Sunday, 6 March 2011

Sumaye: CCM ijibu hoja za Chadema



Claud Mshana
WAKATI CCM ikitaka dola ikidhibiti Chadema, Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya tatu, Fredrick Sumaye, amekitaka chama hicho tawala kukabiliana na hoja za Chadema kisiasa badala ya kuiachia Serikali ipambane nao.Juzi CCM kilisema nyendo za Chadema zina agenda ya siri ya kuking’oa madarakani kwa kutumia nguvu kinyume cha katiba hivyo kiliitaka Serikali na vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria haraka.

“CCM inaviomba vyombo vya dola viwe imara kuchukua hatua za kisheria… Wanachofanya Chadema ni kutuchonganisha na wananchi, kutoa kauli hatari za kujaribu kughilibu akili za watu ili kuchochea machafuko, umwagaji wa damu na uasi. “Wanachochea wananchi wakisema, ‘peoples’  na hujibu ‘power’! (nguvu ya umma), Je mpo tayari kufanya kama Tunisia, Misri? (ambako serikali zilipinduliwa kwa nguvu ya umma)”  alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, John Chiligati kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika juzi, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili bila kujua kwamba CCM wangekuwa wanazungumzia suala hilo, Sumaye alisema CCM inatakiwa kukabiliana kisiasa na hoja za Chadema na si kuiachia Serikali ipambane nao.

Kwa mujibu wa Sumaye, kazi ya siasa ni ya chama na si serikali, hivyo CCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na Chadema kwa sera na kujibu hoja zao zote ili kuongeza imani ya wananchi kwa chama hicho.Sumaye alisema si ishara nzuri kwa CCM kukaa kimya wakati wapinzani wanaendelea kukishtaki kwa wananchi kuwa kimeshindwa kufanya kazi.

Sumaye ambaye Mwananchi Jumapili ilimtafuta kusikia maoni yake kuhusu mfululizo wa mikutano ya Chadema na mustakabali wa CCM, alisema chama hicho tawala kinapaswa kujibu hoja zote za Chadema kisiasa na kama hakina majibu kiiombe Serikali majibu hayo na iyatoe kwa wananchi.

“Wale (Chadema) wanafanya kazi za siasa na hawa (CCM) wamekaa kimya, wanaiachia Serikali ndio inatoa majibu, hali hiyo si nzuri, chama kinapaswa kujibu hoja zote na kama hakina majibu, kiombe kwa serikali,” alisema Sumaye.Mjadala wa uhalali wa mikutano na maandamano ya Chadema uliibuliwa na Rais Jakaya Kikwete alipolihutubia taifa kupitia radio na televisheni Februari 28, mwaka huu na kuwaleza wananchi kuwa chama hicho cha upinzani kina lengo la kuleta machafuko nchini.

Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa akilihutubia taifa mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.Kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye Chadema waliipuuza, ilisisitizwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Steven Wassira, aliyesema kuwa Chadema wasije kuilaumu serikali ikikosa uvumulivu na kuanza kutumia dola kukishughulikia.

Akihojiwa na gazeti hili Sumaye hakuishia kuishauri CCM kuja na hoja za kisiasa kujibu mapigo ya Chadema, bali pia alieleza aina ya watu wanaofaa kukiongoza chama hicho tawala wakati huu wa mabadiliko makubwa ya kisiasa.Sumaye alisema CCM inahitaji viongozi waadilifu, wachapakazi na wasio waoga kumshauri rais ili kuwa na mabadiliko ya kiutendaji yanayoendana na joto la kisiasa lililopo. “Tunahitaji viongozi wasioogopa kumshauri rais juu ya masuala mbalimbali, kama utakuwa na viongozi waoga, lazima kutakuwa na matatizo,” alisema Sumaye.

Kuhusu mabadiliko ndani ya CCM ambayo Rais Kikwete alisema ni lazima yafanyike, Sumaye alisema anakubaliana msimamo huo na anampongeza Rais kwa kutambua kuwa chama kinahitaji mabadiliko makubwa ya kiutendaji.“Kwanza nampongeza Mwenyekiti, maana ameona hilo. Watu wengi  wanaona kuna umuhimu chama kurekebishwa na eneo muhimu ni utendaji wa viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya chama,” alisema Sumaye.

Sumaye alieleza kuwa CCM kitaendelea kushika dola, lakini kama kinataka hayo yatimie, mabadiliko ndani ya chama ni muhimu.Alisema umuhimu wa CCM kujifanyia tathmini ya utendaji ulianza kujionyesha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ambapo ikilinganishwa na chaguzi nyingine, chama kilipata upinzani mkali."Sasa ni dhahiri kunahitajika mikakati madhubuti ili kuhakikisha mwaka 2015 unakuwa mrahisi kwa CCM," alisema Sumaye.

Ndejembio atabiri anguko
Habel Chidawali anaripoti kutoka Dodoma kuwa, Kada maarufu wa CCM, Pancras Ndejembi amekitabiria chama hicho kikongwe kuzama.Kada huyo ambaye ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Dodoma alisema jana kuwa  hali ilipofikia kwa sasa, CCM inaonekana kupoteza mwelekeo na kutia shaka mustakbali wa chama hicho siku za usoni.

Ndejembi ambaye aliwahi kutumikia nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali na chama katika utawala wa Serikali ya awamu ya kwanza, alisema CCM bado haijaingia shimoni ila inaelekea huko.“Ni kweli chama hakifuati utaratibu uliokuwepo ndio maana nasema kuwa kinaelekea kuzama tofauti kabisa na enzi zetu  ambapo Mwalimu Julius Nyerere alikuwa anasisitiza kuwa turudi kwa wanachama tukae nao na kuzungumza, jambo ambalo sasa hilo halipo na viongozi wamebaki huko juu,” alisema Ndejembi.

Alisema viongozi wa ngazi ya taifa wamebaki katika maofisi yao na kushindwa kurudi katika ngazi za chini kuimarisha chama na matokeo yake wanaishia kupiga kelele bila ya kuwa na uhakika wanachama ngazi ya chini wanataka nini.Ndejembi hivi alisema hakuna mshikamano wa dhati ndani ya chama jambo linalowafanya wanachama kumuachia mzigo wote Mwenyekiti wa Taifa.

“Watu wanaishia kulaumiana kila kona kwamba chama kimefanya nini, mara wanasema bado kimesimama wengine wanasema kuwa kinayumba, ila ukweli utabaki palepale kuwa CCM tunazama sasa,” alisisitiza.Kuhusu nguvu ya wazee ndani ya Chama Ndejembi alisema: “Sisi tumestaafu hivyo tupo tupo na kama hawataki kutuita unadhani tutakwenda ? Lakini, wakisema tuende tuko tayari kukaa pamoja nao kutengeneza utaratibu wa kukinusuru chama kisizame kabisa katika tope”.Ushauri

Kuhusu nini kifanye ili kukinusufu CCM, alisema unahitajika mshikamano wa dhati kati ya viongozi na wanachama: “viongozi wanahitaji kutambua kwa dhati kuwa chama kiko ngazi ya chini kuanzia kwa wajumbe wa nyumba kumi sio ngazi ya mikoa”.Alishauri kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa anatakiwa abaki kama kiongozi wa kutoa ushauri kwa juu, lakini awe na watu wanaochukua mawazo kutoka kwa wanachama wa ngazi ya chini.

Hata hivyo, alisema viongozi wa taifa bado wana mfumo mbovu wa mawasiliano, kwani kila mtu katika nafasi ya juu ni msemaji, jambo linalofanya wajichanganye katika taarifa zao.

No comments:

Post a Comment