Wananchi wafukua bomu kivyao
Raia mkazi wa Kipunguni `B' Machimbo, jijini Dar es Salaam, Stanley Chinoto (29 ), kushoto, akiwa mita tatu chini ya ardhi akichimbua bomu lililozama karibu na nyumbani kwao eneo la Ukonga jijini Dar es Salaam.
Wakati serikali imetangaza kuwa kazi ya uthamini wa nyumba zilizobomoka kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea katika ghala la kuhifadhi silaha kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) KJ 511 ya Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam itaanza Jumatatu, baadhi ya wananchi wameamua kufukua mabomu ambayo yako kwenye makazi yao.
Zaidi ya wakazi 30 wa Kipunguni “B” Machimbo wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, walifukua kombora lililokuwa limejichimbia chini ya ardhi katika kisima.
Tukio hilo lililodumu takribani saa nne, lilitokea Februari 19, majira ya saa 10:30 alasiri huko Kipunguni karibu na mnara wa Tigo.
Mmiliki wa kisima hicho, Meshack Mnyambwa, alisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya askari wa JWTZ kushindwa kulifukua kombora hilo kwa siku mbili.
Mnyambwa alisema kuwa mara baada ya kupeleka taarifa za kombora hilo kuwepo katika eneo la kisima hicho, walifika wanajeshi watatu, ambao walibaini kuwa kombora hilo lilizama mita tatu ardhini na kukiharibu kisima hicho.
Aliongeza kuwa wanajeshi hao waliahidi kurudi kesho yake baada ya kushindwa kulifukua, lakini hata baada ya kurudi walishindwa kulitoa wakisema kuwa mazingira ya eneo hilo yalikuwa ya hatari kutokana na uwezekano wa kuporomoka kwa udongo.
Mjumbe wa Serikali za Mitaa Kipunguni, Sabai Sabai, alishuhudia zoezi hilo likikwama.
Mnyambwa aliongeza kuwa yeye na majirani zake waliwaita askari wengine wanne wakiongozwa na askari mwenye cheo cha Kepteni ili waende kusaidia, lakini walishindwa na ndipo wakazi wa eneo hilo walipoamua kulifukua kombora hilo katika zoezi lililokamilika majira ya saa 2:00 usiku.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wakazi hao wakiwa wamelibeba kombora hilo mabegani huku wakiimba “Tulipeleke kombora hili kwenye nyumba ya serikali” huku wakielekea katika ofisi ya serikali za mtaa na kuliacha nje ya ofisi hizo.
Akifafanua kazi ya uthamini, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, amesema kuwa utaanza kwa nyumba 75 baada ya kamati ya uhakiki wa nyumba zilizoathiriwa kukamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti kwa timu ya uthamini keshokutwa.
Sadiki alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jana katika kituo cha Kamati ya Maafa cha kupokea misaada kwa waathirika wa milipuko hiyo, kilichopo katika Ofisi za Kata ya Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Alisema kamati ya uhakiki inaanza rasmi kazi yake leo, ambapo itakwenda kwenye nyumba zote zilizoathiriwa na milipuko hiyo ili kujiridhisha kama zipo.
“Kutakuwa na watazamaji watakaohakikisha nyumba ipo na thamani yake inalingana na hasara iliyopatikana,” alisema Sadiki.
Alisema wamejipanga hivyo, ili kudhibiti wimbi la watu wasiokuwa waaminifu, ambao wanatengeneza mazingira ya kutaka waunganishwe na watu watakaolipwa fidia kutokana na nyumba zao kubomoka kutokana na milipuko ya mabomu.
Akizungumzia jaribio la utapeli huo, Sadiki alisema jana asubuhi katika eneo la Kinyerezi, kuna mtu aliyevunja nyumba yake baada ya kusikia kwamba, kuna ulipaji wa fidia unaotaka kufanywa na serikali kwa watu wote, ambao nyumba zao ziliathiriwa na milipuko ya mabomu.
Hata hivyo, alisema jaribio la mtu huyo liligonga mwamba baada ya wananchi waliomshuhudia akivunja nyumba hiyo kueleza ukweli.
“Sasa (mtu) huyo imekula kwake,” alisema Sadiki akimlenga mtu huyo, ambaye jina lake linahifadhiwa.
Alisema kumalizika haraka kwa uthamini kutategemea na ushirikiano utakaotolewa na wananchi na kwamba, iwapo (wananchi) watakuwa wadanganyifu, zoezi hilo linaweza kuchelewa kumalizika.
Kuhusu fidia za hasara ya mali za wapangaji waliokuwa wakiishi katika nyumba zilizoathiriwa na milipuko, Sadiki alisema watafikiria suala hilo.
“Maana kule Mbagala kuna mtu aliwahi kudai kuwa alikuwa na TV, lakini nyumba aliyokuwa akiishi ilikuwa haina umeme. Sasa hapo utaamini vipi kama kweli mtu huyo alikuwa na TV?” alihoji Sadiki.
Alisema hadi kufikia jana, wasamaria wema 94 waliorekodiwa kwenye kumbukumbu zao, wameshatoa misaada ya vitu mbalimbali, vikiwamo vyakula, magodoro, dawa pamoja na mavazi vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi kwa lengo la kuwasaidia waathirika.
Miongoni mwa wasamaria waliokabidhi misaada yao kwa Kamati ya Maafa jana, ni pamoja na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Khamis Mdee, ilitoa vitu mbalimbali, zikiwamo shuka katika hospitali za MOI, Muhimbili, Temeke na Amana, vyenye thamani ya Sh. milioni 6.5.
Pia Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqama kupitia Mwenyekiti wake, Seif Ally Salum, ilitoa viroba 100 vya unga, katoni 100 za maji ya kunywa, katoni 20 za tende, jozi 12 za viatu, suruali 92, mashati 92, makoti matatu, magauni 50, magodoro 100, vyote vikiwa na thamani ya Sh.13,245,000.
Wengine ni Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii kupitia Rais wake, Saudy Mwakanosya, walitoa vitu mbalimbali, vikiwamo vyakula na sabuni, vyenye thamani ya Sh. 200,000.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa, alisema fedha taslimu pamoja na zile zilizotolewa na wasamaria wema kwa njia ya hundi kwa ajili ya kusaidia waathirika, zitaelekezwa kwenye huduma za jamii, kama vile zahanati.
Alisema fedha hizo kwa sasa hazijafika kwa kamati ya maafa na kwamba, zinaendelea kuhifadhiwa kwenye Mfuko wa Taifa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
No comments:
Post a Comment