Friday, 4 March 2011

Viongozi sasa ni zamu yenu kufunga mikanda

 
<> 
<> 
Na Editha Majura

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
 Benno Ndullu


TUMEZOEA kuambiwa na viongozi kwamba; “hali ya
uchumi ni mbaya, wananchi fungeni mikanda.” Sasa ni zamu ya watawala nao kufunga mikanda ili nchi ihimili mtikisiko wa uchumi unaoelezwa kusababishwa pamoja na mambo mengine, kuyumba kwa uchumi duniani.

Hata Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benno Ndullu, ameliona hilo na kusema endapo watawala watafanya hivyo huku wakitekeleza mipango na mikakati kwa dhati ya kweli na uadilifu wa kutosha, tutaepuka kuanguka kwa uchumi.

Ingawa ni kweli kwamba kutikisika kwa uchumi duniani ni kiini cha hali mbaya ya uchumi nchini, ni vyema watawala wakatambua kuwa ni wakati ambao wanatakiwa wawe na dhamira ya kweli ya kulikomboa taifa katika uchumi tegemezi.

Nchi kufikia uwezo wa kuwa na uchumi unaojitegemea siyo jambo lelemama, viongozi wanatakiwa kuzingatia umuhimu wa kuweka mazingira ya kuboresha uchumi usiyo tegemezi ambao ndiyo nguzo ya kukabiliana na mtikisiko wa aina hii.

Hata hivyo kudhani tunaweza kufikia hatua hiyo huku asilimia 70 ya bajeti ya nchi, ikiendelea kufujwa kwenye upande wa utawala badala ya kutengwa kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ni kujidanganya.

Bila uadilifu wa kweli ni vigumu kwa taifa lolote hata kama linakuwa na vyanzo vya mapato vingi kiasi gani, kufikia hatua ya kujitegemea kiuchumi.

Miongoni mwa sumu kali inayoweza kuangamiza uchumi ulio imara ni pamoja na pamoja na kushamiri kwa rushwa.

Hakuna ubishi kwamba nchini vitendo hivyo vimepamba moto kwa kiwango ambacho ni vigumu kupambanua nani muadilifu nani si muadilifu. Hali hiyo imegubika karibu katika  kila ngazi ya jamii.

Pamoja na rushwa nchi kuongozwa na watu wenye sifa ya ubinafsi na uroho wa kujilimbikizia mali ni jambo linalohatarisha zaidi uchumi na kusababisha hata misaada inayotolewa kusaidia angalau kuimarisha uchumi kuyeyuka kama barafu juani.

Rejea mwezi uliyopita wakati wa vikao vya kwanza vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mara baada ya wabunge kuapishwa ambapo kila mbunge alipewa 90 milioni eti akanunue gari la kufanyia shughuli zake za kibunge.

Ingawa Spika wa Bunge, Anna Makinda, wakati akiahirisha mkutano huo alitoa ufafanuzi kuwa fedha hizo zilitolewa ikiwa ni mkopo ambao kila mbunge atatakiwa kuurejesha, bado hiyo siyo hoja ya kutosha kuhalalisha kitendo hicho wakati taifa likikabiliwa na hali mbaya kiuchumi.

Haieleweki ni katika mazingira gani wabunge wote zaidi ya 300 walihitaji mkopo wa kiasi hicho cha fedha ili wanunue gari la kazi jimboni!

Ina maana hata wabunge waliyodumu bungeni tangu nikisoma shule ya msingi pia walihitaji mkopo wa aina hiyo? Kama hivyo ndivyo, basi nchi yetu ina tatizo kubwa, ambalo utatuzi wake utahitaji muda na gharama kubwa.

Inapoelezwa kuwa nchi ina hali mbaya kiuchumi, isidhaniwe kuwa hali iliyopo sasa ni sawa na ambayo tumezoea kuambiwa bali ubaya wa sasa umeifikisha serikali mahala pa kufyeka bajeti ya wizara zake zote ili kufikia mahitaji yanayowiana na kiasi kiduchu cha fedha zilizopo.

Endapo hatua za kuacha au kupunguza mahitaji na huduma zinazoagizwa kutoka nje hazitatekelezwa huku bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zikiendelea kupungua kutokana na nchi wateja kukumbwa na mtikisiko huo, tutegemee kushuhudia ugumu mara dufu wa uchumi.

Wahaya wana msemo; “okitega mka’sho kiija na nyoko” (unatega mtego ukikusudia anaswe mama yako wa kambo, ananaswa mama yako mzazi) ndivyo ilivyo kwa watawala wetu sasa ambao mara kwa mara wametutaka tufunge mikanda, lakini sasa hali hiyo inamekuwa ya kweli tena kwa wote.

Katika hali ya kushangaza, ambapo viongozi nao wanatakiwa kufunga mikanda watu muhimu kwa jamii na uchumi wa nchi kama wabunge wanaibuka na kioja cha kukopeshana mamilioni ya fedha ili wakanunue magari aina ya Land Cruzer yenye mikonga, kama ilivyoelezwa na Spika Makinda.

Mbaya zaidi wakati wakitekeleza hayo, ndani ya ukumbi wa bunge wanajadiliana namna ya kuwapelekea wapiga kura wao pikipiki za magurudumu matatu ili zitumike kama daladala kwa madai kwamba zina uwezo wa kupenya kwenye foleni na hata mahala ambapo magari hayawezi kufika kwa urahisi.

Ni muhimu sasa kutambua kuwa badala ya watawala kuendelea kugawana keki ya nchi ‘jikoni’ na kuila kutokea mifukoni mwao keki hiyo ni ya Watanzania wote sharti iachwe iive, iwekwe mezani kisha igawanywe kwa usawa ili kila mmoja afurahie matunda ya uhuru wa Nchi yake.

Kipindi hiki cha dunia kukabiliwa na hali mbaya kifedha, kichukuliwe kuwa ni changamoto inayopaswa kujengewa mikakati madhubuti na ya haraka ili taifa livuke salama.

Hali mbaya ya uchumi kuendelea kuimbwa huku watawala wakihaha kujitajirisha kwa namna tofauti inaweza kuleta hatari siyo tu kwa uchumi bali hata kwa amani ya nchi yetu.
Editha Majura ni mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi.
0716 263949

No comments:

Post a Comment