Thursday, 10 March 2011

Kuzagaa kwa noti za bandia

*BoT yajisafisha

Na Stella Aron, jijini

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) limewatoa hofu Watanzania juu ya matumizi ya noti mpya na kuwashauri wananchi kuzichunguza kwa makini noti hizo kwa kutumia alama za usalama ambazo ni rahisi kuzitambua.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari leo asubuhi, kuna alama iliyofichika kwenye noti inayoonesha sura ya Mwalimu Julius Nyerere na thamani ya noti husika.

Taarifa hiyo imesema kumekuwa na wasiwasi wa kuwapo kwa noti bandia katika mzunguko wa fedha, hivyo wananchi wanashauriwa kutumia alama zilizoainishwa kwenye matangazo na vipeperushi vilivyotolewa na Benki Kuu.

Taarifa hiyo imesema namna ya kuzitambua noti halali na kuitofutisha na ya bandia ni kuwapo kwa utepe mwembamba unaoonekana kwenye noti wenye umbo la almasi ambalo hubadilika noti inapogeuzwa geuzwa upande au juu na chini.

Alama nyingine ni maalumu yenye rangi ya dhahabu yenye mchoro wa Twiga iliyoko upande wa nyuma wa noti ambayo hubadilika kuwa kijani na kurudia tena kuwa ya dhahabu inapogeuzwa.

BoT mewataka wenye maduka na biashara wanaopokea fedha nyingi kutumia taa zinazotoa mwanga wa zambarau unaojulikana kitaalamu kama 'Utra-Violet light' ili kutambua alama nyingine ambazo hujitokeza pale tu notu inapomulikwa kwa mwanga huo.

Pia wafanyabiashara hao wanashauriwa kutumia vifaa au mashine zenye uwezo wa kuhesabu na kutambua noti kwa kutumia alama zilizofichika ambazo husomeka kwa kutumia mashine hizo.

Taarifa hiyo imesema kuzagaa kwa noti bandia kwenye mzunguko siyo tatizo la Tanzania tu, kwani nchi zote duniani zimekumbwa na tatizo hili na zinaendelea kupambana nalo na kwamba tenkolojia ya vinakili vya rangi imefanya udhibiti wa tatizo hili kuwa gumu kwa nchi zote duniani.

“Kwa wale wanaoendesha uhalifu huu ni vyema wakafahamu kuwa hilo ni kosa na wakipatikana hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
 

No comments:

Post a Comment