Liyumba akwaa kisiki, arudishwa gerezani
Aliyekuwa mklurugenzi wa utumishi na utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba (wa pili kushoto) akisindikizwa na askari magereza mara baada ya uamuzi wa mahakama kuu wa kutupilia mbali rufaa yake jana.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali rufaa iliyokatwa mahakamani hapo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, kupinga hukumu ya miaka miwili jela iliyotolewa dhidi yake baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.
Kutokana na uamuzi huo, Liyumba (62) alirejeshwa jela jana kuendelea kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani alichohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam Mei 24, mwaka huu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Emilian Mushi akikubaliana na hukumu iliyotolewa na mahakimu wawili waliokuwa katika jopo la mahakimu wakazi watatu wa mahakama hiyo (Kisutu) waliosikiliza kesi ya msingi iliyokuwa ikimkabili Liyumba.
Jopo la mahakimu hao liliongozwa na Hakimu Edson Mkasimongwa. Mahakimu wengine waliounda jopo hilo, walikuwa ni Lameck Mlacha na Benedict Mingwa.
Hata hivyo, ilipofika hatua ya kutoa hukumu, jopo hilo liligawanyika makundi mawili na kuandika hukumu mbili tofauti ya kesi hiyo.
Hukumu moja, ambayo iliandikwa na Hakimu Mkasimongwa, ilimuachia huru Liyumba kwa maelezo kwamba, hakimu huyo alibaini ushahidi wa upande wa mashtaka unaning’inia.
Hukumu ya pili iliyoandikwa na mahakimu Mlacha na Mingwa, ilitoa adhabu dhidi ya Liyumba ya kutumikia kifungo hicho. Hukumu zote zimehifadhiwa kwenye kumbukumbu za mahakama hiyo.
Jana katika uamuzi wake, Jaji Mushi alisema athari ya kosa lililotendwa na Liyumba, si tu kwamba liliiathiri Bodi ya Wakurugenzi wa BoT, bali liliathiri pia uendeshaji wa shughuli za benki hiyo pamoja na uchumi wa taifa kwa jumla.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mushi alisema sababu zilizotolewa na mahakimu hao wawili kuhusu adhabu iliyotolewa dhidi ya Liyumba, ni sahihi.
Liyumba aliwasilisha rufaa hiyo namba 56 ya mwaka huu, katika mahakama hiyo kupitia mawakili wake; Majura Magafu, Onesmo Kyauke, Jaji Mstaafu Hillary Mkate na Hudson Ndusyepo.
Alitaja sababu 12 kupinga hukumu iliyotolewa na mahakimu hao wawili; ya kwanza ikiieleza kuwa Mahakama ya Kisutu ilishindwa kuchambua ushahidi uliotolewa mahakamani kikamilifu na matokeo yake jopo hilo la mahakimu wakazi watatu likajikuta linatoka na hukumu mbili tofauti.
Sababu nyingine, alidai mahakimu hao wawili walifanya makosa kwa kushindwa kukubali kwamba, mabadiliko ya mradi wa ujenzi wa minara pacha ya BoT, yalifanywa baada ya Meneja Mradi huo, Deogratius Kweka kuketi kwenye kikao na timu ya wataalamu wa ujenzi na kujadili shughuli za mradi huo.
Alidai ushahidi uliokuwapo kwenye rekodi za mahakama, hauonyeshi Liyumba alikuwa akihudhuria kwenye kikao hicho cha wataalamu wa ujenzi wa mradi.
Sababu nyingine; alidai mahakimu hao wawili walifanya makosa kwa kushindwa kukubali kwamba, shughuli zote za uendeshaji wa mradi ule zilikuwa chini ya Meneja Mradi, Kweka, ambaye alikuwa akiwajibika moja kwa moja kwa Gavana na si kwake (Liyumba).
Alidai sababu ya nyingine; alidai mahakimu hao wawili walifanya makosa kwa uamuzi wao wa kuutupilia mbali ushahidi uliotolewa naye na shahidi wake, ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa BoT, Bosco Kimela kwa maelezo kuwa mashahidi wote walikuwa wakiishi pamoja katika gereza la Keko.
Sababu nyingine, alidai Mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema malipo ya mradi huo yalikuwa yakiidhinishwa na Liyumba akidai kwamba hoja hiyo haikuwa ya kweli kwani ni kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama, hauonyeshi Liyumba alikuwa akiidhinisha malipo ya mradi huo na kuhoji wapi mahakimu hao walikopata ushahidi huo?
Alidai sababu nyingine; Mahakama ya Kisutu ilifanya makosa kusema Bodi ya Wakurugenzi wa BoT ilipoteza mwelekeo na kwamba, Liyumba na aliyekuwa Gavana wa BoT, Daud Balali walikuwa wakiiburuza bodi.
Sababu nyingine; alidai mahakama hiyo ilifanya makosa kwa kushindwa kufuata taratibu zilizoainishwa kisheria katika kutoa adhabu.
Hata hivyo, katika hukumu yao, mahakimu hao wawili, walipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba, kulingana na hali ya rushwa iliyokithiri kwa watumishi wa umma nchini, adhabu iliyofaa kwa Liyumba ilikuwa ni kifungo cha jela.
Hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa Liyumba wakidai kwamba, kauli hiyo ya mahakimu hao ilikuwa ni maneno ya kisiasa.
Liyumba alituhumiwa kutumia nafasi yake alipokuwa BoT kuongeza mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo yaliyoko jijini Dar es Salaam kutoka ghorofa 14 hadi 18, jambo lililosababisha kuongeza gharama za mradi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment