Wednesday, 9 March 2011

Mkurugenzi Zanzibar ataka wanawake wasaidiwe
Mwandishi Wetu
 MASHIRIKA yasiyo ya  kiserikali yametakiwa kuwasaidia wanawake wasio na uwezo  wa kujielimisha  ili waweze kufikia malengo ya kukuza vipaji na kujiajiri  hapa nchini.
Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa  ya The British School of Zanzibar iliyopo Maisara Zanzibar, Aysharose Mattembe, alisema hayo alipozungumzia mtazamo wake juu ya mafanikio ya wanawake nchini wakati wakiadhimishi siku yao.

Mattembe ambaye alizungumzia zaidi uzoefu wake kwa wanawake wa Mkoa wa Singida alisema  wana uwezo mkubwa katika masomo, kazi na hata utunzaji wa familia, lakini tatizo ni umaskini katika mapato.
Pamoja na kuwatakiwa heri wanawake nchini katika kuadhimisha siku maalumu ya wanawake duniani, alisema wanawake wanahitaji kusaidia katika masuala ya mitaji na hata elimu.

“Wanawake wengi wana bidii katika  kutafuta elimu, ujuzi na maarifa na pia  ni wabunifu , lakini tatizo kubwa ni mtaji”alifafanua.

Alisema wanawake nchini wakiwemo wa Mkoa wa Singida wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama za elimu duni, afya na elimu ya uzazi wa mpango, ajira, elimu ya Sayansi na Teknolojia na kupata haki za msingi mbele ya sheria ili waweze kufikia malengo mbalimbali yakiwemo yale ya milenia na  yale ya mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Tanzania.

Alisema wanawake pia wamekwamisha mara nyingi na suala la kutojua haki za kisheria pamoja na mila na desturi potofu, kunyanyaswa kijinsia, kunyanyaswa kifamilia, vipigo kwa wanawake kutoka kwa waume na elimu duni.

Akikifafanua zaidi alisema mwanamke ni nguzo ya familia hivyo  akielimika yeye atahakikisha na familia yake inaelimika na kwamba elimu ni silaha tosha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali  kwa dunia ya sasa ya utandawazi.

Alitoa wito kwa vijana wa kike kuonge\za kasi ya kupenda elimu na kujifunza mambo mapya kila siku ili kuweka misingi bora ya kupambana na umaskini.

Kuhusu masuala ya amani nchini, alisema  pamoja na upanuzi wa demokrasia nchini,  vyama vya siasa  vina wajibu wa kuilinda na kuienzi   amani na utulivu wa nchi na kwamba kamwe Watanzania wasiingize mambo ya Misri, Tunisia, Libya  na kwingineko  ili kuepusha madhara yatakayowapata wanawake na wenye ulemavu.

“Hivi majuzi  mabomu ya Gongo la Mboto yametushtua sana , watu tayari wameshaathirika kisaikolojia sasa kama ni vita vyenyewe bila shaka inaweza kuwa balaa kubwa”, alisema.
Alisema akiwa mwanamke kiongozi wa shule anaamini kwamba Wanawake ndio nguzo ya mabadiliko kuelekea kwenye neema.

No comments:

Post a Comment