Friday, 4 March 2011

Pinda aenda 'kufuta nyayo' za Dk Slaa




 
<><>  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Mwandishi Wetu

KATIKA kile kinachoonekana kama mpango wa Serikali kukabiliana na nguvu za maandamano na mikutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo anatarajiwa kuanza ziara ya siku nane katika Mkoa wa Kagera ambako atakagua shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kutembelea wilaya zote za mkoa huo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri Mkuu ataanzia ziara yake katika Manispaa ya Bukoba kisha atakwenda Muleba, Chato, Biharamulo, Ngara, Karagwe, Missenyi na kumalizia Bukoba Vijijini.

Katika ziara yake ya Kanda ya Ziwa, Chadema kilitembelea na kufanya mikutano katika Wilaya za Biharamulo, Misenyi, Muleba na Chato ambako viongozi wake walifanya mikutano na maandamano huku wakitaka Kampuni ya kufua umeme ya Dowans isilipwe, bei ya umeme ishuke na kikitaka utawala wa CCM uwajibike.

Baadhi ya shughuli kubwa ambazo Waziri Mkuu amepangiwa kufanya wakati wa ziara hiyo ni pamoja na kuzindua Barabara ya Zamzam na mkutano wa hadhara kwa wakazi wa Manispaa ya Bukoba katika Uwanja wa Mayunga (Uhuru Platform).

Akiwa wilayani Muleba, Waziri Mkuu Pinda atakagua shamba la mkulima bora wa kahawa katika Kijiji cha Ilogero kabla ya kwenda Buganguzi ambako atakagua mashamba ya migomba yaliyoshambuliwa na magonjwa ambayo mpaka sasa hayajajulikana kisayansi.

Pia ataweka jiwe la msingi katika mradi wa umwagiliaji katika Kijiji cha Buyaga na kuhutubia wananchi katika Viwanja vya Shule ya Msingi ya Kasharunga.

Akiwa wilayani Chato, Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi katika jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kufungua Saccos ya Mshikamano kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Shule ya Msingi Chato.

Akiwa Biharamulo, Waziri Mkuu atakagua mnada wa ng’ombe wa Lusahunga, kukagua ujenzi wa wodi katika hospitali hiyo na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya St Clara huko Rukaragata na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Michezo wa CCM.

Akiwa Biharamulo, Jumanne ijayo Waziri Mkuu atakwenda Ngara kufungua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Ngara Farmers kabla ya kwenda kwenye Mgodi wa Nickel wa Kabanga. Pia atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara huko Muurusagamba.

Akiwa Karagwe, Jumatano ijayo atakagua bwawa la samaki huko Kishoju na kusalimiana na wananchi kisha atakwenda Kayanga kuzindua jengo la masjala ya ardhi. Mchana ataweka jiwe la msingi katika Chuo cha Ualimu Katera kabla ya kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Isingiro.

Akiwa Missenyi, Alhamisi ijayo, Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo. Baadaye ataelekea Kiwanda cha Sukari cha Kagera kuona mitambo ya kisasa ya umwagiliaji mashamba ya miwa. Pia atakagua shughuli za kiwanda hicho na kisha kuzungumza na wananchi katika Uwanja wa Mashujaa wa Bunazi.

Akiwa Bukoba Vijijini, Ijumaa, Waziri Mkuu atatembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku, maabara na baadhi ya vijishamba vya utafiti wa kilimo. Pia atakwenda Hospitali ya Izimbya kuzindua majengo ya OPD, watoto, maabara, chumba cha upasuaji na jengo la ushauri na upimaji VVU (CTC).

Jumamosi ijayo,  Waziri Mkuu atafanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu Mkoa na kurejea jijini Dar es Salaam mchana huo.

No comments:

Post a Comment