Thursday, 10 March 2011

Mahita aibukia Mahakama Kuu
*Ataka kumuhudumia mtoto wake kwa sh.1
Na Rehema Maigala, Mahakama Kuu

ALIYEKUWA Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Omari Mahita, amekata rufaa dhidi ya hukumu ya shauri la madai iliyokuwa inamkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.Mdai huyo ambaye alipeleka pingamizi zake
tatu Novemba 2010 katika Mahakama Kuu alidai kuwa malipo yamekosewa kisheria kwa sababu baba mzazi anatakiwa kulipa sh. 100 kwa mwezi na si vinginevyo.

Pingamizi jingine ni kuchelewesha kwenda mahakamani kushitaki madai ya mtoto, na jingine ni kwamba si kweli kuwa yeye (Mahita) alikataa kwenda kupima kipimo cha DNA.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na mdai Rehema Shabani akidai kupewa huduma ya mtoto wake, Juma Omari Mahita, ambaye inadaiwa kuwa alizaa na mdaiwa huyo kipindi mdai huyo alipokuwa anafanya kazi za ndani kwa mdaiwa.

Mdai huyo alidai mahakamani hapo kuwa tangu mtoto huyo azaliwe mdaiwa (Mahita) hajawahi kutoa huduma yoyote, ndipo mdai alipoamua kwenda mahakamani kufungua kesi ya madai ili mtoto wake apate huduma kutoka kwa mdaiwa.

Baada ya kesi kuendelea katika mahakama hiyo, Hakimu Suzan Kihawa alitoa hukumu kuwa mdaiwa anatakiwa kulipa sh. 100,000 kuanzia pale mtoto alipozaliwa hadi atakapoanza kujitegemea.

Vilevile katika hukumu hiyo mahakama hiyo ilimtambua Omari Mahita kuwa ni baba mzazi wa mtoto Juma Omari Mahita, hivyo anatakiwa kulipa gharama zote alizoamriwa na mahakama.

Kesi hiyo kwa sasa ipo kwa Jaji Faudh Twalibu ikiongozwa na wakili upande wa mdaiwa Semgawala na Wakili upande wa mdai, Fredrick Mkatambo, kutoka kituo cha sheria haki za binadamu.

Shauri hilo lililotakiwa kuanza kusikilizwa leo katika Mahakama kuu ya Tanzania imeahirishwa hadi Mei 18, mwaka huu kutoka na Jaji anayesikiliza shauri hilo na wakili wa mdai kutofika Mahakamani.

Hata hivyo, mdai amelalamikia kukosa ada na michango mingine ambayo jumla yake ni sh. 62,000.

No comments:

Post a Comment