Saturday, 18 December 2010

Pinda apinga hoja ya Waziri Sitta

Imeandikwa na Mwandishi Wetu;
KAULI za Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Nape Nnauye, ikiwamo ya kuitaka serikali kutolipa fidia ya kushindwa kesi kati ya Kampuni ya Dowans dhidi ya Tanesco, zimepingwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Pinda amesema, Tanzania inafuata sheria katika utawala bora.

Sitta alikuwa Spika wa Bunge,wiki iliyopita alikaririwa akisema kuwa, serikali haipaswi kuilipa Dowans fidia hiyo ya Sh bilioni 185, kwa madai kuwa ni njama za baadhi ya watu aliodai wanaitafuna nchi na waliokosa uzalendo na kulituhumu Baraza la Usuluhishi lililotoa hukumu hiyo, akiihusisha na ukosefu wa uadilifu.

Kwa upande wake, Nape aliyeteuliwa Oktoba mwaka huu kuwa Mkuu wa wilaya hiyo katika mkoa wa Mtwara, alikaririwa akisema ni vyema Watanzania wakaandamana kupinga fidia hiyo ya Dowans ambayo kiini chake ni mkataba wa Kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Corporation.

Lakini jana, Waziri Mkuu Pinda alizipuuza kauli zote mbili hizo za watendaji wake akisema Tanzania ni nchi inayofuata utaratibu wa sheria, kwa hiyo, katika kushughulikia suala hilo, imelipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya msaada wa kisheria na hatua za kuchukua.

“Kwa mambo ya kisheria, ni muhimu mkafuata sheria, hatuendi namna hiyo (walivyoshauri Sitta na Nape). Huyu anasema ooh, jaji katuonea, tusilipe. Nikamsikia DC wangu mmoja naye anasema tuandamane. Hatuendi hivyo. Hayatatusaidia,” alisema Waziri Mkuu.

"Katika utawala wa sheria, unachambua mambo ya msingi kwa mujibu wa taratibu, kama haiwezekani mliboronga, mnafanyaje? Eeh, tukatafute fedha tulipe? Tumekwama, tusitupiane mpira.”

Alifafanua kwamba, hakuna sababu ya kusaka mchawi sasa kwa sababu suala la kuvunja mkataba wa Dowans liliamuriwa na Bunge na kila mtu anafahamu hivyo, na kwamba kilichotokea ni ‘tembe chungu, lakini hatuna budi kuimeza’, na kama kuna makosa yametokea, ni vyema kukiri makosa hayo.

Alisema, alimwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuzungumza naye kuhusu suala hilo na ushauri wa mwanasheria huyo ni kwamba ataipitia hukumu baada ya kuipata na kitakachofuata ni kuishauri serikali namna bora ya kuchukua hatua baada ya fidia hiyo kubwa kuwahi kutolewa dhidi ya serikali.

Alisema, serikali imechukua hatua ya kumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu fidia hiyo imetolewa dhidi ya Tanesco, ambayo ni taasisi ya umma, na hakuna shaka, maamuzi hayo yataigusa serikali katika hatua kadhaa za utekelezaji wake iwe ni kulipa fidia au la.

No comments:

Post a Comment