Wednesday, 9 March 2011

China ‘yamwaga’ Sh 25bn mkongo Mawasiliano Z'bar  
Ramadhan Semtawa
BAADA ya kusaidia ujenzi wa mkongo mkubwa wa mawasiliano kwa Tanzania bara, China imetoa mkopo nafuu wa dola 20 milioni za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa mkongo kama huo kwa upande wa Zanzibar.

China kupitia Kampuni yake ya Chinese International Constructions (CICC), ndiyo ilifanya upembuzi yakinifu kwa mkongo wa mawasiliano wa taifa (Fibre Optic Backbone) kwa Tanzania bara, ambao umegharimu takriban Sh 200 bilioni.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kusaini hati ya makubaliano kati yake na Kaimu Balozi wa China nchini Jinjun Tu, mbele ya Rais Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi Ramadhani Kijjah, alisema mkongo huo unalenga kuunganisha ofisi za serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika utoaji huduma za kisasa.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mradi huo ambao utaanza wakati wowote baada ya SMZ kukamilisha taratibu husika, utaondoa hatari ya kupotea kwa nyaraka za kumbukumbu za serikali na kuwezesha uhifadhi wa kisasa.

Alifafanua kwamba, mkongo huo wa ICT pia utaongeza ufanisi zaidi katika shughuli za usalama  wa taifa na kuongeza kasi ya maendeleo kwa visiwa vya unguja na pemba.

"Katika sekta ya utalii, watalii ambao hutumia intaneti wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa wawapo visiwani, lakini mradi huu utarahisisha gharama za mawasiliano, "aliongeza Kijjah, katika hafla hiyo ambayo ujumbe wa China uliongozwa na Mshauri Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo Ji Peding.

Akifafanua zaidi, alisema mfumo huo pia utasaidia mipango mbalimbali ya kupambana na vitendo vya uhalifu ikiwemo vita dhidi ya ugaidi inayoendelea duniani.

Tanzania imekuwa ikitajwa kuwa na miundombinu ya mawasiliano ya Fibre Optic ambayo humilikiwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Tanesco, Shirika la Reli (TRC), Tazara na Songas, ambayo hata hivyo, haijatumika vya kutosha kuboresha mawasiliano ya ICT.

Katika hatua nyingine, China imetangaza mpango wa kusukuma gurudumu la elimu ya msingi kwa kutoa dola 1milioni za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa shule maeneo yenye mahitaji makubwa, hati ambayo awali ilisainiwa kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Profesa Juma Dihenga na Meng Tu Katibu Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana ya China.

No comments:

Post a Comment