Friday, 17 December 2010

Ziara za Dk Shein Pemba

CCM Watakiwa Kufanya Tathmini Ya Kushindwa Pemba

17 12 2010
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Ali Mohammed Shein amewataka wana CCM Kisiwani Pemba kufanya tathimini ya kina juu ya chama hicho kushindwa kupata hata kiti kimoja katika uchaguzi mkuu uliomalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Dk Shein alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanaCCM katika vikao vyake ya ndani vya ikiwa ni mfululizo wa ziara yake ya kutembelea wilaya kumi za mikoa yote mitano ya Zanzibar kwa ajili ya kutoa shukurani kwa kufanikisha ushindi wa chama hicho na kumaliza uchaguzi salama.
Akizungumza na wazee na wanaCCM wa Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, Dk Shein alisema serikali ya awamu ya sita imetekeleza ilani ya chama chake vizuri lakini ameshangazwa kukosa jimbo hata moja kisiwani Pemba hivyo tathimini ya kina inahitajika kufanywa ili ijulikane sababu zipi zilizopelekea kukosekana kwa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kisiwani humo.
Alisema kutakuwa na fomu za tathmini ya uchaguzi ambazo kila mmoja atatakiwa kuzijaza na kueleza ni kwa namna gani alishiriki na kuchangia kufanikisha ushindi wa CCM huku akisisitiza waliofanya vizengwe ya kushindwa pia wasisite kuzijaza na kueleza walishiriki vipi.
“Si mambo ya kuyapuuza kama ulifanya mizengwe basi andika nilifanya mizengwe hivi na hivi mpaka CCM ikashindwa” alisema na kuacha kicheko kwa baadhi ya wana CCM waliokuwepo katika mkutano huyo ambao ulifurika wanachama wa chama hicho ndani ya ukumbi na wengine kukosa sehemu ya kukaa kwa ndani na kulazimika kuwekewa mabomba hadi nje.
Viongozi hao wametakiwa kutafakari suala hilo na kujiuliza ni kwa vipi wameshindwa kusimamia majukumu yao hadi kukosekana kiti hata kimoja kisiwani Pemba wakati wanachama wa CCM wapo wengi na wana imani kubwa na chama chao.
Aliwataka wanaCCM hao kuacha kulaumiana na kutafuta mchawi bali wajiulze wenyewe walikosea wapi na wapi panahitaji kurekebishwa ili uchaguzi utakaofuata wafanye vizuri kwa kutumia taratibu za kuvuta wanachama kwa kistaarabu na zinazokubalika chini ya demokrasia ya kweli.
Aidha waliwataka wanachama hao kufanya kazi kwa mashirikiano na kuachana na tabia ya kuachiana majukumu na kununiana kwani kufanikisha ushindi wa CCM ni kazi ya kila mmoja na sio watu fulani kama inavyondaniwa na baadhi ya wanachama kwamba viongozi pekee ndio wenye jukumu la kufanikisha ushindi katika uchaguzi.
“Tunamlaumu nani kama wenyewe hamjataka kumpa kura mgombea wenu tena yeye atafanya nini? Au kwa kuwa mtu hajakupa kura ndio unune? “ alihoji Dk Shein
Hata hivyo amewataka wanachama wa CCM Kisiwani Pemba kutokuwa wanyonge kwa kukosa viti kwani kura zilizopatikana kisiwani humo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kushindwa kiti cha urais hivyo amewataka kuendelea kukiunga mkono chama hicho na kujipanga vizuri ili katika chaguzi zijazo kishinde nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kisiwani humo.
Dk Shein amemalika ziara yake ya mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba na leo atapokelewa na kwa maandamano makubwa yaliotayarishwa na jumuiya ya kina mama ya chama cha mapinduzi Zanzibar na baadae kuhutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kisonge Mjini Unguja.


No comments:

Post a Comment