Serikali: Rites fungasha virago nenda kwenu
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu
Serikali imeitaka kampuni ya Rites kutoka nchini India kufunga virago na kurudi kwao kwa kuwa imeshindwa kutatua suala la usafiri wa reli kama ilivyokubaliana nayo wakati inaingia ubia.
Kadhalika, Rites wametakiwa kuchukua vichwa vya treni na mabehewa yake walivyokuja navyo kwa kuwa vimeshindwa kufanya kazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, wakati akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu inayokutana kwa ajili ya vikao vyake vya kawaida.
Nundu alisema kuanzia Ijumaa iliyopita serikali ilikamilisha taratibu zote za kuvunja mkataba huo na sasa vimebaki vipengele vichache ambavyo vinapitiwa na wanasheria kabla ya kuuvunja rasmi muda wowote.
Alisema kampuni hiyo kutoka nchini India tangu ilipoingia ubia na serikali haikuwahi kufanya kazi kwa ufanisi na badala yake imezidi kufanya madudu kuliko ilivyokuwa huko nyuma kabla ya kubinafsisha shirika hilo.Waziri Nundu aliongeza kuwa kampuni ya Rites ilikuja na mtaji mdogo wa dola za Marekani milioni 10.2 fedha ambazo haziwezi kuendesha reli na kuihudumia.
Aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa ilifika mahali hata ikashindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi jambo ambalo lilikuwa ni hatari.
Alisema ili kufufua shirika hilo, serikali inahitaji Sh. bilioni 63 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu kuwezesha treni zianze kufanya kazi katika reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na mikoa mingine. bAlisema hivi sasa hali ya shirika hilo ni mbaya kwa kuwa halina treni na reli ni mbovu maeneo mengi.
No comments:
Post a Comment