alisema matatizo ya kiuchumi yaliyopo, siyo kigezo cha Chadema kuandamana. "Mwaka 1930 Marekani uchumi wao ulidorora,  lakini wenzetu hawakuandamana. Walifanya jitihada tu.

Tunakubali kweli kuwa hali ya uchumi ni mbaya, hata wabunge wa Chadema wako kwenye kamati za Bunge wanajua hilo. Sasa kama tatizo la umeme tu ndiyo unakwenda nchi nzima? Wangeangalia hali ya nchi imejipangaje,” alisema Tendwa. Hata hivyo Ofisa Mwandamizi wa Chadema, Victor Kimesela akizungumza na TBC1 juzi alikiri Tendwa kuiandikia Chadema barua ya onyo na kueleza kuwa tayari chama kimeshamjibu.

Alisema pamoja na mambo mengine, Chadema imemtaka Tendwa aeleze na kutoa ushahidi  mkutano na mahala ambako viongozi hao wa Chadema walitoa lugha ya matusi na kuchochea vurugu."Huu si wakati wa porojo.
Kweli msajili wa vyama ameiandikia Chadema barua ya onyo ya kuwataka viongozi wetu waache kutoa lugha ya matusi pamoja na kuchochea vurugu," alisema Kimesera na kuongeza:"Lakini pamoja na mambo mengine, chama kimemtaka Tendwa aeleze  na kutoa ushahidi wa mahali gani viongozi wetu walitoa lugha ya matusi pamoja kutoa maneno ya kuchochea vurugu nchini,'' alisema Kimesela.

No comments:

Post a Comment