Friday, 4 March 2011

Kanisa Katoliki lakataa msaada wa mbunge


Mussa Mwangoka, Sumbawanga
KANISA Katoliki katika Jimbo la Mpanda mkoani Katavi, limeagiza  kurudishwa kwa msaada  uliotolewa na Mbunge  wa Mpanda Vijijini (CCM), Moshi Kakoso   kwa ajili ya kusaidia   vigango vya  Parokia  ya  Karema.

Agizo hilo linatokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kanisa kukerwa na hatua ya uongozi  wa CCM wilayani Mpanda, kulikashifu.

Habari zilisema agizo hilo lilitolewa juzi na Makamu Askofu wa Jimbo  hilo, Padri  Patrick  Kasomo, ambaye pia  ni  Paroko wa Karema,  kufuatia maneno  ya  kejeli na kashfa  yanayodaiwa kuwa yalitolewa na Katibu  wa CCM  wa Wilaya  ya Mpanda.

Padri Kasomo alidai kuwa Katibu huyo wa CCM alitoa kashfa hizo alipokuwa akihutubia  mkutano wa hadhara,  ulioitishwa na mbunge huyo kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu madai hayo, Katibu huyo Jacob Nkomola, alisema hakusema maneno hayo dhidi ya kiongozi huyo wa kanisa na kwamba  kilichopo ni mgogoro baina ya wananchi na kanisa baada ya Padri Kasomo kupora sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji, yakiwemo maeneo ya wazi.

Alidai kuwa maeneo hayo ni pamoja la uwanja wa kuchezea mpira, ambao alipitisha trekta na kuubadilisha kwa ajili ya  shughuli za kilimo.
"Nilichozungumza kwenye mkutano wa hadhara ni kwamba kiongozi wa dini anayevaa msalaba na kanzu anatakiwa kuwa mkweli, sasa huyu padri anaingiza ushabiki wa kisiasa, yeye tangu wakati wa uchaguzi alikuwa akipigia kampeni Chadema na anafanya hivi huku akipora maeneo ya wazi ili kumkwamisha diwani wa CCM aliyeshinda  katika Kata ya Karema," alidai katibu huyo katika mazungumzo ya njia ya simu.
Msaada uliokataliwa ni wa Sh300,000 zilizotolewa kwa nyakati tofauti katika  vigango vya Kaparamsenga, Ikola, na Karema.

Kila kigango kilipewa  kilipata Sh 100,000 ikiwa ni msaada kutoka  kwa mwanasiasa huyo.

Padri Kasomo alidai kuwa katika mkutano huo, Katibu  wa CCM wa Wilaya ya Mpanda, alimkashifu yeye  na  imani ya kanisa.
Alisema kuwa mtendaji huyo wa CCM aliwasalimia wananchi kwa salamu inayotumiwa na Kanisa hilo Katoliki  inayosema ‘Kristu’ na kujibiwa tumaini letu lakini mtendaji huyo alisema tumaini liwe kwenu tu si kwa padri wenu Kasomo,fisadi ambaye   hastahili kuwa kiongozi  wa kiroho .

Padri huyo alidai kuwa kejeli  na  kashfa   hizo zilizotolewa mbele ya waumini wake.

Alidai katibu huyo aliwataka waumini wa kanisa kuandamana kwenda parokiani kumvua kanzu ya upadri

Mkuu  wa Wilaya ya Mpanda Dk Rajab Rutengwe alipohojiwa  kwa  njia ya  simu  alikiri  kupokea malalamiko  hayo  kutoka  kwa Makamu  wa Askofu  Kasomo.

No comments:

Post a Comment