Waziri wa Nchi, ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia alimshukuru
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa ofisi yake iko tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kuhakikisha Muungano unaendelea kuimarika maana ofisi yake iko kwa ajili ya kumsaidia Rais wa Zanzibar katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kuimarisha Muungano
Mhe. Maalim Seif Hamad amesema hayo leo jioni wakati akiongea na Waziri wa Nchi, ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia Suluhu Hassan alipomtembelea Makamu huyo wa kwanza Rais ofisini kwake Zanzibar katika ziara ya kujitambulisha.
Maalim amesema anatambua umuhimu wa kuwepo kwa Waziri mwenye dhamana ya kushughulikia masuala ya Muungano kutokana na changamoto kubwa zilizopo katika ofisi hiyo ila ana imani kwa uwezo alionao Mhe. Samia ataweza kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya pande mbili za Muungano pamoja na kuendelea kutatua kero mbalimbali ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi mpaka sasa.
“Ninajua jukumu lako hasa ni kumsaidia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kushughulikia masuala ya Muungano ambayo yana changamoto kubwa, hivyo hunabudi kuhakikisha unajenga mahusiano mazuri baina ya wizara na Taasisi za Muungano na zisizo za Muungano ili kuondoa mvutano na kuleta maelewano kwa njia ya vikao vya pamoja” alisema Maalim.
Amesisitiza kuwa kero za muungano zilizopo zizungumzwe kwa uwazi kabisa ili kuleta suluhu, akiamini kuwa endapo watazungumza kwa uwazi mambo mengi yatapatiwa ufumbuzi wa haraka hali ambayo itapunguza muda wa majadiliano ya kutatua suala fulani. Aidha, alishauri ni vyema kwa masuala ambayo yalishafanyiwa maamuzi yaendelee ketekelezwa.
Alimalizia kwa kuunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutaka vikao vile vya Makamu wa Rais na kamati yake vya kujadili masuala ya Muungano viendelee kukaa hata kama havina kero ya kuzungumza lakini kukaa kwao kutaboresha mahusiano ya pande mbili na kuondoa mikinzano isiyokuwa ya lazima.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Mhe. Samia alimshukuru Makamu huyo wa kwanza wa Rais, na kusema kuwa ofisi yake imejipanga vyema kuhakikisha inaratibu vizuri masuala ya Muungano kwa kushirikiana na wizara husika ili kuendelea kupatia ufumbuzi changamoto zilizopo.
Aidha, amesema ofisi yake inajaribu kubuni njia ya kuhakikisha vijana wanapatiwa nafasi ya kuelimishwa kuhusu Muungano maana miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili ofisi yake ni uelewa wa vijana kuhusiana na Muungano hasa ukizingatia vijana wengi wamezaliwa baada ya Muungano.
“ofisi yangu inajaribu kubuni njia mbalimbali za kukutanisha vijana wa pande zote mbili ili kupata nafasi ya kujifunza na kuujua Muungano iwe kwa midahalo, vipindi vya radio, ziara na michezo tukishirikiana na sekta binafsi kuona namna sekta hizo zitakavyoweza kusaidia gharama mbalimbali ili kufanikisha jambo hili” alisema waziri.
Waziri huyo wa Muungano ambaye, ameambatana na baadhi ya wataalamu kutoka ofisini kwake yuko katika ziara ya kikazi Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha katika wizara mbalimbali, ambapo leo ameanzia ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, waziri huyo kesho ataendelea na ziara yake ambapo anatarajia kukutana na Makamu wa Pili wa Rais, Pamoja na Mawaziri wa wizara nyingine na siku ya Ijumaa anatarajia kukutana na Waandishi wa habari.
Habari hii imeandikwa na Riziki Abrahamu