| na Mauwa Mohammed, Zanzibar |
| MAKAMU wa pili wa rais na Mbunge wa Kitope, Balozi Seif Ali Iddi, ameonya watu wanaotumia nyadhifa zao kudhulumu ardhi za wananchi au kukiuka taratibu za ugawaji wa ardhi nchini. Onyo hilo alilitoa juzi huko Kitope wakati akihutubia Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo hilo wenye lengo la kuwashukuru wananchi baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika Julai 31 mwaka huu na kuwapongeza viongozi wote walioshinda katika nafasi walizoomba. Balozi Seif aliwataka watendaji wa ngazi zote zilizohusika kugawa ardhi kinyume cha taratibu wakiwemo masheha, watendaji wa halmashauri na wengineo kuachana na tabia hiyo na kurejesha fedha walizouzia mara moja za maeneo na kufuta nyaraka walizozitoa. “Serikali ya Zanzibar imeliona hilo la ardhi, wananchi wananyang’anywa ardhi hovyo au heka zao bila ya kufuata taratibu za kisheria au idhini ya wamiliki kama viwanja vya michezo na maeneo ya wazi,” alisema balozi Iddi. Alisema iwapo watendaji hao hawatatekeleza agizo hilo watafukuzwa kazi na serikali itaendelea kuwatumikia wananchi kwa manufaa yao na sio kuendekeza tamaa za watumishi wanaofanya mambo kwa maslahi binafsi. Aliwataka masheha na maafisa ardhi kufanya kazi kwa kufuata taratibu na kuonya kwamba hatovumilia kumuachia yeyote ambaye atahusika na uharibifu wa utoaji wa ardhi ya serikali bila ya kufuata taratibu kwani kwa muda mrefu wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamikia maeneo yao kuchukuliwa bila ya taratibu husika. |
No comments:
Post a Comment