Wednesday, 23 February 2011

Mabomu ya Polisi yarindima Arusha

 
  Wawatawanya wafuasi wa Chadema
  Korti yatoa onyo wanaoingilia kesi
Polisi wa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)

Polisi wa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoa wa Arusha jana waliwapiga tena mabomu ya machozi wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakimshangilia Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwa kumuita waziri. Tukio hilo lilitokea nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa mkoa wa Arusha, baada ya mahakama hiyo kuahirisha kesi inayowakabili viongozi na wafuasi wa Chadema kwa tuhuma za kuandamana bila kibali.
Wafuasi hao walianza kumshangilia Lema kwa kumumuita “waziri, waziri” baada ya mbunge huyo anayeshitakiwa kwa tuhuma za kufanya maandamano ya Januari 5, mwaka huu.
Baada ya kuwambia wafuasi hao kuwa waungane kudai haki yao na yeye ataendelea kushikilia msimamo wake kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema uongo bungeni hadi kieleweke.
Askari hao walifyatua mabomiu matatu na kuusambaratisha umati mkubwa wa wafuasi wa chama hicho, kisha Lema akaingia katika gari na kuondoka eneo hilo.
Hata hivyo, hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa wala kukamatwa na polisi. Februari 10, mwaka huu Lema alitaka mwongozo wa Spika juu ya hatua ambazo anaweza kuchukuwa mbunge endapo atagundua kiongozi mkubwa wa serikali kama Waziri Mkuu amelidanganya Bunge.
Aliomba mwongozo huo baada ya Pinda kujibu maswali ya papo kwa papo mojawapo aliloulizwa na Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe, juu ya vurufu za Arusha za Januari 5, mwaka huu.
Mbowe alikuwa akitaka kujua kwa kuwa kumekuwa na matukio mengi ya polisi kuua raia, na hasa kuhusu suala la Arusha la Janauri 5, mwaka huu, kama serikali ilikuwa na mpango wa kuunda tume ya kimahakama kuchunguza tukio hilo, lakini pia kama Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani wangejiuzlu kutokana na kadhia ya Arusha.
Ajibu swali hilo Pinda alisema kuwa vurugu za Arusha zilisosababisha vifo hivyo zilisababishwa na ukaidi wa viongozi wa Chadema kukataa ushauri wa polisi. Kutokana na maombi ya mwongozo wa Spika, Makinda alikuwa mkali akitafsiri kuwa Lema alikuwa anamtuhumu Waziri Mkuu Pinda, kuwa kwa kauli yake bungeni alikuwa amelidanganya Bunge.
Spika Makinda akiwa ameonyesha kukerwa na kauli ya Lema, alimpa siku tano hadi Februari 14 kuwasilisha ushahidi bungeni kama Pinda alisema uongo. Hata hivyo, Jumatatu ya Februari 14, mwaka huu Lema alipokuwa akijiandaa kuuwasilisha, aliambiwa auwasilishe ofisini kwa Spika kwa maandishi.
Katika tukio la jana la mabomu, kabla ya FFU hawajafyatua mabomu, Wakili wa Utetezi wa kesi inayowakabili wafuasi 30 Chadema, Method Kimomogoro, aliiomba Mahakama kutokubaliana na ombi la upande wa mashitaka, kuhusu kusogeza mbele shauri hilo kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.
Wakili huyo alidai kuwa huo ni ujanja na kwamba inaonyesha upelelezi umekamilika kutokana na Waziri Mkuu kuzungumzia kesi hiyo bungeni.
Kimomogoro alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Charles Magesa, wakati akijibu hoja iliyotolewa na Wakili wa upande wa mashitaka, Haruna Matagane, ya kuomba kesi isogezwe mbele kutokana na kutokamilika kwa uchunguzi na kuwasilisha hati ya kuomba kibali cha kusogeza mbele kesi hiyo.
Kimomogoro alidai hakubaliani na ujanja unaofanywa na upande wa mashitaka kwani hali halisi inaonyesha uchunguzi wa kesi hiyo umekamilika kwa sababu viongozi wa juu wa serikali kama Waziri Mkuu ana ushahidi na ndiyo maana aliizungumzia bungeni ambako ni nje ya Mahakama.
“Isitoshe, tunasikia katika vyombo vya habari na kuona Polisi wakitoa maelezo juu ya mwenendo mzima wa kesi hiyo, hivyo kwa haya yote inaonyesha uchunguzi wa kesi umekamilika na inapaswa kusikilizwa,” alisema Kimomogoro.
Alisema kuwa lazima ifike mahali Mahakama ichukulie kesi hiyo kwa uzito unaostahili na kuacha kusikiliza sababu za uongo za upande wa mashitaka, kwa sababu siyo za kweli, ila zina nia ya kuchelewesha kesi.
Aidha, aliiomba Mahakama hiyo, isiiahirishe kesi hiyo, badala yake ipange tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali. “Naomba pia, upande wa Mashitaka Mawakili husika wawakumbushe viongozi wa serikalini, kuacha kuingilia shauri lililo mahakamani na kutoa matamko yanayoathiri mwenendo wa kesi hii,” alisema Kimomogoro.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa mashitaka, ambaye ni Wakili Msaidizi wa serikali, Haruna Matagane, aliiambia Mahakama kuwa Jamhuri, ndiyo inayohusika kuendesha kesi hiyo na hoja za kuwa Polisi wanatoa vielelezo vya kesi siyo za kuzisikilizwa.
“Mheshimiwa Hakimu, naomba shauri hili lisogezwe mbele kwa sababu hatujakamilisha uchunguzi wetu, pia tunaomba upokee hati ya ombi la kibali cha kusogezwa mbele kesi hii kwa sababu uchunguzi unaendelea,” alisema Matagane.
Naye Hakimu Magesa alikubaliana na hoja ya wakili wa utetezi na kutoa onyo kwa wale wote wanaozungumza kesi hiyo nje ya mahakamani. “Mahakama hii inatoa onyo kwa mtu yeyote kuacha mara moja kuzungumzia kesi iliyopo mahakamani, kwani wanaofanya hivyo wanajua wazi sheria zinakataza na hata wale wanotoa vielelezo kwenye vyombo vya habari, nao waache mara moja, kwani wanavunja sheria,” alisema. Aidha, Hakimu Magesa alikubaliana na ombi la upande wa Mashitaka, lililotolewa na wakili Matagane, kuomba kesi isogezwe mbele, na kusema kuwa anakubaliana nayo kwa mujibu wa sheria.
Hakimu huyo pia alitoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa watano, ambao ni Elisante Noel, Peter Kimario, Mathias Valerian, Walter Mushi na Peter Maruwa, kwa kosa la kutofika mahakamani hapo bila taarifa. Washitakiwa 24, wakiwemo viongozi wote wa ngazi ya Taifa wa Chadema na wabunge walihudhuria mahakamani hapo, isipokuwa Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini, ambaye ilielezwa kuwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Umati mkubwa wa wananchi ulijitokeza mahakamani hapo licha ya polisi kutanda eneo la mahakama
Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 25, mwaka huu.
Kesi hii inatokana na vurugu zilizotokea Arusha Janauri 5, mwaka huu wakati wafuasi wa Chadema walipoandamana na kufanyana mkutano wa hadhara jijini Arusha wakipinga kile walichookiita kuchakachuliwa kwa uchaguzi wa meya wa Jiji la Arusha.
Katika vurugu hizo ambazo polisi walitumia risasi za moto, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwadhibiti waandamanaji, watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

No comments:

Post a Comment