Friday, 4 March 2011

Mchungaji adaiwa kutibu ukimwi

 
Daniel Mjema, Moshi
KWA takribani wiki moja sasa, mji wa Moshi na vitongoji vyake, umekuwa ukizizima kufuatia taarifa za kuwapo kwa mchungaji mstaafu anayetoa dawa zinazotibu magonjwa makuu manne ukiwamo ukimwi, kwa gharama za Sh500 tu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa makundi ya watu wakiwamo Watanzania wenye asili ya kiasia, yamekuwa yakisafiri kwenda Loliondo, ili kupata tiba kutoka kwa mchungaji huyo.

Habari zilizozagaa katika mji wa Moshi na vitongoji, zinadai kuwa mchungaji huyo amekuwa akitibu magonjwa ya kisukari, ukimwi, shinikizo la damu na ugonjwa wa saratani.


Juzi mchana, nusu ya abiria waliokuwa katika basi moja la abiria lililokuwa likitokea Dar es salaam kwenda Arusha, walikuwa ni wale waliokuwa wakienda Loliondo lakini wakipanga kuanzia safari zao Arusha.

Wakili mmoja wa kujitegemea ambaye alikuwa ndani ya basi hilo, akitokea Moshi kwenda Arusha, aliliambia Mwananchi kuwa nusu ya abiria hao, walikuwa wanaelekea Loliondo.

Magari yanayokwenda eneo anakopatikana mchungaji huyo ni yale yenye nguvu (4WD) na nauli ya kwenda na kurudi kutoka Moshi ni kati ya Sh70,000 na Sh80,000 ingawa wenye uwezo wamekuwa wakitozwa hadi Sh100,000.

Dereva mmoja Haji Sadiki, juzi usiku alionekana akiondoka na kundi la watu nane kuelekea Loliondo na inadaiwa kuwa kila mmoja alilipa Sh70,000 kwa ajili ya nauli ya kwenda na kurudi.

Mkazi mmoja wa Mwanga, Rodgers Msangi, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM aliitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutoa tamko kuhusu uhakika wa tiba inayotolewa na mchungaji huyo.

"Watu wanasema unapewa dawa kwenye kikombe kimoja cha chai na hata kama una ngoma (ukimwi) unapona na wala hataki pesa yako zaidi ya Sh500 tu. Watu makundi kwa makundi wanakwenda huko kila siku," alidai Msangi.

Habari zilizozagaa mkoani Kilimanjaro zinadai kuwa hata baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini,wabunge na viongozi wastaafu wamekwishakwenda na kupewa dawa hiyo, ingawa hakuna uthibitisho wa kimaabara unaothibitisha nguvu ya dawa hiyo.

Tangu kuzagaa kwa taarifa ya mchungaji huyo, watu wamekuwa wakikusanyika katika vikundi kujadili suala hilo.

No comments:

Post a Comment