Friday, 25 February 2011

Karume aula APARC




na Mwandishi wetu
RAIS mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, ameteuliwa kuwa rais mkazi wa saba wa kituo cha utafiti na hifadhi za urithi wa marais (APARC), chenye makao yake katika Chuo Kikuu cha Boston, Marekani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mkurugenzi na balozi wa zamani wa Marekani nchini, Charles R. Stith, alisema anaamimi nafasi yake hiyo itaendeleza uhusiano baina ya Afrika na Marekani.
Stith alisema kituo hicho kimekuwa kikiwapa fursa marais wastaafu wa Afrika wakiamini kuwa wataweza kuwapa wanafunzi wa huko mbinu mbalimbali walizozitumia katika kipindi chao cha uongozi.
Alisema Karume anatarajiwa kwenda Boston mwezi Machi ambapo pia atatembelea shule mbalimbali za huko kwa ajili ya kuwafunza mambo mbalimbali.
Naye rais Karume alishukuru kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kuahidi kufikisha ujumbe kwa lengo lililokusudiwa.
Alisema akiwa huko anatarajia kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo demokrasia, haki za binadamu, afya, utawala bora, usuluhishi wa wa kisiasa na mengine mengi.
“…hili la usuluhishi wa kisiasa ndilo lengo kubwa,” alisisitiza Karume.
Karume alifafanua jingine alilofanikiwa kupitia utawala wake kama Rais wa Zanzibar kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 ni suala la afya na hasa ugonjwa wa malaria ambao kwa sasa haupo.
“Katika afya tumeshafikia malengo ya milenia mfano tumeuondoa ugonjwa wa malaria pia kuhakikisha kunakuwepo vituo vya afya kila baada ya kilomita tano,” aliongeza.


No comments:

Post a Comment