Saturday, 25 December 2010

Taarifa za faragha zaanikwa, vigogo wakana

Mkapa amponza Kikwete

Mwandishi Wetu



KASHFA dhidi ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, sasa zimeanza kusambazwa kimataifa baada ya kuguswa na mtandao wa Wikileaks unaovujisha taarifa za mazungumzo ya faragha kati ya maofisa wa balozi za Marekani na vigogo wa nchi mbalimbali duniani.
Mkapa tayari ametajwa kama mtu anayelindwa na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, ili asichukuliwe hatua za kisheria kuhusu madai ya ufisadi katika kujimilikisha mgodi wa makaa ya Kiwira, ambao baadaye ilibidi utwaliwe na Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Wikileaks unaomilikiwa na raia wa Australia, Julian Assange, Kikwete anatajwa kama Rais aliyepania kulinda madai ya ufisadi unaomhusu Mkapa.
Wikileaks wanataja chanzo cha taarifa hizi kuwa ni kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Edward Hosea, katika mazungumzo yake na ofisa ubalozi wa Marekani yaliyorekodiwa na kuvujishwa kwa mtandao huo unaowatia homa wanadiplomasia wengi duniani.
“Rais Kikwete anasita kumchukulia hatua Rais wa zamani, Benjamin Mkapa, au baadhi ya watu wake wa karibu katika kashfa za rushwa,” Hosea ananukuliwa akimweleza kwa faragha ofisa huyo wa ubalozi Marekani aliyetajwa kwa jina la Purnell Delly.
Taarifa hizi zilizovuja kuhusu Kikwete kutaka kumlinda Mkapa na wastaafu wengine katika kuwafikisha mahakamani kwa tuhuma za ufisadi, zimewahi kuzungumziwa na Kikwete binafsi katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari katika awamu yake ya kwanza, Ikulu Dar  es Salaam.
Katika mkutano huo, Kikwete alisema si busara kuendelea kuwaandama wazee (marais wastaafu) na kwamba ni vema wakaachwa wapumzike. Kati ya kashfa anazohusishwa nazo Mkapa ni mradi wa makaa ya mawe Kiwira, akitajwa kwa namna fulani kushirikiana na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.
 Mkapa binafsi aliwahi kuzungumzia sakata hilo Mei mwaka huu, akisema tuhuma hizo ni maneno ya watu na kwamba wameyazua kwa manufaa yao. Hakueleza iwapo baadhi ya nyaraka zilizomhusisha na ufisadi huo, zikiwa na sahihi yake na anwani ya Ikulu zilikuwa ni za kughusi au halali.
Kuhusu kashfa ya kujiuzia mgodi wa makaa ya mawe kwa bei chee alijibu akisema: "Hayo ni maneno ya watu; wameyazusha kwa manufaa yao wenyewe.” Alitoa majibu hayo kwa waandishi wa habari na kusisitiza kutokuwa na hisa kwenye mgodi huo ambao sasa tayari umetwaliwa na Serikali.
"Sijui kwa sababu gani... na mimi nashangaa. Hata nyinyi wana habari mmeandika sana hayo, lakini nasema sina ‘share’ (hisa) katika mgodi wa Kiwira, alisema, na kusisitiza : “Mmeandika sana hayo, nasema sina share Kiwira, ninyi nendeni mkasome vizuri,”
"Kama ule ulikuwa mradi wa kuzalisha umeme, cha kuuliza hapa uliishia wapi; ulizeni; mimi sina share yoyote Kiwira," alisema Mkapa.
Mkapa amekuwa katika kashfa ya kuhusishwa na umiliki wa mgodi huo akishutumiwa kwa kujiuzia kwa bei ya chee kinyume cha thamani yake halisi akishirikiana na mkewe Anna pamoja na Daniel Yona.
Sakata hilo la umiliki wa mgodi wa Kiwira lilisababisha baadhi ya wabunge wa Bunge la tisa kupendekeza aondolewe kinga ili afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Wabunge hao ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, aliyelifikisha sakata hilo bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na kudai Mkapa, kwa kushirikiana na mkewe, pamoja na Daniel Yona mwaka 2004, walianzisha kampuni ya TanPower Resources Ltd na mwaka mmoja baadaye wakauziwa mgodi huo kwa kificho.
Kimaro alidai ingawa thamani ya mradi huo ilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni nne, iliridhiwa mgodi huo kuuzwa kwa Tanpower Resources kwa shilingi milioni 700, lakini akadai kubwa zaidi  ni kwamba kiasi kilicholipwa na Mkapa na washiriki wake kilikuwa ni shilingi milioni 70 tu. Aliongeza kudai kuwa mwaka 2006 Mkapa, Anna na Yona, waliingia mkataba wa kufua umeme na TANESCO kwa makubaliano ya kulipwa sh milioni 46 kila siku, pasipo kujali kama umeme umefuliwa ama la.
Jumanne wiki hii magazeti ya hapa nchini yaliandika habari ikinukuu ile iliyochapishwa katika gazeti la The Guardian la Uingereza, zikihusu sehemu ya taarifa za Wikileaks.
Katika habari hizo, imeelezwa kuwa Dk. Hosea ameueleza ubalozi wa Marekani nchini kuwa Rais Kikwete anasita kuwachukulia hatua vigogo wakubwa wa rushwa, ikiwamo walioshiriki katika ununuzi wa rada ya kijeshi kwa bei kubwa.
Hosea pia ananukuliwa kueleza kuwa maisha yake yako hatarini na kwamba mara kwa mara amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa vigogo wanaohusika na kashfa za ufisadi.
Mbali na Hosea kutajwa ‘kumkaanga’ Kikwete kwa Wamarekani, pia anadaiwa kumtaja Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume kuwa ni kati ya vigogo wanaohusika katika rushwa, sambamba na baadhi ya maofisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Kutokana na taarifa  hizo kutikisa wakubwa nchini, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, amenukuliwa akisema Kikwete ametekeleza kwa vitendo mapambano dhidi ya rushwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi na inapostahili amepewe pongezi.

No comments:

Post a Comment