Wednesday, 23 February 2011

JWTZ: Mabomu mengine yametumbukia chooni

 
Moja ya bomu lililoanguka ndani ya nyumba katika mlipuko wa mabomu uliotokea Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema linakabiliwa na changamoto kubwa katika uokotaji wa mabaki ya mabomu yaliyoangukia katika makazi ya watu kwa vile baadhi yake yametumbukia kwenye vyoo na hivyo kushindwa kuyatoa.
Mabomu hayo yalilipuka katika Kambi ya JWTZ Kikosi cha 511 KJ, iliyoko Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, Februari 16, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 26, majeruhi 512, wengine kukimbia makazi yao, uharibifu wa nyumba na mali nyinginezo zenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Kiongozi wa kikosi kazi cha kukusanya mabaki ya mabomu hayo cha JWTZ, Kanali Mushi, aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyotembelea kambi hiyo jana kuwa wanaendelea na jitihada za kuyatoa mabomu hayo na kwamba, iwapo watashindwa, watashauriana na ngazi za juu kuona nini cha kufanya.
Alisema mbali ya kutumbukia kwenye vyoo, mabomu mengine yametumbukia kwenye mashimo ya kawaida na mengine yamekwama kwenye kuta za nyumba.
“Katika ukusanyaji wa mabomu kuna changamoto. Askari wamekuta mengine yametumbukia kwenye vyoo, mashimo na kuta. Wameshindwa kuyatoa. Jitihada za kuyatoa zinaendelea. Iwapo itashindikana kuyatoa, tutashauriana na ngazi ya juu,” alisema Kanali Mushi.
Alisema uokotaji wa mabaki hayo, ulianza rasmi siku iliyofuatia baada ya milipuko kutokea na kwamba, mabomu mengi yalitua na kuathiri zaidi maeneo ya Gongo la Mboto, Majohe, Pugu Mnadani, Kinyerezi, Kwembe, Kinyamwezi, Mbezi na Mbagala.
Kanali Mushi alisema jumla ya mabomu mchanganyiko yaliyookotwa kufikia jana yalikuwa 2,204, risasi ndogo 303, fyuzi za mabomu 668 pamoja na silaha nyingine ndogondogo, ambazo hazifai tena kutumika.
Alisema kinachofanywa hivi sasa na kikosi hicho kwa awamu tatu tofauti; ni kukusanya mabaki ya mabomu, huku yaliyoingia kwenye nyumba za watu yakipewa kipaumbele; pia kukusanya yaliyotua porini; na kusafisha eneo (kambi) ilikotokea milipuko.
Awali, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, aliiambia Kamati hiyo ya Bunge chini ya uongozi wa mwenyekiti wake, ambaye ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuwa milipuko ya mabomu hayo imeleta maafa makubwa kwa askari wa JWTZ pamoja na familia zao wanaoishi katika kambi hiyo.
Mkuu wa Kikosi cha 511 KJ cha Jeshi hilo, Kanali Aloyce Mwanjile, alisema familia nane za askari na maofisa wa JWTZ hazina makazi kutokana na walizokuwa wakiishi katika kambi hiyo, kuteketea kwa milipuko ya mabomu.
Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa JWTZ, Brigedia Jenerali Paul Meela, aliiambia kamati hiyo kuwa tukio hilo lilikuwa la kutisha na kwamba, walishindwa kufika katika kambi hiyo wakati wa mabomu yanalipuka kutokana na msongamano wa watu waliokuwa wakikimbia.
Alisema wanafanya maandalizi ya kuteketeza masalia ya mabomu, huku mchakato wa kuunda Baraza la Uchunguzi ukiwa umekamilika.
Kamati hiyo pia ilitembelea waathirika, ambao nyumba zao ziliharibiwa na milipuko hiyo.
Mmoja wa waathirika, Regina Mlawa (45), alisema amefurahishwa na kutembelewa na viongozi wa serikali pamoja na Kamati ya Bunge akisema kitendo hicho ni ishara kwamba, wanawajali.
“Tangu alipokuja DC (Mkuu wa Wilaya), viongozi wetu wanatusaidia sana. Wametupatia mahema, magodoro, unga. Nimefurahi sana, inaonyesha wanatujali,” alisema Mlawa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Lowassa alisema kamati yake imeridhishwa na taarifa ya JWTZ na kuwaahidi wananchi walioathirika kuwa watafanyia kazi matatizo yanayowakabili.
Wengine waliokuwapo wakati wa ziara hiyo ya Kamati ya Bunge, ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT, Andrew Nyumayo.
Wengine ni Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, majenerali na maofisa wapiganaji wa JWTZ.

No comments:

Post a Comment