Friday, 17 December 2010

Sio Lazima Kupokea Ushauri Ninaopewa-Dk Shein




17 12 2010
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein amesema anakhiari kupokea au kukataa ushauri wowote atakaopewa na watendaji wake wakuu wa serikali ikiwa hautokuwa na manufaa katika serikali yake.
Dk Shein ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wana CCM Kisiwani Pemba katika mfululizo wa ziara yake ya mikoa mitano ya Zanzibar kwa lengo la kuwashukuru wana CCM kwa kushiriki uchaguzi mkuu kwa salama na kukipatia ushindi chama hicho.
Alisema anaongoza serikali ya mapinduzi Zanzibar iliyo chini ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa mfumo ambao umechaguliwa na wazanzibari wenyewe katika kura ya maoni kwa kuungwa mkono kwa asilimia 66.4 hivyo amelazimika kuchagua makamu wa kwanza na wa pili wa rais pamoja na baraza lake lenye uwiano sawa kutoka vyama vya CCM na CUF.
Yeye ndiye rais wa Zanzibar amesema na ana wasaidizi wawili ambao wanatoka vyama tofauti ambao ni washauri wake wa karibu katika kuendesha shughuli zote za serikali pamoja na baraza lake la mawaziri ambalo lenye sura mbili tofauti kwa hivyo ana hiari kupokea ushauri atakaopewa.
“Watu wana wasiwasi sana lakini mimi ndio rais wa Zanzibar hapa na Maalim Seif ni makamu wangu wa kwanza wa rais ambaye ni mshauri wangu lakini kwenye ushauri kuna kushauriwa ukakubali na kushauriwa ukakataa au sivyo?” alihoji Dk Shein.
Kauli ya Dk Shein imekuja kumaliza tetesi na minongono miongoni mwa wana CCM wenye wasiwasi na utendaji wa serikali yenye vyama viwili na sera tofauti ambao baadhi yao walikuwa na khofu na utendaji kazi wa Maalim Seif ambapo Dk Shein mwenyewe aliwatoa khofu kwa kuwaeleza kwamba yeye na makamu wake wote wawili wanafanya kazi kwa uaminifu na unyenyekevu mkubwa.
Sambamba na hilo Dk Shein aliwaambia wana CCM katika vikao vyake hivyo vya ndani watoe mashrikiano na msaada wa hali ya juu na mawaziri wake wote bila ya kujali huyu anatoka chama gani kwani kufanya hivyo kutasaidia kuleta maendeleo na kuondosha chuki miongoni mwao na wananchi wote wa Zanzibar.
“Tunafanya kazi kwa uaminifu mkubwa sana na tuminiana na hilo ndio jambo kubwa linalotakiwa mimi na makamu wangu wote wawili na baraza langu la mawaziri tunafanya kazi kwa kwa vizuri na mashirikiano, kwa unyenyekevu kabisa na hakuna waziri wa CUF wala wa CCM wale wote ni mawaziri wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar…muwape mashirikiano makubwa na sitaki kusikia mmembagua eti huyu wa CUF huyu wa CCM hapana…” alionya Dk Shein.
Dk Shein aliwahakikishia wan CCM hao kwamba anafanya kazi vizuri chini ya wasaidizi wake wawili ambao ni makamu wa kwanza Maalim Seif Sharif Hamad na wa pili Balozi Seif Ali Iddi na baraza lake la mawaziri anaamini watakwenda vyema kwa uwezo wa mwenyeenzi mungu kwani kufanya kazi kwa mashirikiano na umoja ndio lengo la serikali yake.
“Mimi ndio rais na nina washauri wakuu ambao nimewateuwa mimi sio wao wamejiteuwa wenyewe na mawaziri nimewapataje nimeteuwa kwa mujibu wa katiba ilivyonielekeza na kwa nini nimeunda baraza la mawaziri lenye wizara 16 najua mwenywe, hakuna anayeweza kunizuwia, kunihoji na wala kunishitaki. ..mwenyewe nakhisi zinatosha na naweza kubadilisha wakati wowote” alisema Dk Shein kwa kujiamini.
Aidha aliwamwagia sifa mawaziri wake akisema wamejipanga vizuri na wanafanya kazi kwa ari na ufanisi mkubwa huku kila mmoja akijua wajibu wake wa kuwatumikia wananchi bila ya upendeleo na kuwataka wananchi wakiwemo wana CCM kuiunga mkono serikali yao na kuipa mashirikiano na kuondosha tofauti zilizokuwepo huko nyuma kwani kufanya hivyo ni kuleta umoja na mshikamano na maendeleo.
“Mawaziri wangu wamekula kiapo kuwa watatetea katiba na hawatatoa siri za baraza la mapinduzi hivyo naamini kama wamekula kiapo watafanya kazi vyema na wameanza vizuri sana wanafanya kazi na serikali licha ya kuwa wana vyama vyao lakini hawapendelei mtu, wanajituma sana na kila mmoja anataka aonekane anafanya vizuri kuliko mwenzake na makamu wangu wote wawili ni watu makini sana wote watiifu kwangu na waaminifu tunafanya wajibu wetu na tumejipanga vizuri sote kwa pamoja”alisema Dk Shein kuwaeleza wana CCM.


No comments:

Post a Comment