Wednesday, 22 December 2010

Umeme waiweka serikali pabaya


•  CHADEMA kufanya maandamano nchi nzima kupinga bei mpya

na Mwandishi wetu


banner


KUKOSEKANA kwa umeme wa uhakika na kupandishwa kwa gharama za nishati hiyo hivi karibuni kunaiweka serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika shinikizo kali la kupingwa na umma wa Watanzania nchi nzima ukiongozwa na chama kikuu cha upinzani – CHADEMA.
CHADEMA jana ilitangaza msimamo mkali wa kufanya maandamano nchi nzima wenye lengo la kuhamasisha na kuwaongoza wananchi wote kupinga ongezeko kubwa la gharama za umeme ikiwa serikali haitatengua haraka gharama mpya za kutumia nishati hiyo zilizotangazwa hivi karibuni.
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini nchini (EWURA) juzi ilitangaza kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 18.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho zilizopo Kinondoni mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Erasto Tumbo, alisema kiwango hicho ni kikubwa mno kwa wananchi wa kawaida.
Alisema ni vema gharama hizo za umeme zingebebwa na serikali kwa sababu yenyewe ni moja ya taasisi zinazolimbikiza madeni sugu ya TANESCO hivyo kulifanya shirika hilo kushindwa kujiendesha.
“Kulingana na kipato cha wananchi wengi wa kawaida kuwa cha chini ongezeko hilo la asilimia 18 linakuwa mzigo mwingine mzito unaokuja kuyakandamiza maisha ya wananchi wa kawaida,” alisema Tumbo.
Aliitaka serikali kusitisha haraka ongezeko hilo kwani litawaongezea wananchi machungu ya maisha.
“Tunaiomba serikali isitishe ongezeko hili na kama itashindwa CHADEMA tutaitisha maandamano ya amani nchi nzima kupinga ongezeko hilo,” alisema Tumbo.
Alisema kwa kuwa serikali ndiye mdaiwa sugu wa TANESCO ni vema ikaweka wazi inadaiwa kiasi gani na shirika hilo pamoja na madeni ya vigogo na taasisi nyingine badala ya kukimbilia kuutua mzigo huo kwa wananchi ambao wengi hawana uwezo wa kumudu gharama mpya za umeme zilizotangazwa.
Kupandishwa kwa gharama hizo kunaweza kuwa ni mpango wa serikali wa kulipa deni la Dowans ambalo waliamriwa kulilipa na Mahakama ya Biashara ya kimataifa hivi karibuni.
CHADEMA pia imeishutumu TANESCO kwa tabia yake ya kupenda kujitangaza kila kukicha kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari wakati bado inashindwa hata kuboresha huduma zake.
Wakati CHADEMA ikitoa msimamo huo jana hiyo hiyo serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ilitangaza kuridhia kupanda kwa gharama zilizotangazwa na Ewura.
Ngeleja alisema kupanda kwa bei ya umeme hakuna uhusiano wowote na suala la kutafuta pesa ili kulipa deni la sh bilioni 185 ambalo TANESCO inadaiwa na kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans.
Serikali imewataka wananchi kukubali gharama hiyo ili kulifanya shirika hilo kupata pesa kwani limekuwa likijiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Ngeleja alitoa msimamo huo jana alipokuwa katika ziara ya kikazi kwenye ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
“….. TANESCO linajiendesha lenyewe na halitegemei ruzuku yoyote toka serikalini. Katika kupanda kwa bei ya umeme tunajua wananchi ndio wanaoumia kwa hilo, lakini hatuwezi kumfurahisha kila mtu…bei wanazotoza haziendani na gharama halisi za uendeshaji.
“Kwa hili lazima wananchi waelewe juu ya kupanda kwa gharama hizo, wote ni wa hapa hapa, suala sio kubinafsisha shirika bali kutafuta njia ya kutatua tatizo,” alisema Waziri Ngeleja.
Katika maelezo yake Ngeleja alisema gharama za umeme kwa wateja hapa nchini ziko chini ikilinganishwa na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema mwaka 2006 shirika lilipata hasara ya sh bilioni 168 na mwaka jana ilipoteza sh bilioni 5 kama hasara.
“Nchi inakosa umeme wa uhakika kwa sababu mbalimbali ikiwemo miundombinu mibovu na zingine; ambapo maombi ya kupandisha gharama hizo kwa Ewura ni ya msingi ingawa wananchi wanalalamika,” alimalizia Ngeleja.

No comments:

Post a Comment