Maaskofu waja juu Mahakama ya Kadhi |
*Wadai waanzishe kwa fedha zao *Waionya Serikali Na John Daniel MAASKOFU wameitaka Serikali kuzika mara moja suala la Mahakama ya Kadhi na kuagiza Bunge kutojadili suala hilo kwa kuwa lina madhara kwa umoja na mshikamano wa Taifa.Wakizungumza Dar es Salaam jana, Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wamesema kwa mujibu wa Katiba, Serikali au Bunge kujadili Mahakama ya kadhi ni kosa. “Tukiona mambo yanaenda visivyo na sisi tukakaa kimya tutakuwa tunafanana na hao wanaoharibu. Suala la Mahakama ya Kadhi ni la kidini na kamwe halipaswi kuihusisha Serikali au Bunge,” alisema Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa la Anglikana. Askofu Mokiwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCT alisema kimsingi suala la Mahakama ya Kadhi inapaswa kuwa la dini husika na si kuihusiha Serikali kwa maana ya kutumia kodi za Watanzania kuishuhulikia. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Peter Kitula, alisema Serikali ilifanya makosa kujiingiza katika suala hilo wakati Katiba imeweka wazi kuwa hiyo siyo kazi yake. Naye mjumbe wa Tume ya CCT Askofu Askofu Owdenburg Mdegella, alisema nchi inatakiwa kuendeshwa kwa mfumo ulioweka kisheria mama na si vinginevyo.Maaskofu hao waliweka wazi kushtushwa na hali ya udini iliyojitokeza nchini hususan wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita na kuitaka Serikali kurekebisha makosa hayo. Walisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitambua hatari ya Serikali kujihusisha na siasa hivyo kutengansha suala hilo na uongozi wa nchi. Walisema Serikali imekaa kimya wakati suala la udini likiachwa liendelee kushamiri katika jamii, lakini madhara yake ni makubwa zaidi. Waliwataka wabunge pia kuwa makini na kutokubali kupokea malipo ya kodi za wananchi kwa kujadili masuala ya kidini. |
No comments:
Post a Comment