Monday, 6 December 2010

ROBO FAINALI CHALENJI






 Kili Stars, Zanzibar Heroes vitani kesho


•  Zambia, Ethiopia, Malawi, Ivory Coast leo

na Dina Ismail

WAKATI robo fainali ya kwanza ya michuano ya Chalenji inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo kwa Zambia kukipiga na Ethiopia, macho na masikio ya mamilioni ya Watanzania ni kesho ambapo timu zake zote za bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Zanzibar Heroes zitakuwa zikitupa karata zao. Mbali na mechi kati ya Zambia na Ethiopia leo hii pia kutafanyika mchezo kati ya Ivory Coast na Malawi.
Kesho itakuwa mshikemshike ambapo Stars inayonolewa na Mdenish Jan Paulsen itashuka Dimba la Taifa kuumana na Rwanda ‘Amavubi’, mechi inayotabiriwa kuwa na ushindani mkubwa hasa ikizingatiwa timu zimekutana hivi karibuni na zinajuana, wakati Zanzibar chini ya Muingereza Hall Stewart itakuwa na kibarua kigumu mbele ya mabingwa watetezi Uganda ‘The Cranes’.
Mechi ya Kilimanjaro Stars na Amavubi itatanguliwa na ile ya Zanzibar na Uganda.
Katika hatua hii ya robo fainali, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limebainisha kuwa mshindi atapatikana katika dakika 90.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema kwamba katika hatua ya nusu fainali itakayorindima Ijumaa, iwapo mshindi hatopatikana katika dakika 90, zitaongezwa 30.
Alisema, maandalizi kwa ajili ya hatua zote za michuano hiyo itakayofikia tamati Jumapili ijayo yamekamilika, huku akisifu umahiri na nidhamu ulioonyesho na baadhi ya timu shiriki na matokeo yake kutinga hatua hiyo.
Wakati huo huo, mwandishi Juma Kasesa anaripoti kuwa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mechi hizo hadi hatua ya nusu fainali, ambapo kiwango cha juu kitakuwa ni sh 5,000 huku cha chini kikiwa ni sh 1,000.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni, alisema, viingilio hivyo vimewekwa ili kuwawezesha mashabiki na wadau wa soka kumudu kuingia uwanjani.
Katika viingilio hivyo mashabiki watakaokaa jukwaa la kijani na bluu watalipa sh 1,000, Machungwa sh 2000, VIP C 3,000, VIP D 3,000 na VIP A itakuwa sh 5,000.
Aidha, Kayuni aliwatahadharisha mashabiki watakaokaa jukwaaa la VIP D, kuepuka kufanya vurugu na vitendo vingine visivyo vya kistaarabu, kwa kuwa eneo hilo limetengwa kwa ajili ya waandishi wa habari, waamuzi na wachezaji wa timu mbalimbali zinazoshiriki michuano hiyo mikongwe barani Afrika.
Mshindi katika michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya bia ya East African Breweries Limited (EABL), kupitia kampuni tanzu ya Serengeti Breweries (SBL) chini ya bia ya Tusker atazawadiwa dola 30,000 wakati mshindi wa pili atapata dola 20,000 na mshindi wa tatu atapata dola 10,000.

No comments:

Post a Comment